Awamu ya kwanza ya harambee ya ujenzi wa kituo cha yatima, shule ya sekondari na msikiti Patandi, Arumeru mkoani Arusha, imefana kwa kiwango kikubwa na kuwa miongoni mwa vielelezo muhimu vya kuuendeleza umoja na mshikamano wa Watanzania bila ya kujali madhehebu, rangi na dini.
Hamasa iliyojitokeza katika viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa jijini Arusha, imenikumbusha moja ya mafunzo makuu niliyoyapata kutoka kwa mwalimu wangu wa sayansi ya tabia na mwenendo wa viumbe (behavioral science), Dk. Masalakulangwa Mabula.


Katika mengi ya madarasa yake alikuwa akipenda kutuambia kuwa ‘mambo huendeshwa’ kamwe hayajiendeshi yenyewe. Mambo makubwa hutakiwa kuendeshwa na kusimamiwa na wajuzi wenye weledi nayo ‘kindakindaki’.
Maneno haya tunduizi yamekuwa yakijirudia bongoni mwangu na pia kunifanya kumkumbuka baba wa mama yangu mzazi, Al marhum Jumbe Kapteni Mkopi, Mola amrehemu na amlaze Mahali Pema Peponi.


Swahiba wangu huyu akipenda kutuwaidha kuwa ‘Wawekeni watu kwenye nafasi zao’ ili kusiwe mwanzo wa anguko na kushindwa kwa vingi. Ajenda ya waumini wa Kiislamu jijini Arusha ni kuona mafanikio makubwa ya ujenzi wa kituo hicho, wakiikumbuka dhima ya binadamu mbele ya Mola muumba kuwasaidia yatima na wasiojiweza huku wakiwalea vyema na kuwafanya wawe bora kiimani, kimaadili na kiraia. Hakika huko ndiko kuijenga dunia na kuifanya mahali salama na kutarajia malipo yasiyokatika.


Katika kuliendea hilo, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, aliombwa kuwa mgeni rasmi wa kusimamia harambee, lakini kutokana na majukumu yaliyombana hakusita kumtafuta na kumuagiza mtu mwenye sifa ya kusimamia na kufanikisha harambee hiyo.
Ikumbukwe imekuwa ni ada kuwatafuta na kuwaalika watu wenye mvuto, ushawishi, kupendwa na hata kuaminika kuliko kukubwa na jamii kusimamia harambee mithili ya hii ndani ya nyumba za ibada, mashuleni na maeneo mengine.


Ni ukweli  usio mawaa na usiohitaji tochi kuumulika kuwa waratibu wa hafla za harambee hujipanga vyema kuhakikisha malengo yao yanafikiwa kwa mafanikio makubwa kwa kumpata ‘mtu wa watu’, awezaye kuhanikiza hamasa ili waliokuwapo waweze kutoa kile ambacho ni vigumu kukitoa iwapo jukumu la usimamizi angekabidhiwa mtu mwingine asiye na sifa za kufikia ‘kaliba’ yake.


Kwa mapenzi yake makubwa na waumini wa Kiislamu Arusha na kwingineko, Edward Lowassa alitanabahi heshima ya kuagizwa na Makamu wa Rais, Dk. Bilal, akajumuika na kuiongoza harambee hiyo iliyomalizika kwa kufanikisha kupatikana kwa michango ya shilingi zaidi ya milioni 235.
Michango hiyo ikitolewa na waumini wa Kiislamu na wachangiaji wengine wenye hamu ya kuona maendeleo bila ya kujali tofauti za kidini. Wako marafiki wa Lowassa wakiongozwa na Mathias Manga, mjumbe wa NEC (CCM) Arumeru. Kwa uchache walikuwapo wabunge – Peter Serukamba, Namelock Sokoine, Sioyi Jeremiah Sumari na wengineo waliochangia jumla ya Sh. milioni 20.


Kwa upande wake, msimamizi na mgeni rasmi wa harambee hiyo, Lowassa, Makamu wa Rais (hakuwapo), marafiki zake Lowassa walichanga kiasi cha Sh. 105 milioni, mbali ya ahadi ya Sh. milioni 50. Ikumbukwe kukamilika kwa ujenzi huo wa ghorofa tano kunatarajiwa kugharimu Sh bilioni moja, na hapa ninaamini kuwa kwa hamasa kubwa iliyokuwapo siku ile ya awamu ya kwanza ya uchangiaji, kiasi hicho kilichobakia kitafikiwa iwapo kutaendelezwa mshikamano uliooneshwa na wote waliojitokeza.  


Kwa maneno yake Lowassa alinukuliwa akisema: “Hii ndiyo Arusha ninayoijua mimi, tumeishi kwa upendo na amani miaka mingi, tusikubali kugawanywa kwani sote ni binadamu tulio sawa.” Hakika hayo ni maneno adhimu na yaliyotuama hasa kwa faida ya afya na utengamano wa Taifa letu.
Taifa hili litaendelea kuwa moja dahari, iwapo tutaendelea kuziishi tunu zetu za kuendelea kufahamiana, kuwa na ada ya kujifunza kutoka kwa wengine na yale yaliyo ya wengine huku tukivumiliana kwa tofauti zetu za kidini, kiitikadi na mitazamo.


Nimalizie kwa kusema kuwa safari ya kukamilika ujenzi wa  kituo cha watoto yatima, shule na msikiti hapa Patandi imeongezewa kasi na harambee hii na hakuna shaka binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.