Kuna ‘kosa’ nimelitenda hivi karibuni. Kosa lenyewe ni la kuwakwida vijana wawili walioamua-bila soni- kujisaidia hadharani katika barabara tunayoitumia mtaani kwetu.

Wale vijana sura zao zilikuwa ngeni kwangu. Nilipowakaribia, nilishuka katika gari na kuwauliza kwanini wameamua kujisaidia hadharani. Jibu lao likawa: “Samahani mzee”.

Wakati wakijiandaa kufunga suruali zao, nikajikuta tayari nimeshawadaka. Kama wangeamua kujibanza kichakani (kumbuka walikuwa mbele ya kichaka), sidhani kama ningesikitishwa na kitendo chao.

Nilijaribu kujiuliza kwanini wafanye kitendo kile hadharani. Je, ni matokeo ya bangi? Ni jeuri tu? Ni ulimbukeni? Je, ni kwa kuwa hawana mtu wa soni wanayemjua eneo letu? Kwanini waamue kujisaidia wakiwa wamelekeza utupu wao kwa wapita njia?

Shida tunazopata mara nyingi kwa watu wa aina hii ni pale tunapokuwa na watoto, mama, dada, kaka au watu wengine wa karibu. Unakuwa wakati mgumu mno unapoendesha gari ukiwa na watu wa karibu kama hao niliowataja, halafu ukasikia tusi la nguoni likifurushwa. Hii imechangia wenye magari wajikute wakifunga vioo hata kama wanajua kwa kutumia viyoyozi wanaingia gharama. Kwenye matusi kuna afadhali. Shida ipo unapoendesha gari au kumpita mtu anayejisaidia akiwa ameelekea usawa unaomfanya aonekane mwenu kirahisi. Hapo ndipo wengi wetu tumejikuta tukijitahidi kuangalia kando au kubadili mazungumzo alimradi tu kukwepa kadhia hiyo.

Nimekumbuka kisa hiki baada ya kumsikia Rais John Magufuli, akishangazwa na hatua ya baadhi ya wananchi kuvigeuza vituo vya Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi kuwa sehemu zao za malazi na za kujisaidia!

Rais akashangaa kuona hali hiyo ya aibu ikitokea, lakini viongozi wa maeneo husika wakiwa kimya au wakiwa hawachukui hatua za kuikomesha.

Jambo hili linaweza kuonekana dogo, lakini kwa hakika ni tatizo kubwa linalozidi kuota mizizi kila leo. Tatizo hili tumeliunda sisi wenyewe katika miji yetu mingi.

Moshi wamejitahidi kuidhibiti hali hii, na kwa kweli wamefanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu. Sijui ni nani aliyesema mtu akifika Dar es Salaam au katika mji wowote mkubwa, ili aonekane wa mjini, basi afanye matukio ya aibu kama haya ya kujisaidia ovyo katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Nasema tatizo hili la ustaarabu ni kubwa kwa sababu inawezekana kabisa haya ni matokeo ya namna tunavyolelewa katika familia zetu.

Mtoto aliyekulia katika nyumba yenye utaratibu wa kutoruhusu utupaji taka ovyo, hawezi kunywa maji mtaani halafu akarusha chupa barabarani au sehemu isiyostahili.

Mara kadhaa tumeona abiria wakinywa na wakishamaliza wanarusha chupa barabarani. Anayefanya hivyo akiulizwa, majibu yamekuwa kama haya: “Hao wanaolipwa kwa kufagia watafanya nini?” “Hizo chupa kuna watu ndio ajira yao, wataziokota”.

Haya ni majibu ya kipuuzi kwa sababu kama ni kuchafua tu kwa sababu kuna mtu anayepaswa kusafisha, nani miongoni mwetu anaweza kuingia sebuleni akajisaidia eti tu kwa kuwa yupo yaya anayelipwa kwa kufanya kazi za usafi?

Kila kitu kina mpangilio wake. Ndio maana kuna vyoo kwa ajili ya shughuli yake mahsusi. Ukiingia nyumbani kwa mtu ukakuta anavua soksi na kuziweka ndani ya jokofu, mara moja utajua ndani ya hiyo nyumba kuna mtindio usio wa kawaida.

Vivyo hivyo, unapoona mtu anakunywa maji halafu anarusha chupa barabarani, ukiamua kumchimba utabaini malezi aliyoyapata yalikuwa na upungufu fulani au ni ulimbukeni tu unaosababishwa na unafsi.

Na hivyo ndivyo wageni wanaozuru nchini mwetu wanavyotupuuza kwa mipangilio yetu ya ovyo. Ukiacha ujenzi wetu usiovutia na ‘mi-kuta’ iliyopamba kando ya barabara na mitaa, bado tumeruhusu wachuuzi wavamie sehemu za waenda kwa miguu. Wale wanaoishi Dar es Salaam sasa wanaona hali ilivyo kule Mbezi Mwisho, Kimara, Ubungo na kwingineko.

Barabara nzuri zimejengwa kwa thamani kubwa. Simewekwa sehemu maalumu kwa waenda kwa miguu. Sasa maeneo hayo mengi yamevamiwa na wachuuzi. Wanauza nyanya, bamia, pumba, mitumba, matunda na kila kinachopata mnunuzi.

Maeneo mazuri yaliyotengwa kwa waenda kwa miguu yamejengwa mabanda mabovu ya miti na vipande vya mbao na kutundikwa sidiria, mitumba ya kila aina, mabegi na bidhaa nyingine.

Eneo la katikati ya Jiji la Dar es Salaam-sehemu zote za waenda kwa miguu zimepangwa viatu. Mama Ntilie kila mahali. Wachoma mihogo na viazi kila kona. Wauza mitumba wanajipanga mistari wakiwashawishi wapitia njia wanunue biadhaa zao walizozishika mikononi. Kwa ufupi kila mahali katikati ya Jiji la Dar es Salaam ni wachuuzi tu!

Ashakhumu si matusi, kwa wenzetu hali kama hii ni uchafu! Huwezi kuyaona haya mambo Kigali. Kwa watu wastaarabu huwezi kuyaona haya.

Juzi, pale Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, nikashangaa. Kuna idadi kubwa mno ya waendesha teksi walioiga tabia za makondakta wa daladala. Mgeni anashuka, anafuatwa na madereva wanne au watano. Mgeni anagombewa. Hakuna tofauti tena ya Uwanja wa Ndege huo na Kituo cha Mabasi Ubungo. Kila mmoja ‘anapiga debe’. Nchi ya watu waungwana huwezi kukutana na kadhia ya aina hii.  

Rais John Magufuli, alipozindua Bunge la 11 alisema maneno haya ya mwelekeo wa aina ya Serikali yake ya Awamu ya Tano.

Alisema: “Kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha shughuli za kina mama lishe, wachuuzi mbalimbali, machinga, waendesha boda boda na maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k.

Shughuli za makundi haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha.

“Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka mipango na taratibu nzuri na rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo utokanao na shughuli nilizozitaja tutauondoa. Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.”

Hapo kwenye wino weusi ndiko nilikokusudia. Miezi saba sasa, viongozi na watendaji wa Serikali na hasa Halmashauri nchini, wanasubiri nini kutenga maeneo ili wachuuzi hawa wapishe maeneo waliyovamia?

Endapo mamlaka zitachelewa kutekeleza maagizo haya ya Rais, hili jambo litaibua chuki na manung’uniko kama yale ya wakati wa kuwaondoa wananchi wanaoishi mabondeni.

Hawa wachuuzi waliovamia maeneo ya waenda kwa miguu, hawa wanaouza mitumba mitaani na katika mitaa yote, siku wakitakiwa waondoke, hawataondoka. Nguvu itakapotumika kuwaondoa, tayari hilo litakuwa donda jingine kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa vile watakuwa wamekaa maeneo hayo muda mrefu na hivyo kujiona wana haki zote, kitendo cha Serikali au mamlaka za miji kuwaondoa watakiona kuwa ni cha uonevu, na kwa kweli hawatakubali kwa urahisi.

Haya yalianza hivi hivi pale “Mahakama ya Ndizi”. Siku Serikali ipothubutu kuwaondoa, ‘ilishindwa’.

Jiji la Dar es Salaam limepoteza mvuto wake kutokana na uzembe huu wa kuruhusu kila kitu kutendwa katika mazingira au aneo lisilo lake. Ndugu Rais ajue kero si kwa wale wanaojisaidia kwenye vituo au mitaani tu, bali hata hawa wachuuzi walioachwa waenee kila mahali ni kero pia. Kwa kasi yao, sioni nani atawazuia kuutumia ukuta wa Ikulu kutundika mitumba yao. Ustaarabu ni somo lililotushinda Watanzania wengi. Tunahitaji mjadala wa pamoja kurekebisha hali hii.