Hakuna wiki inayopita bila taifa letu kuingizwa kwenye mijadala. Mijadala yenye tija ni kitu cha maana. Shida ni pale tunapojikuta tukihangaishwa na mambo yasiyokuwa na faida yoyote – si kwa mtu binafsi wala kwa taifa letu.

Kwenye mitandao ya kijamii tumesoma habari kuwa Serikali ya Kenya imesaini makubaliano na Serikali ya Afrika Kusini kwa ajili ya kupeleka walimu wa somo la Kiswahili nchini humo.

Itakumbukwa kuwa Afrika Kusini imeridhia Kiswahili kifundishwe katika shule na vyuo; lengo likiwa kuwasaidia wananchi wa taifa hilo kuachana na lugha za kikoloni na kuanza kuzikumbatia lugha za Kiafrika.

Niliwahi kuandika jambo kama hili nchini nikiwa Comoro. Nakumbuka Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania wa wakati huo, Bernard Membe, na Rais Jakaya Kikwete, walisisitiza sana umuhimu wa Watanzania kuanza kunufaishwa na fursa za ukombozi wanaoufanya katika mataifa mbalimbali.

Ukiacha fursa za kibiashara, fursa nyingine kubwa kabisa nchini humo ni walimu wa Kiswahili na mahitaji ya vitabu vya ziada na kiada vya lugha hii adhimu. Wacomoro wanataka kujifunza Kiswahili. Wanakipenda. Hawana walimu. Baada ya kulijua hilo, Kenya wakawa wa kwanza kupeleka vitabu na walimu. Sisi tuliohangaika na ukombozi wa Comoro tangu miaka ya 1970 tumelala.

Kenya haina mchango wowote wa maana kwenye ukombozi kwa Comoro, Afrika Kusini au mataifa mengine ya Afrika. Tanzania tumeshiriki ukombozi kwa hali na mali. Kuna makaburi ya ndugu zetu wengi katika mataifa tuliyoshiriki kuyakomboa. Leo tulipaswa kupata malipo ya damu za Watanzania wenzetu kupitia fursa kama hizi za elimu na biashara.

Tuna bahati mbaya kuwa katika kipindi ambacho tunapaswa kuzisaka na kuzidaka fursa hizi, tumeendeleza mijadala ya Bunge na CAG. Tumeendelea na mjadala wa Spika na Naibu Rais wa Bunge la Afrika. Tumeendelea na nani afanye mikutano na nani asifanye.

Katika ulimwengu wa leo ambao watu wanabangua bongo ili kujiletea maendeleo, sisi bado tunawaza kuua vyama vya siasa vya upinzani. Tunaona fahari hata kumuomba rais atawale milele!  Tunapoteza muda na rasilimali kufunguliana kesi za ghiliba. Tunahangaika na viwango vya kodi ambavyo vinaamuliwa na maofisa wa TRA kwa mfumo wa ramli. Hakuna viwango vinavyojulikana, na hata kama vipo vinapuuzwa. Ni kama tumeweka kando mizani na kuamua kutumia macho kupima uzito wa nyama!

Tunapuuza mambo ya msingi ya uchumi na kuamua kuamini kuwa bodaboda ndiyo ajira mahususi na yenye tija kwa kizazi hiki na kijacho. Wanaoutaka uongozi wanaahidi bodaboda kwa vijana.

Muda wa kujadili hatima ya elimu kwa vijana wa taifa letu hatuna. Tumekubali mfumo wa elimu utokane na utashi wa wanaoingia madarakani. Wakitoka wanatoka nao. Ndiyo maana leo tunaweza

kuambiwa hakuna somo la historia, kesho tukaambiwa hakuna michezo shuleni! Tunageuzwa kama chapati. Hata jeshini aina ya gwaride haitokani na nani ni mkuu wa jeshi kwa wakati huo. Hakuna anayehangaika kujiuliza haya masomo wanayopata vijana wa taifa hili yatawawezeshaje kumudu maisha yao na ya taifa lao?

Hatuna muda wa kujadili umuhimu wa elimu ya ufundi katika nchi yetu badala yake kila mbunge anayesimama anaulizia fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu. Nchi gani imeendelea kwa elimu ya vyuo vikuu pekee? Nchi gani ina idadi kubwa ya makandarasi kuliko mafundi mchundo? Hatuna muda wa kuyajadili haya.

Tunahimiza kuwa na Tanzania ya viwanda, lakini tunawaandaa vijana wa Tanzania kuwa wachuuzi. Leo tunaona sifa ya kuwa nchi ya wachuuzi. Hatuwezi kujinasua kwenye umaskini kama mipango yetu itakuwa ya kuwa na wamachinga wengi badala ya wazalishaji viwandani na mashambani.

Tunapaswa kuwa na mipango ya kuwafanya vijana waone ni udhalili kuwa wamachinga, badala yake wajikite kwenye shughuli nyingine za uzalishaji. Hatuwezi kuacha kilimo kiwe kazi ya wazee halafu tutarajie mapinduzi katika maendeleo yetu.

Si rahisi watu wote wa taifa kuwa na mawazo au mijadala yenye tija. Hilo haliwezekani. Hata hivyo, wenye kutusaidia kuondoka kwenye mijadala rahisi rahisi ni viongozi wetu waliopewa dhamana ya kutuongoza.

Fursa kama hii ya kufundisha Kiswahili Afrika Kusini, Comoro, Marekani na kwingineko duniani sharti tuichangamkie. Tupunguze songombingo, fitina, husuda na mijadala isiyokuwa na faida kwa nchi na wananchi.

Tulipaswa kusikia kwa hili la Kiswahili sisi tukiongoza kila fursa inapotokea popote duniani kwani kuna ushahidi usiotiliwa shaka kuwa lugha hii maridhawa nyumbani kwao ni Tanzania. Ni aibu leo Wakenya kutupiku. Lakini hili halitakoma hadi tutakapoacha kujadili mambo mepesi mapesi.