Hivi karibuni Serikali yetu imeridhia kuiuzia Kenya tani 50,000 za mahindi. Mahitaji ya Kenya yalikuwa kupata tani 200,000.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, aliiwakilisha Tanzania kwenye makubaliano hayo ambayo Kenya ilimtuma Waziri wake wa Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Felix Koskei.
Kenya walifikia hatua hiyo baada ya kuhofu kuwa upungufu wa chakula unasababisha mfumko wa bei nchini mwao, na hivyo kuwapo tishio la kuporomoka kwa uchumi wake.
Tanzania, kama ilivyo ada, haikuwa na hiyana kuwasaidia majirani zetu hawa. Ni utaratibu wa Tanzania na Watanzania kuwa mbele kuwasaidia binadamu wenzao wanaofikwa na matatizo kama haya ya chakula. Jirani mwema huwezi kustarehe ilhali mwenzako akiwa anataabika. Hapa ndipo tunapoona utekelezaji wa kauli ile ya “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja”. Isitoshe, kwa Wakristo amri kuu ni Upendo. Kwao, na hata kwa madhehebu mengine, kuna amri inasema, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako”.
Vitabu vitakatifu, na pia waasisi wetu waliyatumia sana maneno haya na kututaka tuyatekeleze bila kujali aina ya jirani tuliye naye. Yapo madai mengi, yakiwamo ya kwamba ndugu zetu kadhaa Wakenya roho zao si za kiutu. Madereva wa malori wanaoingia Kenya, au wanaopita nchini humo wakiwa njiani kuelekea Uganda, Somalia, Sudan na hata Sudan Kusini, wanapata suluba nyingi za kuonewa na Wakenya.
Kudhihirisha hili, juzi tu nilikuwa katika eneo moja la burudani linaloitwa Loliondo. Lipo Kibamba CCM, Dar es Salaam. Tulipigwa na butwaa kumuona raia mmoja wa Kenya, aliyekosa uungwana, akimporomoshea matusi ya nguoni mhudumu wa kike. Hatukuvumilia. Tulimsema na kumtaka ajitahidi kuishi kwa staha kama walivyo wenyeji wake — Watanzania. Hiyo ndiyo sifa yetu hata kama wapo wanaojitahidi kuivuruga.
Wiki iliyopita nilikuwa mkoani Arusha. Nilisafiri hadi mpakani Namanga. Namanga niliyoijua miaka ile, si ya leo. Ni mahali panapovutia kweli kweli. Kuna majengo ya kisasa yaliyojengwa vizuri mno. Kwa hakika Namanga inavutia kuanzia barabara inayotoka jijini Arusha (kilometa 104), hadi kwenye majengo ya kibiashara. Pengine haya ni miongoni mwa matunda ya ushirikiano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pamoja na sababu nzuri za Serikali yetu kuwasaidia Wakenya kwa kuwauzia mahindi, nadhani kuna sehemu tunajidanganya, na hii bila shaka inasababishwa na udhaifu wetu wa kiintelejensia katika biashara.
Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuilisha na kuinufaisha Kenya kibiashara. Tofauti na huko nyuma, safari hii kilichofanywa na Kenya ni ustaarabu tu. Wamefunga safari na kuja kuomba kuuziwa mahindi kwa utaratibu rasmi. Ukweli ni kwamba kwa miaka yote Tanzania inailisha Kenya, iwe kwa njia za wazi au kwa njia za kificho.
Watanzania tukiri kuwa bado tuna udhaifu mkubwa kibiashara, na hii bila shaka yoyote inasababishwa na Serikali yetu. Inasababishwa na Serikali kwa sababu kadhaa.
Mosi, imekuwa haieleweki linapokuja suala la mkulima kuachwa afaidi jasho lake kwa faida nzuri. Tumeshuhudia mara kadhaa wakulima, ama wakizuiwa, au wakiwekewa mikingamo mingi wanapotaka kuuza mazao yao katika soko wanalotaka.
Mwaka 2000 wakati wa Uchaguzi Mkuu, mgombea urais kupitia United Democratic Party (UDP), John Cheyo, moja ya ajenda zake kuu ilikuwa kwamba akiingia madarakani angehakikisha anafungua mipaka ili wakulima wauze mahindi, kahawa na chochote walichonacho nje ya nchi bila vikwazo ilimradi tu wapate faida na walipe kodi na ushuru wa Serikali.
Hoja yake ikawa kwamba kwa kuwaruhusu kuuza nje chakula chao, wangepata fedha nyingi zaidi, na kwa sababu hiyo wangeongeza kilimo kwa kuwa wangeona tija yake. Kwake, hiyo ilikuwa njia sahihi ya watu “kujazwa mapesa.”
Serikali yetu ‘sikivu’ iliendelea kuziba masikio, lakini baadaye ikalegeza msimamo. Hoja dhaifu za Serikali zilikuwa kwamba kuuza mazao nje ya nchi ni kukaribisha baa la njaa nchini. Hii ni hoja dhaifu. Kwanini mkulima awe mtu wa kupangiwa namna ya kufaidi jasho lake?
Kuna amri nyingine za wakuu wa wilaya za kupiga marufuku uuzaji mahindi mabichi au utengenezaji pombe kutokana na nafaka kama mahindi, ulezi au mtama. Kwanini mkulima awekewe vizingiti katika matumizi ya mali yake anayoivuna kihalali? Kwanini mkulima akatazwe asiuze mahindi mabichi kama kwake yana faida nono kuliko mahindi makavu?
Kwanini mkulima azuiwe kutengeneza pombe kwa kutumia nafaka ilhali akiona bei ya bia na konyagi ikizidi kupaa kila uchao? Je, mkulima hana haki ya kuburudika baada ya kazi ngumu za kushika ngwamba? Kwanini acheze ngoma wakati wa msimu wa mavuno bila kinywaji?
Hili la Kenya nasema ni udhaifu wa Serikali kwa sababu si kweli kwamba mahindi yanayonunuliwa na Kenya yanauzwa nchini humo. Si kweli. Kama ni kweli, basi mahindi hayo yanapelekwa kuziba pengo la mahindi ya Kenya yanayopelekwa kuuzwa katika mataifa ya Somalia, Sudan Kusini na Sudan.
Tumekuwa kama tumelogwa. Waziri Chiza anashangilia mkataba dhaifu wa kuuza mahindi badala ya kuhakikisha kinachopelekwa Kenya ni unga wa mahindi! Tangu mwaka jana tulipaswa kutambua kiintelejensia kuwa Kenya itafikwa na baa la njaa.
Tungekuwa na taarifa nzuri za kiuchumi yale mahindi tani 50,000 yangesindikwa na kuwa unga hapa hapa Tanzania. Kenya tungewauzia unga, na kwa sababu hiyo, wakulima wetu wangepata na Serikali yetu ingepata. Tunashindwa nini kutoa fedha na kuwawezesha Watanzania ili wawe na viwanda vikubwa na vya kisasa kwa ajili ya kusindika unga wa mahindi na kuuza kwa majirani zetu?
Wanachofanya Kenya ni hadaa. Wanachukua mahindi nchini mwetu. Wanapeleka kuyasindika katika viwanda vyao na kwenda kuuza unga nchi jirani. Wanaoijua Kenya wanasema haitatokea iwe na chakula cha kutosha, wala Sudan Kusini, Sudan na Somalia hazitakuwa na chakula cha kuwatosheleza.
Ghala lao lipo Tanzania. Wanajua Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba nzuri. Wanajua hali ya hewa ya Tanzania ni njema. Wanajua hawawezi kuhangaika kulima wakati wanaweza kuingia Tanzania wakajitwalia mahindi kadiri wanavyotaka kwa bei ya kutupa na kwenda kupata faida nono huko ughaibuni.
Wanajua vizuizi vinavyowekwa na Serikali ya Tanzania katika maeneo kama Longido ni danganya toto tu. Rushwa kidogo, shehena inaachwa. Inapitishwa. Kenya hawana kigugumizi cha kupokea mzigo wowote ilimradi uwe na tija kwao. Hiyo ndiyo sera yao ya kiuchumi.
Kwa sasa kila siku kuna makumi kama siyo mamia ya malori yanasafirisha nafaka kutoka Tanzania kwenda Kenya. Kuna madai kwamba Kenya ni mapito tu, lakini ukweli ni kwamba nafaka hiyo inapelekwa mbali zaidi kuuzwa. Wanajua faida wanayopata ni kubwa na kwa hiyo kuwaamsha Watanzania ni wao kupoteza neema.
Wanajua Watanzania hawajui kinachoendelea. Kwa mfano, hizi sausage zenye maneno “The Product of Kenya”, nyama yake inatokana na ng’ombe wanaonunuliwa Longido, Monduli, Tarime na kwingineko nchini Tanzania. Wanachofanya ni kuja kuwanunua ng’ombe hapa nchini, wanawapeleka kuwanenepesha kidogo ili nyama iwe laini, kisha tunarejeshewa sausage.
Tunasifu sausage bila kutambua kuwa nyama imetoka Tanzania. Yale yale ya ndugu zetu wa Morogoro ya kuuza muhogo na kisha kununua unga wa muhogo kutoka dukani kwa sababu ni mzuri unanukia kisoko-soko! Tunanunua sausage kwa bei mbaya kwa sababu yule ng’ombe au ile nyama inakuwa imeongezwa thamani.
Wanafanya hivyo kwenye maziwa. Wakenya walitumia hila kwa kushirikiana na Watanzania. Wakanunua Kiwanda chetu cha Maziwa pale Arusha kwa kivuli cha uwekezaji. Wakaahidi kukiwekea mashine za kisasa. Walichofanya baada ya kukipata, tena kwa baraka za Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, ni kuhakikisha kinabaki kuwa kituo cha kupokea maziwa kutoka kwa wafugaji wa Tanzania.
Wakapiga akili. Wakaenda katika wizara zetu chovu. Wakapewa kibali cha kusafirisha maziwa kutoka Tanzania kwenda Kenya bila kuyalipia ushuru kwa sababu ni malighafi. Walipoyasindika, wakayarejesha kama mali iliyokwishaongezwa thamani. Hawakulipa chochote. Kile kiwanda chetu cha Arusha sasa si kiwanda. Ni ghala linalotumiwa kuhifadhia maziwa yaliyokwishasindikwa kutoka Kenya! Uhaini huu wa kiuchumi ulisimamiwa vilivyo na watu wakubwa kabisa katika nchi hii.
Matokeo yake viwanda vya Wakenya vinamwaga maziwa nchini mwetu na kuua au kupunguza nguvu za viwanda vyetu kama Tanga Fresh, Musoma Dairy, Mara Dairy, Asas na kadhalika. Ukichukua maziwa (ya Tanzania yaliyosindikiwa Kenya), ukajumlisha na haya yanayotoka Zimbabwe na Ulaya, wafugaji na wakulima wetu wamebaki malofa.
Wao Kenya hawaruhusu maziwa yetu kuingizwa kwao, wala bia yetu murua ya Safari kuonekana katika baa na ma-supermarket yao. Nayasema haya si kwa sababu nawachukia majirani zetu hawa, la hasha! Ninachotaka kina Mheshimiwa Chiza na mawaziri wengine wakifanye, ni kuwa na uwezo wa kiintelejensia wa kupenya katika masoko ya hawa wenzetu. Tujue kitu gani wanakiuza Sudan Kusini, Sudan na Somalia. Hicho wanachokiuza, kinatoka wapi?
Wakati wakijiandaa pengine kuyafanya hayo, yapo mambo kadhaa ambayo hatuhitaji muda kuyashughulikia. Moja ya hayo ni hili la mahindi. Tukomeshe utaratibu wa kuuza mahindi makavu. Tuuze unga uliokwishasindikwa. Kama kweli wana baa la njaa, watanunua unga.
Kufanya hivyo kuna faida nyingi, lakini moja kubwa ni kwamba tutakuwa tumehamasisha kilimo; na tutakuwa tumepanua ajira miongoni mwa vijana wengi ambao kwa sasa wanataabika. Lakini lililo kubwa zaidi ni kuwa tutakuwa tume-add value, na kwa sababu hiyo Serikali itapata; na wakulima watapata zaidi.
Tufanye hivyo kwenye sekta za maziwa, kahawa, nyama, katani na kwingineko. Mfano mmoja tu wa mahindi haya, si kweli kuwa yanapelekwa kusagwa unga pekee. Yapo yatakayokobolewa. Zile pumba tu ni pesa za uhakika.
Tufanye hivyo kwenye pamba — tusafirishe na kuuza nguo. Tufanye hivyo kwenye mbao — tusafirishe samani. Tufanye hivyo kwenye madini yetu na kwenye kila kile tunachodhani tunaweza kukipeleka kwenye soko la kimataifa kikiwa kimeshaongezwa thamani.
Serikali ina wajibu wa awali na halali wa kuhakikisha inawahamasisha wananchi kutambua fursa zilizopo pamoja na faida za kuuza bidhaa zilizokwishasindikwa badala ya kuuza malighafi.
Asasi za kiraia, badala ya kuhangaika na mambo mengi kila siku ya haki za nini, sijui Katiba na mambo ya aina hiyo, zijikite kuwapa elimu wananchi wetu, hasa wakulima ili wawe na jeuri ya kujua nini kinachoendelea kwenye ulimwengu wa kibiashara ili na wao waweze kuwa na jeuri ya kushiriki wakiwa wanajiamini.

Mwaka kesho Wakenya wakirejea kuomba wauziwe chakula, tuwasikilize, lakini tuwaambie, “Safari hii mtauziwa unga uliokwishasindikwa”.