Katika kuwajali mashujaa waliopigania Uhuru na heshima ya Tanzania mwaka 1968, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha TANU chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, iliamua kuweka siku maalum ya kuwaenzi mashujaa hao. Ikachaguliwa Septemba Mosi kila mwaka iwe Siku ya Mashujaa Tanzania.

 

Septemba 1, 1969 ikaadhimishwa Siku ya Mashujaa kwa mara ya kwanza Tanzania. Wakati ule TANU ilikuwa na sababu mbili za msingi za kuchagua Septemba Mosi kuwa Siku ya Mashujaa.

Kwanza, ilikuwa siku kama hiyo (Septemba Mosi) mwaka 1905 Gavana Mjerumani, Adolf Graf Von Grotzen, alipotuma simu kwao Ujerumani kuomba msaada baada ya Wajerumani kuzidiwa katika Vita ya Majimaji iliyopiganwa Kusini mwa nchi yetu kuanzia Julai 28, 1905 mpaka Januari 14, 1907.

 

Pili, ilikuwa siku kama hiyo mwaka 1964 Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipozaliwa, ambapo linaundwa na mashujaa wapiganaji na walinzi wa mipaka ya Tanzania. Ukaja mwaka 1978. Oktoba 30, 1978 majeshi ya Uganda yalivamia Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kwa amri ya dikteta Idi Amin Dada.

 

Novemba 2, mwaka huo, Amiri Jeshi Mkuu, Rais Julius Nyerere, akatangaza vita dhidi ya majeshi ya uvamizi Kampala, mji mkuu wa Uganda kutekwa Aprili 1979 na wapiganaji shupavu wa Tanzania. Vita ya Kagera ikamalizika mwanzoni mwa Julai mwaka huo.

 

Julai 25, 1979 mashujaa waliopigana Vita ya Kagera wakapokewa Kambi ya Kaboya, mkoani Kagera wakitokea Uganda.

 

Ghafla tukasikia Julai 25 imechaguliwa kuwa Siku ya Mashujaa! Sababu? Ndiyo siku ambayo walipokewa wapiganaji wa Tanzania wa JWTZ wakitokea Uganda baada ya kumalizika Vita ya Kagera.

 

Hakuna asiyeenzi kazi iliyofanywa na wanajeshi wa JWTZ katika vita hiyo. Hata hivyo, uamuzi wa kubadili Siku ya Mashujaa kuwa Julai 25 badala ya Septemba Mosi ulifanywa kimakosa na zaidi kisiasa: Kulifurahisha JWTZ.

 

Kwanza, wakati tunakubaliana kwamba mapambano katika Vita ya Kagera yaliyoongozwa na Mkuu wa JWTZ, Abdallah Twalipo, si sahihi kuleta picha kwamba waliopigana vita hiyo ni wanajeshi wa JWTZ peke yao. Hapana. Wanajeshi na Polisi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Mgambo walishiriki vita hiyo wakachangia ushindi.

 

Pili, hakukuwa na sababu yoyote ya msingi ya kutupilia mbali Septemba Mosi kuwa Siku ya Mashujaa. Ni upotofu usiovumulika kuleta picha kwamba waliopigana Vita ya Kagera ndiyo watu muhimu zaidi kuliko wale waliopigana Vita ya Majimaji, Vita ya Mkwawa, Vita ya Isike, Vita ya Meli, Vita ya Machemba, Vita ya Makunganya, na kadhalika.

 

Ungeweza kusema kwamba hao ndiyo waliokuwa mashujaa zaidi ukizingatia kuwa walishika silaha hafifu kama mikuki, pinde, mishale na migobore (bunduki zilizoliwa na kutu), wakayakabili majeshi ya Wajerumani yaliyokuwa na bunduki za kisasa na mizinga.

 

Kikubwa zaidi tunapotosha historia ya Tanzania kuleta picha kwa watoto wetu kuwa kabla ya Vita ya Kagera nchi hii haikuwa na mashujaa.

 

Lengo la Siku ya Mashujaa ya awali lilikuwa kuwaenzi mashujaa wote wa Tanzania ikiwa ni pamoja na wale waliomwaga damu Zanzibar Januari 12, 1964 wakitafuta Uhuru wa walio wengi.

 

Kwa hivyo, tuweke kando siasa za kuwafurahisha wanajeshi, turudi kwenye mstari bila kuona aibu. Tuone kosa tulilofanya, Septemba Mosi irudi kuwa Siku ya Mashujaa Tanzania.

 

Tena, tusiifanyie mzaha siku hiyo. Iwe Sikukuu ya Taifa ambapo wananchi wa kila pembe ya Tanzania watakusanyika vijijini na wilayani kuwaenzi mashujaa wa maeneo yao kwa nyimbo, mashairi, ngonjera na ngoma.

 

Kama itaonekana kuwa sikukuu za Taifa ni nyingi mno, basi tufute siku ya kupeana zawadi (Desemba 26) ambayo haina maana yoyote kwa Mtanzania. Siku ya Mashujaa ina maana kwa kila Mtanzania na kila mzalendo.