Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwapo ongezeko la mitume na manabii wa uongo barani Afrika, hususan Tanzania, wanaohubiri mafanikio ya haraka kupitia miujiza, utajiri wa ghafla na baraka za kiroho zinazotokana na vitu kama udongo, maji, leso na mafuta.
Mafundisho haya, yakiungwa mkono na baadhi ya viongozi wa serikali, yameenea sana na yameanza kuwa sehemu ya maisha ya watu wengi, huku yakileta athari katika jamii.
Dini hizi za kitapeli hazina msingi thabiti wa kiroho, na badala yake zinajikita katika kudumaza watu, kuzorotesha maendeleo na kupotosha maadili ya kazi na maendeleo.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwenye kijitabu chake cha Tujisahihishe cha mwaka 1962, alisema haya: “Sababu moja ambayo ilituzuia sisi Waafrika kuendelea ni majibu ya urahisi kwa matatizo makubwa. Shamba letu kama halikutoa mavuno ya kutosha, jibu lilikuwa wazi; au limelogwa au ni amri ya Mungu. Watoto wetu walipokuwa wagonjwa daima, jibu lilikuwa rahisi; au walilogwa au ni amri ya Mungu. Nyumba yetu ilipopigwa radi ikaanguka, jibu lilikuwa rahisi; au ni uchawi au ni amri ya Mungu. Majibu ya namna hii huzuia binadamu kupata sababu za kweli za matatizo yao, na kwa hiyo yanazuia akili kutafuta njia za kweli za kuondoa matatizo hayo…Mungu ametupa akili ili tuweze kuzitumia kwa manufaa yetu na ya jumuiya.”
Kwa hali tuliyonayo kama jamii na taifa, matumizi yetu ya akili yamekuwa madogo mno kiasi kwamba kufeli kwetu sasa tumeamua tutumie udongo na mafuta kujitakasa ili tuwe na maisha bora. Wazungu, Wachina, Waarabu na Wahindi wanatucheka kweli kweli. Watu wanawaza kwenda kuishi sayari za mbali sisi bado tunahangaika kutafuta mifuko ya kujaza udongo, na kwenda kukanyaga mafuta! Viongozi wakuu wa nchi nao wanabariki vituko hivi.
Katika makala hii, naangazia hatari zinazotokana na kuamini mafundisho haya na jinsi yanavyokwamisha maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Moja ya athari kuu ya mafundisho haya ni ujinga unaojazwa vichwani mwa watu. Mitume na manabii wa uongo hueneza imani ya kipumbavu kwamba vitu kama udongo, maji, leso na mafuta yana uwezo wa kumtajirisha mtu au kumletea miujiza ya kifedha.
Wakati watu wanapoanza kuamini kuwa mali na ustawi wao utatokana na vitu hivi badala ya juhudi zao wenyewe, wanapoteza kabisa msingi wa kufikiri kwa mantiki.
Badala ya kutafuta elimu, kubuni miradi ya kiuchumi, au kujituma katika kazi, watu huanza kushirikiana na matapeli hawa kwa imani kwamba watapokea utajiri kupitia miujiza ya ghafla.
Mafundisho haya yanawafanya watu kuwa wategemezi wa miujiza badala ya kuwa wachapa kazi na wabunifu. Badala ya kufikiri jinsi ya kuboresha maisha yao kupitia elimu, biashara au kilimo, watu wanashawishiwa kwamba miujiza ndiyo suluhisho la matatizo yao yote.
Ujinga huu unadumaza maendeleo ya taifa, kwa kuwa nguvu kazi inayoaminiwa na taifa inaanza kuacha kushiriki kikamilifu katika uzalishaji na kujenga jamii yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Mitume na manabii wa uongo wanapohubiri mafanikio bila kazi, wanawafanya watu waamini kuwa mafanikio ya kiuchumi hayatoki katika juhudi binafsi, bali kupitia miujiza.
Hii inachangia kuzorota kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla. Watu wengi wanapotumia muda wao mrefu katika mikutano ya kidini wakisubiri miujiza ya kifedha badala ya kufanya kazi, sekta muhimu za uchumi kama kilimo, biashara na uzalishaji zinadumaa.
Utafiti umeonyesha kuwa watu wanapopoteza imani katika kazi ngumu na kuanza kutegemea miujiza, uzalishaji wa taifa hupungua kwa kiwango kikubwa.
Katika taifa lolote linalotaka kujikwamua kiuchumi, ni lazima watu wawe na mtazamo wa kujituma, kuwekeza katika elimu, na kuboresha ujuzi wao.
Hata hivyo, mafundisho ya mitume hawa matapeli yanawafanya watu kutokujali elimu na ujuzi, hali inayozuia ubunifu na ujasiriamali, vitu ambavyo ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi.
Mitume na manabii wa uongo wanaohubiri utajiri kupitia miujiza bila kufanya kazi wanachangia kudhoofisha maadili ya kijamii. Watu wanapoanza kuamini kuwa mafanikio yao yatatokana na baraka za kiroho badala ya juhudi binafsi, wanapoteza uwajibikaji na maadili ya kazi. Taifa ambalo watu wake wanakosa uwajibikaji na maadili linakabiliwa na changamoto kubwa za maendeleo. Ujinga huu uko zaidi Afrika.
Kwa mfano, watu wengi wameanza kushiriki vitendo vya udanganyifu, wizi, na ufisadi kama njia za haraka za kupata utajiri. Badala ya kufuata njia halali za kufanikiwa, watu wanakimbilia kwa mitume hawa wakiamini kuwa baraka zao zitaleta mafanikio bila kufuata misingi ya haki, uadilifu na uaminifu.
Mafundisho ya mitume na manabii wa uongo yanakwamisha sana maendeleo ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Afrika inahitaji nguvu kazi iliyo na elimu, ujuzi na motisha ya kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo ya maendeleo.
Hata hivyo, mafundisho haya yanapotosha watu na kuwafanya waamini kuwa maendeleo na ustawi wao hautatokana na juhudi zao binafsi, bali kwa msaada wa miujiza ambayo mara nyingi mtu mwenye akili unashindwa kuelewa ni kwa nini watu wanaangukia kwenye utapeli huu?
Matokeo yake, taifa linalotegemea mafundisho haya linakosa mwelekeo sahihi wa kiuchumi. Sekta za elimu, afya, viwanda na kilimo, ambazo ni mihimili ya uchumi, zinakosa watu wa kuzihudumia kikamilifu kwa sababu wengi wanakimbilia kwenye mikutano ya kidini wakisubiri miujiza.
Kati ya matatizo makubwa yanayochangia kuenea kwa mitume na manabii wa uongo ni ukimya wa viongozi wa serikali, na wakati mwingine kuonekana wakiunga mkono au kushiriki katika shughuli hizi za kitapeli. Wakati viongozi wa kisiasa wanapoamua kunyamazia uongozi wa kidini unaowapotosha wananchi au hata kushirikiana nao, wanatoa uhalali wa shughuli hizo kwa watu wa kawaida.
Ukimuona Makamu wa Rais anashiriki shughuli hizi zinazoendana na watu kugawiwa udongo wa ‘baraka’, au Rais anapotoa ‘fungu la kumi’ kwa matapeli wa kiroho, jamii isiyo na elimu itashindwaje kuamini haya mambo?
Eneo ambalo lilikuwa kiwanda kiliachoajiri watu mamia kwa mamia, kiwanda kilichosindika ng’ombe waliofugwa maeneo mengi nchini, leo kimegeuzwa kuwa uwanja wa maombi ya kupata ajira! Tumelogwa na nani?
Viongozi wakuu wanapohudhuria au kuunga mkono hafla za mitume hawa, wanawapa nguvu na uhalali, hali inayowafanya wananchi waamini kuwa mafundisho hayo ni sahihi.
Hii inaathiri vibaya maendeleo ya kiuchumi kwa sababu wananchi wanapoona viongozi wao wakishiriki katika mikutano ya miujiza badala ya kuhamasisha kazi na elimu, wanaamini kuwa mafanikio yao yanaweza kupatikana kupitia njia za mkato.
Viongozi wa serikali wanapaswa kuwa mstari wa mbele kulinda maadili ya kazi, elimu, na juhudi za kibinafsi kama misingi ya maendeleo ya taifa. Wanapoamua kunyamazia au kubariki utapeli wa kidini, wanadumaza juhudi za wananchi kujiletea maendeleo kwa njia halali. Uongozi ni kuonyesha njia, na hiyo njia ni ile iliyo sahihi, si njia ya kuonyeshwa viwanja vya miujuza.
Athari nyingine kubwa ya kuamini mafundisho ya mitume na manabii wa uongo ni kuongezeka kwa matatizo ya kijamii, kama vile umaskini, ukosefu wa ajira, na kuporomoka kwa maadili ya familia.
Watu wengi wanapopoteza mali zao kwa kuamini kuwa watapata utajiri kupitia miujiza, wanajikuta wakikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Wengine wanakabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, kama vile msongo wa mawazo na unyogovu, kwa sababu miujiza waliyoahidiwa haikutokea.
Hali hii pia inavuruga mshikamano wa kijamii, ambako watu wanaanza kuhisi kukata tamaa na kutafuta njia mbadala za kuishi, ikiwa ni pamoja na vitendo vya kihalifu. Taifa linalokumbatia mafundisho haya linakabiliwa na hatari ya kusambaratika kwa misingi ya kijamii, ambako watu wanakosa mwelekeo sahihi wa maisha. Vitendo vingi vya kihalifu vinavyotokea nchini si kwamba vinasababishwa na waganga wa kienyeji tu, bali vingine vyanzo vyake ni huku kwa mitume na manabii matapeli.
Kuamini mafundisho ya mitume na manabii wa uongo wanaohubiri utajiri, miujiza na mafanikio bila kufanya kazi ni hatari kubwa kwa taifa. Mafundisho haya yameenea sana nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla, yakiwa na athari mbaya kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Ujinga unaopandikizwa katika akili za watu unadumaza maendeleo, huku viongozi wa serikali wakishindwa kuchukua hatua za kuzuia ueneaji wa mafundisho haya ya kitapeli – pengine kwa sababu ni rahisi kuwatawala watu wajinga wanaoamini udongo unaochukuliwa kwa staili ya kiushirikina ni chanzo cha wao kutajirika.
Taifa lolote linalotaka kufanikiwa linapaswa kupinga mafundisho haya na kuhamasisha juhudi binafsi, elimu na maadili ya kazi kama misingi ya maendeleo ya kudumu. Viongozi wetu hawathubutu kuzuia utapeli huu kwa sababu, ama wenyewe ni wanufaika wa ujinga huu kwenye jamii, au wanaogopa kukemea ili wasionekane wanampinga Mungu! Mimi namsemea Mungu wa kweli aliyetuagiza tuishi kwa kazi, si kwa miujiza na kamari.
0759 488955