Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kusema kuwa urais ni kazi ngumu, akaifananisha na mzigo mzito. Nayaamini maneno hayo ya mzee wa Kizanaki.
Nimejitoa wazi kutaka kumsaidia rais wetu kupambana na ugumu huu ninaouona. Kwa sababu rais anaongoza taifa ambalo ndani yake kuna majambazi, wachawi, wezi, waporaji, wanafiki, wazabizabina, wachafu na watu wa kila aina. Ni jukumu lake kuhakikisha anawalinda wote hao ili waweze kukaa salama na taifa kusonga mbele likiwa salama.
Ni vigumu sana kwake binafsi kuwatambua watu wote hawa na kuwafahamu mara moja yupi ni mwenye asili gani au yupi anakusudia kufanya nini. Lakini anayaweza haya kwa sababu ana wasaidizi ambao kimsingi wanafanya kazi kwa niaba yake.
Hawa wanamwonyesha na kumweleza kuhusu mambo mengi na akionyeshwa au kuambiwa ni nani amefanya nini, anaweza kujua achukue hatua gani. Hilo la kumwonyesha na kumwambia rais ni tendo la kiuzalendo.
Yupo mtu aliyejitokeza kuandika kitabu kuhusu mtu ambaye kwa sasa analeta mizengwe kwa rais aliye madarakani, yaani Rais Dk. John Magufuli, kwa vile naye alitamani kukalia kiti ambacho anakikalia rais hivi sasa. Na yeye aliutaka urais.
Tunafahamu kuwa visa vya mtu huyo havikuanza pale rais wa sasa alipoingia madarakani. Visa hivyo vilianza tangu wakati rais wa sasa akiwa waziri, hata kabla hajawa na ndoto ya kuwania urais.
Uzuri ni kuwa, kwa kuwa wasaidizi wake wanamfikishia taarifa, haya yote rais anayafahamu. Lakini kwa wakati huu mtu huyo amegeuka na sasa anajifanya ni kipenzi kwa Rais Magufuli. Anajiweka msitari wa mbele kiasi cha kufikiria kwamba rais anaweza kumteua kuwa mkuu wa wilaya.
Hapa ndipo ninaposema kwamba tunatakiwa kumsaidia rais wetu aepukane na kufanya makosa, makosa ya kumuingiza mbaya wake katika safu ya wasaidizi wake.
Mtu ambaye ninamjua kwa karibu kuwa aliwahi kutamka waziwazi kuwa JPM hafai kuwa kiongozi mkuu wa nchi, leo hii anatamani kuwa msaidizi wake katika kazi ambayo awali alisema JPM haiwezi, ni kitu cha ajabu. Ni lazima tumsaidie rais wetu kuwatambua wazabizabina wa aina hiyo ili aepukane nao.
Mtu huyo alikuwa kiongozi kwenye taasisi nyeti ya kidini, akiheshimika kabisa, lakini baadaye akaanza kufanya mambo yaliyo tofauti na aliyoapa mbele ya Mungu kuyatekeleza. Baadaye uongozi wa madhehebu hayo ukaamua kumtenga baada ya kumuona hafai, ukamtimua.
Kwa sababu mtu anayekwenda kinyume cha alichoapa kukifanya, anajionyesha wazi kuwa hafai kwa chochote, nadhani hata akionyeshwa njia ya kuingia mbinguni atagoma kuingia, utamwamini kwa lipi?
Mtu wa aina hiyo aliyekula kiapo kwa Mwenyezi Mungu kuwa atafanya hili na lile kisha akagoma kufanya kama alivyoapa na badala yake kuamua kufanya kinyume kabisa akiwa kiumbe tofauti leo hii anajifanya kuwa karibu na rais wa nchi.
Nani asiyeona kuwa rais ana kazi kubwa? Inabidi tumsaidie rais walau kumuondolea viumbe kama hawa wa ajabu na kuwasogeza mbali naye. Mtu ambaye hakumuogopa Mwenyezi Mungu atamuogopa rais?
Mtu aliyekuwa akimpinga rais kuwa hafai kukalia kiti hicho kiasi cha kuandika kitabu kwa ajili ya mtu mwingine, leo hii bila aibu wala haya, anajifanya kuwa karibu na rais.
Kweli wananchi wanaomtakia mema rais wao watakubali jambo hili liendelee kuwapo? Mtu huyo mbali na hilo la kumpiga vita tangu mwanzo rais wetu, pia anayo mengi machafu ambayo sidhani kama rais anakubaliana nayo.
Lakini ninamuamini Rais Magufuli kwamba si mtu wa kuhadaika na mambo madogo kiasi hicho, hata kama mtu anamjua au kuwa rafiki yake, akigundua ana kasoro hakawii kumuwajibisha.
Tumeona alivyofanya kwa waliokuwa wakijifanya kuwa karibu naye na baadaye kufanya mambo yasiyofaa. Je, itakuwa kwa mtu aliyekuwa akimpinga tangu mwanzo?
Kwa maana hiyo, hata huyu ambaye anatuonyesha unafiki wake, hata akifika katika hiyo nafasi anayoitamani, ninaamini Rais Magufuli hatamwacha salama pale atakapoharibu.
0654 031 701