Hotuba ya Mwalimu Julius K. Nyerere Aliyoitoa Wakati wa Kilele cha
Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani, Mbeya, Mei Mosi, 1995.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mei Mosi, 1995. Katika hotuba yake, Mwalimu alielezea historia ya vyama vya wafanyakazi duniani. Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa maoni yake kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini pamoja na ushauri kuhusu mambo wananchi wanayopaswa kuzingatia wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huo, hasa sifa za wagombea nafasi za uongozi kuwa ni pamoja na kila mmoja kujiuliza ataifanyia nini nchi yake baada ya kuchaguliwa, na anakwenda kufanya nini Ikulu. Ifuatayo ni hotuba ya Mwalimu…
Ni muhimu kukumbuka kuwa hotuba hii imefuata mlolongo wa mazungumzo Baba wa Taifa aliyokuwa nayo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali, ambako alikuwa anajaribu kuamsha dhamira ya viongozi wetu wa wakati ule. Hotuba hii ni miongoni mwa hotuba ambazo ukweli wa hoja zake ni hazina kubwa kwa vizazi vijavyo vya Watanzania.
Mwenyekiti wa OTTU,
Viongozi wa OTTU,
Viongozi wa Serikali,
Viongozi wa Madhehebu ya Dini Mkoani na
Wananchi wote wa Mkoa na Mji wa Mbeya.
UTANGULIZI
Sababu za kukataa mwaliko wa mwaka uliopita na kuukubali mwaliko wa mwaka huu:
Kwanza kabisa, napenda kuwashukuru viongozi wa OTTU
ambao walinijia na kuniomba nishiriki katika shughuli hii ya leo. Shukurani ya pili nataka kutoa kwa wananchi wa mjini Mbeya na mkoani Mbeya jinsi mlivyonipokea tangu jana mpaka leo. Ahsanteni sana.
Ninyi siku zote, pamoja na mimi, tulikuwa tunazo tabia zetu za maadili ya kumwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ndiye awe Mgeni Rasmi katika shughuli hii. Kweli najua sasa taratibu zimebadilika, vyama vingi vya siasa, na kadhalika, lakini, hata hivyo, bado mnaweza kumwalika Mgeni wenu Rasmi kuwa Rais.
Mwaka huu hamkusudii mnakuja kunialika mimi? Sababu ya pili ya kukataa (mwaka jana) ni ile niliyowaambia. Mwaka huu mmegomeana na Serikali. Sasa mwaka ambao mmefanya mgomo na Serikali kuja kuniomba niwe Mgeni Rasmi katika shughuli kama hiyo ndiyo tunatoa ujumbe gani? Ujumbe wa namna yoyote ile mimi siwezi kuutoa. Nilikataa.
Nasema hizo ndizo sababu zangu za msingi za kuwakatalia mwaka jana na kuwakubalia mwaka huu. Vijana niliowakatalia ndiyo hawa. Sasa mwaka huu niwakatalie tena? Angalao hiyo ni sababu moja ya kuwakubalia mwaka huu. Huwezi kuwakatalia mwaka hata mwaka!
Sababu yangu ya pili iliyonifanya nikakubali ni kwamba huu ni mwaka wa uchaguzi. Sasa, mwaka wa uchaguzi lazima wote tushirikiane kusema tunakwenda wapi? Nafasi kama hii ni nzuri kwa mtu yeyote mwenye mawazo kusema “jamani huu ni wakati wa uchaguzi tunakwenda wapi?”
Nikadhani ni nafasi nzuri mkinipa niitumie kutoa maoni yangu. Si yote. Ni baadhi, lakini ni sehemu ya maoni yangu katika jitihada za kusaidiana kuelewa tunatoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi. Na kama tunataka kwenda huko, tufanyeje ili tufike huko. Tusije tukashtukia tunapelekwa mahala ambako siko tulikokuwa tunakusudia kwenda.
Hizo ndizo sababu zangu kubwa za kuwa hapa. Hasa ya pili ndiyo iliyonifanya nikakubali kuja hapa. Kwa hiyo, kwanza ninawapongezeni ndugu wafanyakazi kwa siku ya leo, Siku ya Wafanyakazi Duniani. Tunaiadhimisha dunia nzima.
CHIMBUKO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI DUNIANI NA HAJA YA MSHIKAMANO
Wazo la kuwa na vyama vya wafanyakazi duniani, kwamba wawe na mshikamano na umoja wa kutetea maslahi yao si wazo la Tanzania wala la nchi zilizoendelea. Kusema kweli, kwa historia, lilianza huko Marekani na lilikubalika.
Wafanyakazi wa wakati huo, katika nchi ambazo maendeleo yake yalikuwa mazuri, waliamua wafanye mshikamano wa kuleta maendeleo yao na hasa ya kupambana na waajiri wao.
Mwajiri anaanzisha shughuli yake na anafanya kwa nguvu zake mwenyewe. Anataka kulima na analima kwa nguvu zake mwenyewe. Kama anataka kufungua kiwanda chake cha mbao, maana ninyi ni wafanyakazi inapasa nizungumzie habari ya viwanda badala ya kilimo, anafungua kiwanda chake cha kutengeneza samani. Anaweza kutumia vitu vyake mwenyewe na akawa anafanya kazi na seremala mmoja. Atakuwa amepata randa, meza, patasi na kila kitu chake.
Anafanya kazi yake mwenyewe, anatengeneza vitu vyake, anauza na anapata hicho anachokipata. Hicho anachokipata kinatokana na nguvu yake mwenyewe. Anakata mbao na anatengeneza. Mtu anamwendea na kumwambia, “mimi nataka meza bwana”, anamtengenezea.
Inabidi mwenyewe ashughulike na meza hii mpaka inakuwa nzuri. Anapata kile anachopata. Nyingine anafidia zile gharama zake za meza, randa na za vyombo vingine vyote hivyo. Halafu, kinachobaki chochote, ndiyo maslahi yake. Lakini, kile anachopata kinatokana na jasho lake mwenyewe.
Akitoka hapo, anaweza kuwa mshiriki na mwenzake, washirikiane wote wawili na si kwamba mmoja atamwajiri mwingine. Hapana! Wote wawili watafanya kazi kwa pamoja. Watasaidiana vizuri zaidi wakifanya pamoja. Wao, vile vile, wanaweza wakapata maslahi kutokana na nguvu zao wenyewe.
Mwanzo wa dhuluma ya unyonyaji
Wakitoka hapo nao wakajifanya ni waajiri wanaotaka kuwaajiri wengine, shughuli ile si ya hawa walioajiriwa tena. Ni ya hawa wawili tu. Wakisha kuwaingiza wengine, hao si yao. Wanasema. Sasa njoo hapa tusaidie kutengeneza meza, vitanda, madirisha na milango. Lakini, meza inapokuwa imekwisha, tunaiuza. Si mali yenu ninyi wafanyakazi. Ni mali yetu. Ninyi chenu humu ni ule mshahara na wala si faida itakayopatikana humu.
Faida, [baada ya kutoa gharama zote za ununuzi wa mbao, usafirishaji wa mbao zote zile pamoja na gharama za kuwaajiri ninyi muitoe meza hii – kwa kuwa mishahara yenu ni sehemu ya gharama] nikitoa gharama zote hizi, kinachobakia ni changu.
Sasa ile inayobaki, baada ya kutoa gharama hizo, inaweza kuwa kubwa na inaweza kuwa ndogo. Inategemea sana gharama zilikuwaje. Kama gharama za kununulia mbao zilikuwa kubwa, zinanipunguzia faida yangu. Kama gharama za wafanyakazi ni kubwa mishahara ya wafanyakazi kama ilikuwa mikubwa, inanipunguzia faida yangu. Kwa hiyo, sipendi vyote viwili. Sipendi muuza mbao aniuzie ghali na sipendi mfanyakazi adai mshahara mkubwa. Napenda wote waniuzie rahisi. Nataka mbao kiurahisi, nataka mishahara iwe chini. Hapo ndipo ninapopata faida kiuchumi.
Hili sijambo la ajabu la Wazungu wenzetu wanaojua bali ni la kila mtu mwenye akili kama zenu kutokana na mtiririko wa mantiki wa hoja yenyewe. Kwamba, mimi nataka mshahara wenu uwe mdogo kwa kuwa faida yangu inatokana na mshahara wenu kuwa mdogo. Sasa ninyi mtasema: ALAA Bwana Mkubwa, kazi tufanye sisi halafu wewe utupe mshahara mdogo. Tukufanyie kazi wewe? Basi uone iwapo tutakufanyia.
Umoja na mshikamano ndiyo silaha ya kupambana na dhuluma ya unyonyaji. Kama watakuwa wananiambia mmoja mmoja, nitawafukuza. Unakuja peke yako na unaniambia ‘Lakini Mzee sasa mimi nataka uniongeze mshahara’. Nitakuambia, unaniambia nini wewe? Unasema nikupe mshahara wa shilingi ngapi? Utajibu. ‘Ah, kama utakavyoona, lakini uniongeze. Mungu anaona na Mtume’. Nikaona kidomodomo chake huyu nikamwambia: Unataka mshahara huo ninaokupa sasa hivi? Nyamaza na nenda kafanye kazi huku utachagua. Kama hutaki, toka. Kazi sikukuomba. Ulikuja mwenyewe.
Nitakutisha hivyo. Ukifikiri mchezo, nitakufukuza. Na wenzako watajua kafukuzwa kwa nini yule. Amedai mshahara mwingi. Mimi kimya! Wengine hawatathubutu tena maana watafikiri. Nikisemasema hapa na mimi nitatimuliwa na watoto wana njaa. Nikitimuliwa nitapata taabu. Wewe unaonaje? Anaendelea huyu kukunyanyasa. Kama anaweza kuwanyonya wauza mbao na kukunyonya wewe mfanyakazi, atawanyonyeni wote mpaka wauza mbao washirikiane kwa pamoja wapate bei nzuri. Mpaka wafanyakazi washirikiane kwa pamoja wapate mishahara mizuri. Bila kushirikiana, hawapati mishahara mizuri.
Hii ndiyo asili ya kuanzisha vyama vya wafanyakazi. Nasema hamkuvianzisha ninyi vilianzishwa zamani, tena Marekani. Lakini, Marekani havikuwa na nguvu sana. Vilikuwa na nguvu zaidi Ulaya. Hata hivyo, havina nguvu sana tena Ulaya. Sitaki kuingilia na kuliendeleza hili kwa kuwa viongozi wenu kama wanaelewa, watawaelezeni.
Zamani, vyama vya wafanyakazi vilianzisha mshikamano wa wafanyakazi duniani. Kaulimbiu yake ilikuwa Wafanyakazi Duniani Unganeni. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo yenu. Mantiki ya kaulimbiu hiyo i1ikuwa kwamba, kwa kuwa mmefungwa minyororo na mmenyonywa unganeni. Huo ulikuwa ndiyo ujumbe wa kaulimbiu hiyo kwa wafanyakazi dunia nzima. Hata hivyo, sisi hatukuwapo.
TUMETOKA WAPI?
Hatukuwa wamoja
Hii ni nchi mpya na ndiyo ambayo tumekuwa tunajaribu kuijenga. Kwanza Tanganyika, kwa muda mfupi na, halafu, Tanzania. Kusema kweli, sisi wengine maisha yetu ya urais wetu ni wa nchi inayoitwa Tanzania.
Nilipokuwa rais wenu, ni1ifanya juhudi za kukomboa eneo hili linaloitwa Tanganyika. Lakini, uongozi wangu niliowaongoza ninyi katika nchi huru inayojitawala na raia duniani wa nchi huru inayojitawala. Niliwaongozeni katika nchi inayoitwa Tanzania. Tanganyika niliwaongozeni kwa muda mfupi tu; tangu Desemba 1962 mpaka Aprili 1964 basi. Kipindi changu kingine chote, niliongoza nchi inayoitwa Tanzania siyo Tanganyika. Kwa kweli, siijui Tanganyika ya watu huru. Ni muda mfupi mno.
Nchi hii Tanganyika, ni nchi changa. Watu wake waliwekwa katika sehemu inayoitwa moja na Wajerumani. Wamakonde na Wazanaki hawakuwa wamoja. Waliwekwa pamoja na Wajerumani ili watawaliwe. Jitihada ya kuwafanya wawe pamoja na kuanza kusema “Ninyi ni wamoja” haikufanywa na Wajerumani.
Hakuna Wajerumani ambao wangeweza kusema “Ninyi ni wamoja” kwa kuwa lengo lao halikuwa kujenga umoja. Wajerumani walichoweza kusema ni kwamba “Ninyi ni tofauti, ninyi ni tofauti!” ili waendelee kututawala.
Jitihada ya kwanza ya dhati ya kusema “Ninyi ni wamoja” ilikuwa ni yetu sisi tulipoanzisha chama cha TANU. Shabaha yake kubwa ilikuwa ni kujaribu kujenga umoja ili tuwatimue Waingereza. Lakini mbinu yake ya kwanza kabisa iliyotajwa ilikuwa ni kufuta ukabila. “Sahau ukabila!” tulitamka kwa ukali.
Wale ambao, labda mpaka leo, wanako kakitabu ka milango ya historia ka Katiba ya TANU wataona tumeshambulia kitu ukabila. Tukaanza hatua ya kwanza kabisa, kusema “Sisi ni Taifa”. Lakini halikuwa likiitwa taifa la Tanganyika.
Itaendelea