Leo ni siku yenye umuhimu wa pekee kwa Kampuni ya Jamhuri Media Limited, wazalishaji wa Gazeti la JAMHURI. Leo tumetimiza miaka mitano (5) tukiwa sokoni tangu tulipochapisha nakala ya kwanza ya Gazeti la JAMHURI siku ya Desemba 6, mwaka 2011. Tangu siku ya kwanza tulitangaza bayana nia yetu ya kutumikia taifa. Tulieleza kuwa JAMHURI utakuwa uwanja huru.

Tulisema sera yetu ni kuwa JAMHURI halitaonea mtu, wala kumpendelea, bila kujali itikadi za vyama, dini, majimbo, mikoa, jinsia na kila liwalo katika kuwatumikia Watanzania na ulimwengu kwa ujumla. Kwa makusudi tuliamua kuwa tofauti. Tulikuja na kaulimbiu isemayo “Tunaanzia Wanapoishia Wengine.”

Shabaha na lengo letu ilikuwa ni kuifahamisha jamii kuwa tunaingia sokoni kutoa huduma hii ya magazeti kwa mtazamo mpya. Kwamba tuliamua tangu mwanzo kuwa gazeti hili liwe la uchunguzi. Tunafanya habari za uchunguzi kwa kina na habari hizi zimekuwa nguzo ya mabadiliko makubwa katika nchi yetu.

Tunajivunia ukweli kuwa katika kipindi cha miaka mitano tunaweza kusimama kifua mbele tukasema tumesaidia nchi hii. Kazi ya mikono yetu imeweza kuziba mianya ya uvujaji wa mapato. Serikali imeweza kukusanya fedha nyingi na za uhakika kutokana na watu waliokuwa wakikwepa kodi au kutenda ndivyo sivyo, lakini tulipowamulika wakanyooka na kufuata mkondo wa sheria.

Tunapenda kukumbusha habari chache kati ya nyingi tulizozichapisha baada ya kufanya uchunguzi kupitia gazeti hili la JAMHURI hadi nchi ikatambua uwepo wetu. Tumeshughulikia kwa kina uozo katika Bandari ya Dar es Salaam ukiwamo upotevu wa makontena. Tunafarijika kuwa Februari 13, 2016 Rais John Pombe Magufuli alitambua kazi ya Gazeti la JAMHURI, tulipochapisha habari ya flow meters za mafuta (TPA), na akatupongeza hadharani.

Tumefuatilia na kuchapisha habari za majangili na matumizi mabaya ya rasilimali zetu katika Idara ya Maliasili na Utalii. Tumechapisha habari juu ya wauza dawa za kulevya hadi Sheria ya Dawa za Kulevya ya mwaka 1995, mwaka 2015 ikabadilishwa na kutoa adhabu kubwa kwa wauza unga. Tumechapisha habari juu ya matapeli wa madini.

Katika sekta ya mafuta kupitia habari za uchunguzi tunazozichapisha, Gazeti la JAMHURI limeandika uovu kuhusiana na uchakachuaji na mafuta ya transit (ya kwenda nje) kuuzwa kwenye soko la ndani. Kampuni nyingi zimewajibishwa kwa mchezo huu ikiwamo Lake Oil iliyolipishwa sehemu ya kodi iliyokuwa imekwepa ya Sh bilioni 8.5. Tumeandika habari za Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuepuka kodi, ufisadi Ngorongoro na tumetetea watu wengi kwa nyakati tofauti waliokuwa wapokwe haki zao zikarejeshwa.

Tunapenda pia kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais John Magufuli. Serikali hii kwa kushirikiana na Waziri Mkuu wake, Kassim Majaliwa imekuwa sikivu. Tofauti na awamu zilizopita tulipokuwa tunachapisha habari tunaishia kuambiwa kuwa “kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala,” tukiandika, Rais Magufuli anachukua hatua na tunafarijika.

Tunawashukuru wasomaji wetu kwa kutuunga mkono kwa muda wote wa miaka mitano. Hatujawahi kukosa sokoni kila siku ya Jumanne hata mara moja. Safari hii imekuwa na mawimbi, wakiwamo watu wasiotaka uovu wao uwekwe hadharani na baadhi wamekimbilia kuzitumia mahakama. Wapo waliotufungulia kesi kupinga kisichopingika, lakini tunasema kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu kazi hii tutaendelea kuifanya kwa masilahi ya taifa. Tunawashukuru wadau wetu wa matangazo na tunaomba wakitangaza nasi watulipe kwa wakati tuweze kuendeleza kazi ya kusukuma gurudumu la maendeleo kupitia Gazeti la JAMHURI.

Kipekee tunaomba kuushukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF) kwa msaada mkubwa wa kutujengea uwezo kupitia Ruzuku ya Mabadiliko uliotupatia mwaka 2014/15. Ujuzi na vifaa tulivyovipata kupitia ruzuku hii, vimetuwezesha kufanya kazi hii kwa ufanisi wa hali ya juu. Tunawashukuru wafanyakazi wote wa JAMHURI kwa kujituma.

Mwisho, tunasisitiza kuwa kazi hii tuliyoianza tutaendelea kuifanya kwa nguvu na msukumo wa pekee unaolenga kulitumikia taifa letu kwa weledi, uadilifu na uaminifu kuhakikisha Tanzania yenye maendeleo ya kweli inafikiwa. Mungu ibariki JAMHURI, Mungu ibariki Tanzania.