Kwa kuwadokeza tu, vijana wale niliwasimulia juu ya chombo kimoja cha muziki tulichokitumia enzi za ukoloni. Chombo chenyewe kinaitwa santuriI (kwa Kiingereza ni gramaphone) ni sanduku la muziki lenye kamani ndani yake na mkono (handle).
Lakini cha muhimu sanduku lile la muziki au santuri ilikuwa na picha ya tarumbeta, na mbele ya hiyo tarumbeta kuna picha ya mbwa aliyekaa akisikiliza muziki. Pia yalikuwapa maandishi juu ya picha ile na juu ya sanduku lile yalisomeka hivi: His Masters Voice” au HMV.
Hii santuri ndiyo tukisikiliza muziki wa Jimmy Reeves, Baba Gastone au Miziki ya Kongo, Ulaya na Cuba tulipata sahani zikiitwa GV hata nyimbo za Fundi Konde, yule mwanamuziki wa Mombasa, aliyeimba “Embe dodo limelala mchangani. Kwa huba na mazoea, uwe wangu wa moyoni”.
Hadithi hii ilionesha mbwa anavyofaidi muziki wa bwana wake. Basi kisiasa huko nyuma sisi wazee kila tulipomuona msomi anaigiza Uzungu kitabia kwa mavazi na miondoko tukimwita “His Master’s Voice” kumaanisha anafurahia asiyoyaelewa wala yasiyomnufaisha!
Hivyo, mwanasiasa asiye na uzalendo anayepokea miongozo kutoka Ulaya au nje ya nchi hana uzalendo, ni HMV. Anapayuka yale (anayotumwa kuyatamka. Si yeye mwenye (not himself but he is a chatter box) hapo basi ni msambazaji ujumbe tu kwa wasikilizaji (no originality ndani yake).
Tunawaomba nyinyi wasomi wetu msiwe HMVs hapa nchini. Kule vijijini mnakotoka si mnakujua? Wengine tunalala na mifugo ndani ya nyumba zetu. Leo tukishaingia vyuoni tunaanza kudai yasiyotekelezeka. Anasa haiji bila kazi au jasho. Ukiona mtu mpiga kelele sana kudai hili au lile ujue kwao hakuna hata choo cha shimo bado anakwenda kujisaidia porini! Ni maskini wa kutupwa huyo!
Nikawakumbusha maneno aliyosema Baba wa Taifa, Oktoba 1966 juu ya watoto wanaosoma chuo kikuu, alitumia maneno haya. Nanukuu “Na wote tumetoka kwa baba maskini, mama maskini, mjomba maskini, jamaa zetu maskini. Mimi nimezaliwa katika nyumba ya mbuzi, ijapokuwa Mzee Nyerere ni Chief, lakini uchifu wenyewe wa ovyo. Nyumba hizi hizi za msonge imegawanywa katikati upande wa kule ndiko kuliko na kitanda na jiko na upande wa huku ndipo tunaweka vigingi na kufungia ndama na mbuzi. Na kuku humo humo. Mimi (Mwalimu Nyerere) nimezaliwa na kukulia katika nyumba hiyo. Sijui hali zenu wenzangu, lakini nadhani wengi wetu hali yetu ni ile ile” (Hotuba ya Mwalimu kwa wananchi mwaka 1966 kutokana na wasomi wa vyuo kudai kugomea mwito wa JKT uk. 14).
Vijana si ya kweli haya? Zile nyumba za Ngondani za Waha kule Kigoma, za mushonge/Nyalusu kule Kagera, za makuti huku pwani kote kutoka Tanga hadi Mtwara au za matembe huko Dodoma si ndiko tulikozaliwa, tumekulia humo na kutokea huko mpaka sasa tumebahatika kuingia katika haya maghorofa ya vyuo vikuu? Babu zetu hawakubahatika kulala katika nyumba namna hii mnazolala nyinyi vyuoni jamani.
Hapo vijana walitabasamu wakaangaliana bila kunibishia. Ndipo nikawauliza, je, msimamo au mwelekeo wangu mlivyo ni-assess uko wapi? CCM au UKAWA au Utanzania?
Wangapi miongoni mwa vijana wa leo wanajua kwamba Rais Dk. John Magufuli anatekeleza kikamilifu Ilani ya Uchaguzi ya Chama chake? Haya tunayoyaona anafanya yako katika sera za Chama Tawala tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Hapo nilichukua kijitabu cha Hotuba ile ya Mwalimu kwenye Sabasaba ya 1981 aliyotoa kule Kigoma. Sikusoma kitabu kile chote bali niliwaonesha maneno katika kurasa wa 6, 10 hadi 11 na uk. 17 wa kitabu chenye kichwa “Tusikubali Kudanganywa”.
Kwa faida ya wasomaji wa makala hii nimeonelea afadhali ninakili yale waliyoona vijana wale ili wasomaji wajisomee wenyewe. Tuanze na hili jambo la kufanya usafi wa makazi yetu siku ya sikukuu ya Jamhuri aliloamuru Rais wetu kupunguza hatari za kipindupindu nchini.
Mwalimu Nyerere, namnukuu hapa, alisema hivi, “Sasa ni kweli kwamba Serikali ya watu lazima ijitahidi kutekeleza matakwa ya watu na kwa matumaini hayo ni kwamba mara nyingi mambo ambayo yatafanywa na Serikali hiyo yatakuwa ni mambo ambayo yanapendeza kwa wananchi. Kwa sababu ni mambo yanayotokana na matakwa yao wenyewe. Lakini binadamu ni binadamu. Na Serikali ni Serikali. Kwa hiyo kuna wakati mambo hayo ni mazuri kufanya lakini kuna watu ambao hawapendi-pendi japo ni mazuri. Na ikifika hapo Serikali inasema – “utafanya” lazima Serikali yoyote iseme “utafanya”.
Usafi wa miji ni usafi wa miji yote. Tunataka miji iwe safi. Lakini haiwi safi bila ya kufagia. Haiwi safi bila kuwa na pipa la takataka mbele ya nyumba yako na unaposafisha takataka lazima uzimwage katika pipa. Halafu zije zisombwe. Lazima ziwepo taratibu hizi ama sivyo usafi hautakuwapo”. (Hotuba ya Mwalimu J. K. Nyerere Tusikubali Kudanganywa” Kigoma Julai 7, 1981 uk. 67).
Kama haya yangefanyika tangu Julai 7, 1981 mnafikiri leo hii Rais wetu, Dk. Magufuli, angesema tuache sherehe za Jamhuri tujikite kwenye usafi wa makazi yetu? Mbona yeye mwaka 1981 alikuwa bado kijana katika masomo? Amegutuka kuona Watanzania tumebweteka na sherehe na kusahau athari za uchafu katika makazi yetu.
Hivyo kwa uwajibikaji wake na mapenzi kwa Taifa lake ndipo leo ametukumbusha umuhimu wa USAFI katika makazi yetu. Ni azma ya Baba wa Taifa tangu mwaka 1981. Hatuna budi kumsifu Rais Dk. Magufuli kwa kuthubutu kuturudisha katika utendaji kazi wetu.
Rais ameliibua hili suala la usafi wa nchi nzima kwa faida na afya zetu. Lakini wapo wale waliozoea posho (per-diem) za sikukuu, hili limewaudhi na hawalipendi. Serikali imeokoa mamilioni ya shilingi na ndizo zinazotengeneza baraba ile ya Mwenge-Morocco. Wakinuna shauri lao!
Tukija kwenye hili suala la kipato miongoni mwa Watanzania kutofautiana ambalo Rais leo anadai wakwepa kodi walipe ili sote tufaidi matunda ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alisema hivi namnukuu tena, “Sisi tumeamua kwamba Serikali ijitahidi kuleta maendeleo ambayo yatapunguza-punguza tofauti baina ya watu. Wengine wana hali nzuri sana na wengine wana hali ndogo sana. Wale wenye hali za chini ndiyo wanaofanya kazi. Tumesema kwamba jitihada yetu Tanzania si kuongeza mtaji tu. Siyo kwamba tunataka kuongeza mali tu nchi ilundikane na mali.
Tunayo shabaha ya pili ya mali hiyo. Mali kwa desturi ya maumbile ni sawa na mwangaza. Kwa desturi ya mwangaza, unapoingia ndani ya chumba lazima giza likimbie. Ni mwiko kabisa mwangaza kuwepo na giza bado liwepo.
Katika hali ya kawaida ingekuwa vizuri kwamba penye mali hapana maskini. Lakini sivyo ilivyo. Kwa desturi za kibepari inawezekana nchi ina mali lakini watu wanaendelea kuwa maskini. Mali ipo lakini inamilikiwa na vikundi vidogo sana. Vinatumika kuonea wenzao. Kwa hiyo, mali na umaskini zinaishi maisha haramu sana pamoja”. (Hotuba ya Mwalimu Kigoma Julai 7, 1981 ”Tusikubali Kudanganywa” uk. 10 – 11).
Jamani, mmesikia yaliyowasibu maofisa wa TRA kuwa na nyumba zaidi ya moja (naambiwa wengine wana nyumba 73 mtu mmoja). Kule Bandarini maelfu ya makontena yametolewa bila kulipiwa ushuru na kadhalika. Ndipo Rais Magufuli sasa anataka mali za nchi tufaidi sote. Hapo anakosea nini? Watanzania wachache wale wenye mali wanalia lakini mamilioni ya wananchi wanatazamia mali za nchi ziondoe umaskini uliokithiri na haki itendeke kwa wote. Rais anataka aongeze fedha kule Hazina ili aweze kumudu kutoa huduma za jamii kwa wote.
Mtazamo wangu, fedha za ushuru hizo zimalize kabisa malipo ya madai ya walimu na waganga wa nchi hii zilipie mikopo ya wanachuo vyuoni kama nyinyi. Kisha zipangiwe kuwalipa pensheni au malipo ya uzeeni wazee wote wa nchi hii ili nao wafaidi matunda ya Uhuru waliopigania. Hii itawawezesha kununua chumvi, sabuni, sukari, mafuta ya taa na mahitaji muhimu. Matajiri wamezidi kututambia.
Katika kumalizia mazungumzo yetu na wale vijana wa chuo kikuu, niliwaonesha ibara ya mwisho kabisa ya ile hotuba ya Mwalimu ya 1981 ambayo ilisema hivi nanukuu hapa “Lakini katika nchi hizo maskini zenye nafuu katika hali ya umaskini ule ni zile ambazo zina siasa ya kijamaa. Na wakubwa hawataki nafuu hiyo ionekane au idhihirike. Wanapenda kuziyumbisha nchi hizi. Sisi tunafanya kila jitihada tusiyumbe. Tuendelee hatua kwa hatua kujenga nchi ya usawa”. (Hotuba ya Mwalimu Nyerere Kigoma, Julai 7, 1981 uk. 17).
Hiki ndicho Rais wetu anachojitahidi kuwafanyia Watanzania wote. Nia ni kupunguza hali ya tofauti (gap) kati ya walio nacho na wasionacho.
Vijana mnajua vyama vya siasa kiasili havina uwezo kifedha. Basi vipo vyama vinapata misaada kutoka marafiki zao ng’ambo – Ulaya Magharibi. Huwezi kupata msaada usiokuwa na masharti. Hivyo vijana msiyumbishwe na kudanganyika na watoa misaada eti wanawapenda, NG’OO!
Rais Dk. Magufuli anafuata nyayo za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, anakuwa mtumishi wa wanyonge na wahitaji wa Taifa letu. Mnapaswa kumsaidia, kumuunga mkono na hasa mbadilike kifikra na kimtazamo (be mentally liberated).
Baada ya mazungumzo yetu yale (wala chai sikuwapa maana sina uwezo), nikamalizia kwa kuwaonesha ujumbe ulioingia katika simu yangu wakati tukizungumza hapa hapa nyumbani pangu. Nikawasomea maana haukuwa wa siri. Ujumbe ulisema “Salaam, samahani (sorry) nimeona nikutakie heri za X-Mass na Happy New Year mapema maana Magufuli anaweza kuzifuta sherehe hizi maana simwelewi elewi” Desemba 5, 2015.
Nikasema vijana msiogope namna hii. Sisi walimu wa sayansi ni“very reasonable na compassionate people”. Nchi yetu kwa wakati huu inahitaji kiongozi mtoa uamuzi kwa manufaa ya Taifa. Rais hawezi kufuta sikukuu za kidini jamani. Kwani yeye hana dini? Msimhukumu namna hiyo.
Hapo nikasema tu kuwa tunachokihitaji kwenu vijana ni ukomavu na kupevuka kisiasa. Kwanza tuachane na tamaa za ubinafsi, pili muwe na moyo wa kutumikia wahitaji. Hiyo political science mnayosomea isije kuwafanya vivuli vya Wazungu mkajikuta nanyi mu miongoni mwa ‘His Master’s Voice’ kama baadhi ya wasomi wengine walivyo hivi sasa.
Wanafanya mambo yao mie naita “kistereotyped” walivyosomea vitabuni. Hapo wanajifanya kama siyo wazawa wa nchi hii bali wao wanajiona ni Wazungu weusi. Hii kasumba mbaya sana muiache. Tuliagana kwa amani.
Mimi naamini waliridhika tukaachana wakaenda zao.
Kwenu wasomaji wa makala zangu wote naomba niwatakieni HERI ya X-MASS pia niwatakie fanaka katika maisha yenu kwa mwaka ujao 2016. Mungu atubariki sote tuonane mwaka huo.