Akiahirisha Mkutano wa Saba wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julai 5, mwaka huu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pamoja na mambo mengine, alizungumzia sekta ya wanyamapori.
Kwa wahifadhi wengi, kauli ya Waziri Mkuu imewapa matumaini mapya yenye kuwawezesha kuona mwanga katika suala zima la uhifadhi nchini.
Kama alivyosema, asilimia 28 ya eneo la nchi yetu limetengwa kwa ajili ya kuhifadhi rasilimali za Taifa ikiwamo misitu, wanyamapori, na utunzaji mazingira kwa ajili ya matumizi ya binadamu na viumbehai wakiwamo wanyamapori ambao wanachangia kwa kiwango kikubwa katika shughuli za utalii.
Waziri Mkuu akakiri kuwa changamoto kubwa iliyopo sasa katika mapori yetu ya hifadhi ni uvamizi wa mifugo, na kwa bahati mbaya kwenye mikoa ya mipakani, mifugo mingi imekuwa inatoka nchi jirani.
Akalihakikishia Taifa kwa kusema: “Ili kuhakikisha kwamba Hifadhi za Taifa na mbuga zetu za wanyamapori zinalindwa kikamilifu, Novemba, 2016 niliagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka alama za mipaka (beacons) kuainisha maeneo yote ya hifadhi nchini kwa lengo la kuondoa migogoro iliyopo.
“Baada ya kuweka alama hizo, Serikali imeanza rasmi kuondoa mifugo yote ndani ya hifadhi. Aidha, nimeelekeza kwamba, uwekaji wa alama au nguzo hizo uhusishe Halmashauri za Wilaya na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Ramani zinazoonesha mapori zitumike. Aidha, mapori yote yaliyohifadhiwa kisheria yaheshimike.”
Akasema kutokana na kuwapo kwa migogoro baina ya wafugaji na wakulima na migogoro baina ya wafugaji na wahifadhi wa mapori, ameelekeza kwamba ifikapo mwisho wa Julai 2017, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wabainishe maeneo yote ya Ranchi za Taifa za Mifugo ambazo hazitumiki na kuzigawa katika vitalu kwa wafugaji ili mifugo mingi iondolewe vijijini na ipelekwe kwenye maeneo hayo ili Serikali iweze kutoa huduma za ugani za kisasa huko kwenye hivyo vitalu.
Akawaagiza wafugaji wote nchini: “Kufuata Sheria za Hifadhi za Taifa, Mbuga za Wanyamapori, maeneo tengefu pamoja na vyanzo vya maji. Mifugo yote itakayokutwa ndani ya hifadhi, hatua kali zitachukuliwa na kufikishwa mahakamani.
“Aidha, tukumbuke kuwa ardhi haiongezeki, lakini wafugaji na mifugo vinaongezeka, hivyo ni lazima tufuge kisasa na tufuge mifugo michache yenye tija ambayo tutaweza kuihudumia katika maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya ufugaji.”
Nachukua fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kulivalia njuga suala la uhifadhi nchini mwetu. Ni jambo linaloleta faraja kubwa kuona tunaweza kujadili masuala ya kimaendeleo badala ya kujikita kwenye siasa tu.
Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na maeneo mengine ya uhifadhi nchini ni chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni. Asilimia zaidi ya 20 ya fedha za kigeni zinapatikana katika eneo hili.
Pamoja na ukweli huu, sekta ya wanyamapori, kwa muda fulani imeonekana kama si lolote, wala chochote katika uchumi wa Taifa letu. Kuipa kisogo kumesababisha kuongezeka kwa kasi kwa mauaji ya wanyamapori pamoja na uharibifu wa misitu na mapori.
Tishio kuu la uhifadhi nchini ni wanasiasa. Kwa hali ilivyo sasa sioni kama ujangili ni ‘habari’. Tatizo kubwa ni wanasiasa na watu wenye ukwasi. Kumetokea kimbunga cha watu wenye ushawishi wa kifedha na kimamlaka kuingia kwenye ufugaji kwa kasi isiyolingana na mahitaji ya malisho.
Wapo wanasiasa wanaopata kura kwa sababu tu wanawaahidi wananchi kuwa endapo wakipewa madaraka, basi watamega baadhi ya maeneo na kuwapa wananchi kwa ajili ya malisho au kilimo.
Matokeo yake, mwanasiasa anapochaguliwa anafanya kila linalowezekana kutekeleza ahadi yake. Tumewashuhudia wabunge ambao licha ya kupitisha sheria za kulinda maeneo haya ya uhifadhi, wao ndiyo vinara wa kuhamasisha uvunjaji wa sheria.
Wao wenyewe wana makundi makubwa ya mifugo. Wachungaji wanaokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi, mifugo waliyonayo mingi si yao. Ni ya wanasiasa na watu wenye mamlaka katika jamii. Ndiyo maana pindi wafugaji wanapokamatwa kwa kuvunja sheria za uhifadhi, wanasiasa na hao wenye madaraka wamesimama imara kuwatetea na hata kulaani hatua za kisheria zinazochukuliwa na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii au wa Halmashauri.
Tumefanya utafiti na kubaini idadi kubwa ya Watanzania waliokubali kutumikishwa kwa kulisha mifugo ya raia wa nchi jirani. Katika maeneo kama ya Ngorongoro, Ngara, Karagwe, mkoani Kigoma, Katavi na Rukwa, ng’ombe wengi wanatoka nchi jirani. Tofauti na wao, sisi tuna ardhi ya umma, jambo linalorahisisha uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi.
Pengine nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nitashindwa kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu) Salim Kijuu, kwa uamuzi wake wa kishujaa wa kupambana na hatimaye kuondoa mifugo kutoka maeneo ya hifadhi mkoani kwake. Kwenye hili la mifugo katika maeneo ya hifadhi, Meja Jenerali Kijuu anastahili pongezi za dhati. Ni mfano wa kuigwa na wakuu wa mikoa wengine.
Haiwezekani Tanzania ikawa shamba la wageni la kunenepesha mifugo yao, kisha kwenda kuiuza makwao na wakati mwingine nje ya nchi zao. Wanafanya hivyo huku wakiiacha nchi yetu ikiwa imeumizwa mno kimazingira. Hatukatai wageni, lakini ni wajibu wetu kuhakikisha Tanzania inakuwa ya Watanzania kwanza.
Waziri Mkuu Majaliwa amegusia mpango wa kugawa maeneo ya ranchi kwa wafugaji. Huu ni mpango mzuri. Hatuna budi kuanza kufuga kisasa. Ng’ombe wa Tanzania kwa hali ilivyo sasa hawana thamani yoyote mbele ya ng’ombe wa mataifa mengine kama Botswana.
Ng’ombe mmoja wa Botswana thamani yake inaweza kuwa ng’ombe 50 wa Tanzania! Nyama ya ng’ombe wetu inauzika kwenye masoko ya makabwela wenzetu. Nyama ya ng’ombe aliyesafiri kutoka Ngara hadi Tunduma – nyama yake haiwezi kuuzwa, si Uingereza tu, bali hata kwenye migodi ya dhahabu hapa nchini. Ng’ombe waliokomaa kwa sababu ya kutembezwa safari ndefu hawana tija kwa mchungaji mwenyewe na kwa Taifa.
Ufugaji na ukulima wa kisasa ndiyo shughuli zenye tija. Migogoro mingi kati ya wakulima na wafugaji inasababishwa na shughuli za ufugaji na kilimo zinazoendeshwa kijima. Dunia ya leo inatutaka tuondoke huko. Ndiyo maana mpango huu wa Waziri Mkuu hauna budi kuungwa mkono na wananchi wote. Tuwe na mifugo michache yenye tija, na tutumie ardhi ndogo kwa ajili ya kuzalisha mazao mengi zaidi.
Lakini hilo nalo litawezekana endapo Serikali itahimiza ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao yatokanayo na mifugo. Ni jambo la kutia simanzi kuona wilaya kama za Ngorongoro, Tarime, Longido, Bariadi, Maswa, Babati na kadhalika, zikiwa na maelfu kwa maelfu ya mifugo, lakini hakuna hata kiwanda cha kusindika ngozi na mazao mengine ya mifugo. Hii ni simanzi.
Wakati huu ambao Serikali inajitahidi sana kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini, mpango huo mzuri hauna budi kwenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya mazao yatokanayo na mifugo.
Pamoja na mifugo, ni vizuri pia kukawapo viwanda vya kusindika minofu ya samaki katika ukanda wa pwani. Ni aibu kuona kuanzia Tanga hadi Mtwara (umbali wa kilometa zaidi ya 1,000) hatuna viwanda vya aina hiyo. Samaki wetu wanasafirishwa nje wakiwa ghafi. Hii si sahihi hata kidogo.
Basi, itoshe tu kusema tuna wajibu wa kuhakikisha tunalinda rasilimali ya wanyamapori na maliasili nyingine kwa ajili ya faida za sasa na kwa kizazi kijacho.
Na matumaini ya wengi ni kuona kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa aliyoitoa bungeni kuhusu wanyamapori inatekelezwa.