Oktoba 14, mwaka huu, mwasisi na Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ametimiza miaka 13 tangu afariki dunia. Siku ya kuadhimisha kifo chake, tumeusikia ujumbe mzito kutoka serikalini, taasisi mbalimbali na watu binafsi, wote wakiahidi kumuenzi kwa mema yote aliyoyatenda.
Sisi tunasema ni jambo jema kutoa ahadi kama hizi. Hata hivyo, nchi yetu kwa sasa ina tatizo kubwa. Wakati nchi jirani ya Kenya inasumbuliwa na ukabila, Uganda inasumbuliwa na wapiganaji wa msituni akina Joseph Konny, Rwanda na Burundi zinasumbuliwa na ukabila uliosababisha mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, hapa Tanzania tunamezwa na udini.
Udini ni tatizo lililoanza kidogo kidogo, lakini sasa umelifikisha taifa letu pabaya. Tanzania imeruhusu madhehebu mbalimbali kuchipuka kama uyoga, ambayo kwa bahati mbaya hayaratibiwi kufahamu yanafanya nini. Tatizo linaloonekana wazi na kujadiliwa kwa kina ni la Waislamu na Wakristo, lakini sisi tunasema tatizo ni zaidi ya hilo.
Hapa nchini yameibuka makanisa yanayojinadi kuwa ni ya Kilokole, ambayo yanatundika vipaza sauti vikubwa kwenye makanisa yao na kusali usiku kucha, huku wakibeza wafuasi wa dini au madhehebu mengine wasio Walokole kwa kiwango cha kutisha. Walokole wanatamka kauli za kuudhi ikwamo kuhukumu watu wakiwa hapa duniani kuwa ni wa shetani na wakifa hawatakwenda mbinguni.
Ukiacha Walokole wanaokera, wameibuka Waislamu wanaoishi kwa mihadhara na wakati mwigine kupotosha maneno ya Mtume Mohammad (S.A.W). Wakati Mtume Mohammad akihubiri upendo, baadhi ya Waislamu wanahubiri Sharia. Wanakejeli Wakristo kwenye mihadhara kwa kumfanya Yesu aonekane kama kikaragosi kwenye maigizo ya mihadhara. Tukio la Mbagala wiki iliyopita ni mwendelezo na halikubaliki. Makanisa matatu yameharibiwa kwa kisa cha watoto.
Huu unekuwa mwendelezo wa kauli ya kijana mmoja huko Morogoro, aliyefika kwenye mkutano wa Wakristo na kusema Yesu si Mungu. Kwa waliokuwa wakubwa wanakumbuka kilichotokea katika taifa hili. Udini ni hatari. Imani zetu hazituongezei shibe wala pato la taifa, isipokuwa tu kutuandalia makazi ya ahela baada ya kifo chetu.
Mwalimu Nyerere mara kwa mara alikuwa akisisitiza maneno haya; NCHI YETU HAINA DINI. Msisitizo huu umepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni. Kwa sasa hakuna kiongozi wa kitaifa anayesimama na kukemea udini mara kwa mara kama wanavyofanya katika kuihamasisha jamii kuhusu ukimwi.
Sisi tunasema tulipofikia panatosha. Yeyote atakayefanya uhalifu kwa mgongo wa dini ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria kama mhalifu. Tusiogope dhana kwamba wafuasi wenzake wataandamana. Wakiandamana bado tunayo sheria ya kuchapa viboko watu watukutu ya Mwaka 1989. Mahakama iwahukumu wahusika kwa kutumia sheria hii na adhabu hii itolewe.
Tulipofika tunasema udini unatupeleka kuzimu. Viongozi wa kitaifa waanze sasa kukemea udini sawa na wafanyavyo kwa ukimwi. Kwa njia hii tutakuwa tunamuenzi Nyerere kwa vitendo. Tunaitaka Serikali ipambane na udini unaohatarisha umoja wetu bila kusita.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu tuepushe na udini Tanzania.