Wakati taifa likiwa katika wiki ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua kampeni ya maendeleo na mampambano dhidi ya UVIKO-19.
Ni kampeni ya aina yake itakayodumu kwa miezi tisa tu, ikichagizwa na mkopo nafuu kutoka kwa wahisani wa zaidi ya Sh trilioni 1, ambao utaelekezwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo na huduma za jamii.
Rais Samia ameweka wazi, tena hadharani, namna fedha hizo zitakavyotumika na kugusa kila eneo la Tanzania; Bara na Zanzibar, akitaka uwazi katika matumizi yake na kutoa onyo kwa matumizi mabaya au wizi wa fedha hizo.
Kwa namna yoyote ile, matumizi ya fedha hizo yataibadili sura ya Tanzania na uwazi uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita utabaki kuwa alama ya namna sahihi ya matumizi ya mali ya umma, ikiwa ni pamoja na kuondoa minong’ono na manung’uniko ya mara kwa mara ya matumizi mabaya ya fedha za mkopo.
Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, yeye binafsi alikemea kwa sauti kubwa na kwa vitendo matumizi mabaya ya mali ya umma, kiasi cha kuanzisha kampeni kwa njia ya redio, kueleza ubaya wa wizi wa mali ya umma.
Moja ya kampeni hizo ilimtaja mwizi wa mali ya umma kwa kumfananisha na punguani; yaani mtu asiye na akili timamu; mtu anayetumia kitu chenye ncha kali kujikatakata na kunyonya damu yake mwenyewe huku akitabasamu.
Kwa miaka mingi sasa, wizi na ubadhirifu wa fedha na mali ya umma umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya Tanzania, ukidumaza maendeleo ya taifa kwa kuua miradi, mashirika, viwanda huku miundombinu mbalimbali ikijengwa chini ya kiwango.
Sasa Mama Samia anaonyesha njia kwa kukemea namna yoyote ya ubadhirifu wa fedha hizo anazoziingiza kwenye miradi ya kijamii na maendeleo. Jukumu letu kama wananchi wa Tanzania ni kumuunga mkono.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunamuenzi kwa vitendo muasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere, hasa katika wiki hii ya kumbukizi ya miaka 22 ya kifo chake. Mwalimu alikuwa akitamani kuiona Tanzania ikistawi huku wananchi, hasa wanyonge, wakipata huduma zote za msingi.
Tunaamini kwamba ifikapo Julai mwakani, miezi tisa baada ya uzinduzi wa kampeni hii, Mama Samia atarejea tena Ukumbi wa Jakaya Kikwete na kuwashukuru Watanzania kwa kumuunga mkono na kuwaenzi waasisi wa taifa kwa kutekeleza kwa uaminifu mpango huu wa maendeleo.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.