Jamii imeshauriwa kujenga mazoea ya kutumia vyakula asilia, vikiwamo mbogamboga na matunda kupunguza kemikali, kutibu magonjwa na kusafisha damu mwilini.
Changamoto hiyo imetolewa na Dk. Norbert Mchomvu katika mafunzo ya matumizi ya kirutubisho cha ‘Omega Herbal 48’ kitokanacho na mchanganyiko wa ‘Wamime 16’, yaliyofanyika Golden Rose jijini Arusha, hivi karibuni.
Amesema kirutubisho hicho kipo katika hali ya kimiminika kinachosaidia kupunguza kasi ya kemikali katika mwili wa binadamu. Hufanya kazi ndani ya saa 48.
Kutokana na baadhi ya watu kusumbuliwa na magonjwa mbalimbali na mengine kushindikana kupatiwa tiba, Dk. Mchomvu amewashauri watu kutumia mimea asilia kwa ajili ya matibabu. Ametaja aina ya mimea hiyo kuwa ni pamoja na mdalasini, mwarobaini, mafuta ya nazi na vitunguu saumu.
Ameongeza kuwa kirutubisho cha ‘Omega Herbal 48’ chenye ujazo wa mililita 250, kina uwezo wa kutibu magonjwa sugu yakiwamo ya shinikizo la damu, vidonda vya tumbo, maumivu ya mifupa na kukaza viungo vilivyolegea. Amesisitiza kuwa magonjwa mengi hutokana na matumizi mabaya ya vyakula.
Janeth Shaidi ni Mratibu kutoka huduma ya Jehova Rapha, yeye amesema kirutubisho hicho kinatokana na mimea asilia 16. Nao mashuhuda waliopata kutumia kirutubisho hicho wamesema dawa hiyo imewasaidia kupona magonjwa mbalimbali yaliyowasumbua kwa muda mrefu, na kuweza kurejea katika hali yao ya kawaida.