Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

UBORESHAJI wa vifungu kinzani vya sheria ya habari utaiwezesha tasnia hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuchangia kuchochea maendeleo ya sekta hiyo na hata taifa kwa ujumla.

Matumaini makubwa yatapatikana endapo muswada wa maboresho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 utawasilishwa bungeni Novemba,mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja Menyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile amesema kuwa ni miezi kadhaa sasa imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo kuhusu sheria za habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kuminya uhuru wa vyombo vya habari nchini kufanyiwa maboresho.

“Nimeelekeza sheria zirekebishwe, lakini kwa majadiliano pande zote na si tu kwamba sisi tunataka nini.Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote,”aliagiza Rais Samia.

Agosti 11 na 12, mwaka huu, wadau wa habari walikutana na Serikali,walijadiliana na kuelezana kuna vifungu vinavyohitaji marekebisho.

“Ndio maana hatuamini kwamba muswada utapelekwa bungeni Februari mwakani, bali tunaamini kuwa muswada huo utapelekwa bungeni katika Bunge la Novemba, mwaka huu,”amesema Balile.

Rais Samia alitoa maelekezo hayo Mei 2,mwaka huu,wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’,

Balile amesema kuwa lengo la mchakato huo ni kuwezesha marekebisho kadhaa ya vifungu vya sheria hiyo ili kuwezesha taaluma hiyo kutekeleza majukumu yake bila kukumbana na vikwazo.

“Tunaamini kuwa si wanahabari tu wanaofurahia uhuru wa kujieleza na kupokea habari, wenzetu Kenya kuna uhuru ni nchi jirani, unaona wameweza, sisi tuna kosa gani tusifikie huko, lakini haki inakuja na wajibu, inawezekana kukapata marekebisho au maboresho hayo.

“Kwa hatua hiyo itasaidia kuwatofautisha na wale wengine wanaoamka asubuhi na kuanzisha blogu au njia yoyote ya kutoa habari kwenye mtandao na kuanza kuiburuza nchi,wananchi pia bila kufuata maadili na misingi ya taaluma kwani kwa sasa baadhi ya watu wanashindwa kutofautisha wale wa mitandao na wanahabari,”amesema Balile.

Naye Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TEF akizungumza wakati wa mafunzo hayo amesema kuwa mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Habari si wa TEF pekee, bali ni muunganiko wa taasisi mbalimbali vikiwemo vyuo vya uandishi na idara za habari.

“Sula hili ni letu sote si la TEF pekee, na baada ya sheria hii kusainiwa na kuanza kutumika, wadau wa habari tulianza kuipinga ingawa awali hatukupata ushirikiano kama ilivyo sasa.’’ amesema Meena.

Amesema kuwa sheria ya habari ya mwaka 2016 inaweka adhabu isiyopungua miaka mitatu jela na kwamba, haimpi nafasi hakimu kutoa adhabu chini ya miaka hiyo hata kama kosa ni dogo.

Amesema yapo ambayo wameishakubaliana na mazungumzo bado yanaendelea. Sisi tunaamini kuwa, kuna athari chanya itatokea kwenye uandishi wa habari,”amesema Meena.