Hakuna mtu anayeweza kuandika yote ya Dk. Reginald Mengi. Hata watu alioshinda nao na kukaa nao kwa miaka mingi, hawawezi kuyaeleza yote. Huyu alikuwa mtu wa kitaifa na kimataifa. Alikuwa mtu wa watu wote, wadogo, wakubwa, maskini, walemavu, matajiri, wanasiasa hata na watu wa vijiweni. Alizalisha ajira kwa Watanzania na watu wengine kutoka nje ya nchi. Alikuwa mcha Mungu, mshauri wa familia na jamii nzima, alikuwa kipimo cha utu mwema katika jamii yetu ya Tanzania.
Mapokezi ya mwili wake Dar es Salaam na Kilimanjaro, kuuaga mwili wake Dar es Salaam na Kilimanjaro ni ishara inayojitosheleza kwamba huyu hakuwa mtu wa kawaida. Bila kuwa mwanasiasa, kiongozi wa serikali, kiongozi wa dini au kiongozi wa jadi, lakini akapata heshima yote hiyo, si jambo la kawaida. Ni Mtanzania aliyetukuka. Kwa kifupi, tunabaki kusema kwamba Bwana alitoa, Bwana ametwaa, jina lake libarikiwe.
Kwa bahati tuna kitabu alichokiandika Dk. Mengi, tunaweza kukisoma na kujifunza mengi. Hata hivyo tuliishi naye, tulimsikia na tuliona matendo yake makuu. Katika makala hii ya kuziimba sifa zake na kuandika tanzia yenye kutukuka, ningependa kujadili na kutafakari maneno ya mzee Mengi. Alisema mengi, lakini hili la ulemavu wa fikra linahitaji tafakuri ya kina. Taifa letu la Tanzania linaweza kusimama na kustawi likitafakari juu ya ulemavu wa fikra na kuupiga vita.
Nilimsikia mzee Mengi akiongelea ulemavu wa fikra kwenye matukio mawili tofauti. Kama si taifa letu kushambuliwa na ulemavu wa fikra, maoni ya mzee Mengi yangezua mjadala mkali. Watu wangejiuliza, ana maana gani anaposema ulemavu wa fikra? Mara ya kwanza nilimsikia mzee Mengi akiongelea ulemavu wa fikra wakati akiongea na walemavu. Aliwaambia wasifikirie kwamba kwa vile wana ulemavu wa viungo vya mwili, basi wao ndio walemavu au kufikiri kwamba wao si watu muhimu katika taifa au kujisikia unyonge na kukata tamaa, hata watu wenye viungo kamili vya mwili wanaweza kuwa walemavu, hasa ulemavu wa fikra! Kwa maoni ya mzee Mengi, mtu mwenye viungo kamili vya mwili lakini ana ulemavu wa fikra anaweza kuwa mnyonge na mtu asiyefaa katika jamii kuliko mtu mwenye ulemavu wa viungo.
Mara ya pili, nilimsikia mzee Mengi akiongelea ulemavu wa fikra wakati akizungumza na vijana waliokuwa wakishindania zawadi za twiter nzuri juu ya uanzishwaji wa biashara. Alirudia kusema kwamba tatizo kubwa linaloturudisha nyuma kama taifa ni ulemavu wa fikra.
Maoni ya mzee Mengi yalinifanya nitafakari mambo mawili, kwanza nilitafakari juu ya kitabu “Why God Won’t Go Away”. Kitabu hiki ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Andrew Newberg, Eugene D’aquili na Vince Rause, juu ya sayansi ya ubongo na baiolojia ya kuamini. Wazo kuu katika utafiti wao ni je, Mungu anautengeneza ubongo au ubongo unamtengeneza Mungu? Kitu wanachokigundua ni kwamba ubongo ndicho chombo cha pekee katika mwili wa mwanadamu kinachotengeneza kumbukumbu na kuzitunza.
Ubongo unamsukuma mwanadamu kuwa na woga na kujiuliza maswali mengi ambayo majibu yake yanamfanya mwanadamu kuishi tofauti na wanyama wengine. Mwanadamu hujiuliza, kwa nini tulizaliwa kama mwisho wetu ni kufa? Kunatokea nini tukifa? Nafasi yetu ni ipi katika ulimwengu mzima? Kwa nini kuna mateso? Ni nani anayatuma mateso? Ni nani anautunza na kuulinda ulimwengu? Ulimwengu utaendelea kuwepo hadi lini? Tunawezaje kuendelea kuishi kwenye ulimwengu usioaminika bila kuwa na woga?
Majibu ya maswali haya ni lazima yamwelekeze mwanadamu kwa Mungu. Majibu ya maswali haya ndilo chimbuko la dini zote za dunia hii. Mtu asiyejiuliza maswali kama haya, hapana shaka ataishi kama mnyama mwingine wa porini! Huu ni mjadala mrefu na ni utafiti wa kisayansi, ni vigumu kuujadili kwenye makala hii.
Unahitaji makala inayojitegemea, Mungu akiniwezesha nitauendeleza siku za usoni! La msingi katika mfano huu ni kutaka kuonyesha jinsi maneno ya mzee Mengi yalivyonifanya kutafakari mambo mazito.
Baada ya kutafakari kitabu cha “Why God Won’t Go Away”, nilitafakari maneno ya Bwana Yesu: “Ndiyo maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.” (Matayo13:13).
Ulemavu wa fikra unaweza kusababishwa na mambo mengi. Mtu anaweza kuzaliwa akiwa na ulemavu wa fikra. Inawezekana ubongo ukawa na kilema cha kutoweza kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza vizuri. Wapo watu wanazaliwa wakiwa punguani, vichaa na wendawazimu lakini pia kuna ulemavu wa fikra wa kujitakia au kulazimishwa.
Wale wanaotumia dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, wanaulazimisha ubongo kushindwa kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza. Lakini pia kumtawala mtu kimawazo kunaweza kusababisha ulemavu wa fikra. Utumwa na ukoloni ni kati ya vitu vilivyosababisha ulemavu wa fikra. Athari hii inajitokeza katika nchi karibu zote zilizotawaliwa na kuonja adha ya utumwa. Mfano utumwa na ukoloni, ulisababisha baadhi ya watu kukataa mila zao, rangi ya ngozi zao au lugha zao.
Tuchukulie mfano wa jamii za kwanza kuishi hapa Tanzania. Jamii zilizoanza kushuhudia kifo. Mwanaukoo anakufa. Mwili wake unawekwa mbele ya ukoo mzima, na kila mtu anashangaa ni kitu gani kimetokea. Kila mtu anajitahidi kuugusa mwili wa marehemu na kuhisi hauna uhai tena. Mtu aliyekuwa akitembea, akicheka na kufanya kazi, sasa amelala mbele yao bila kujitingisha, mwili wake hauna joto tena, hawezi kuzungumza wala kucheka.
Kiongozi wa ukoo anaagiza ukokwe moto mkubwa, wanaukoo wanauzunguka moto huo wakiwa na mwili wa mwanaukoo mwenzao asiyeweza kusimama. Kila mtu anatafakari juu ya tukio hilo. Ni kitu gani kimetoweka kwenye mwili wa ndugu yao, je, kitu hicho kitakuwa kimekwenda wapi?
Jinsi muda unavyopita kasi ya moto mkubwa inaanza kupungua. Kuni zilizokuwa rundo zinaanza kuungua na kuwa majivu. Kadiri moto unavyopungua ndivyo moshi unavyokazana kupaa juu mawinguni. Moto unatoweka na moshi unaishia mawinguni. Kiongozi wa ukoo anaanza kutafakari juu ya kuni, moto, moshi na majivu.
Ubongo wake unaanza kutengeneza kumbukumbu na kuleta fikra pevu, jinsi kuni, moto na moshi vinavyopotea na kubakiza majivu, ndivyo mwili wa rafiki na mwanaukoo aliye lala mbele yao ulivyopoteza kicheko, sauti, kusimama na kubaki mwili usiokuwa na uhai. Jinsi moshi unavyoishia mawinguni, ndivyo uhai wa rafiki yao unavyoishia mawinguni pia! Fikra hii ya kiongozi inasambazwa kwa wanaukoo wote. Kwa njia hii ukoo wote unamgeukia Mungu.
Mtu ambaye ana ulemavu wa fikra hawezi kutafakari. Atakazana kulimbikiza pesa ambazo hazitamnufaisha yeye wala familia yake. Ni nani ananufaika na pesa za Mobutu au Sani Abacha? Pamoja na mifano hii ya wazi, bado kuna watu hapa Tanzania, wanaendelea kulimbikiza pesa. Watu wanakufa kwa njaa, watoto hawawezi kwenda shule, watu wanakufa kwa magonjwa yanayotibika, wakati kuna watu wachache wamelimbikiza pesa ambayo ingeweza kumaliza matatizo yote hayo!
Hivyo tunapowachagua viongozi wetu, tusiwapime kwa ubora wa viungo vyao, ubora wa pua, miguu, urefu, ufupi, uzuri wa sura, ubora wa kuongea lugha za kigeni, ubora wa kuvaa suti za kigeni! Tuwapime kwa ubora wa fikra zao. Kiongozi ambaye ubongo wake hauwezi kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza, kiongozi ambaye anaitizama maiti bila kutafakari, kiongozi anayeziangalia kuni zikiteketea na moshi ukiishia mawinguni bila kutafakari, kiongozi anayeona yanayotokea kwa majira zetu akaendelea kuishi bila kutafakari, kiongozi anayeishi kwa kunywa, kula na kulala hawezi kuitawala Bongoland! Mlemavu wa viungo vya mwili anaweza kuwa kiongozi mzuri, lakini mlemavu wa fikra ni moto wa kuotea mbali!
Hivyo tunapomlilia mzee wetu Mengi na kuonyesha mapenzi makubwa juu yake na kujifariji kwamba tunasherehekea maisha yake ya hapa duniani, ni bora pia tukatafakari juu ya maneno yake mazito, hasa hili la ulemavu wa fikra. Tunalilia maendeleo, tunalilia mabadiliko kwenye jamii yetu ya Tanzania, tunalilia uongozi bora na siasa safi, tunalilia demokrasia katika taifa, tunalilia amani na utulivu, yote haya yanawezekana kama tukikubali kupambana kwa nguvu zetu zote na ugonjwa huu wa ulemavu wa fikra.