Hapa Tanzania ukitamka neno ‘utalii’, haraka haraka akili za watu hukimbilia kwenye mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro labda na fukwe za Zanzibar: Basi! Hata serikali inaelekea kufikiria hivyo, ndiyo maana mkazo kuhusu utalii uko kwenye aina hiyo tu ya utalii. Namna hii finyu ya kuuangalia utalii ndiyo inayosababisha tuwe na watalii wachache licha ya kuwa na vivutio vingi nadra na vyenye hadhi ya tuzo bora duniani.
Kwa mtazamo wetu finyu namna hii haitushangazi kwa nini mnara mmoja tu huko Ufaransa (Eiffel Tower) hutembelewa na watalii milioni 7 kwa mwaka wakati Tanzania na ujumla wa mamia ya vivutio vyake ipokee watalii milioni 1 na ushei tu kwa mwaka! Au kwa nini watalii milioni 11 watembelee mapiramidi ya Misri mwaka jana ilhali Tanzania yenye Serengeti, Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na Zanzibar ipokee wageni milioni moja pekee.
Nyakati zinabadilika na utalii ni zaidi ya vivutio vya macho!
Nimesoma, pamoja na mapendekezo mengine, mabadiliko ya sheria ya filamu na maigizo kwenye muswada uliopelekwa kwa hati ya dharura na kubaki kinywa wazi.
Kwanza, kwa nini muswada wa sheria nane zilizosheheni mambo makubwa yanayohitaji uamuzi wenye hadhari kubwa unapelekwa bungeni kwa hati ya dharura? Ni suala linalobaki kuwa siri ya waliouandika.
Pamoja na nia njema, baadhi ya vipengele vinatuumiza wenyewe. Sheria hii ikisainiwa na rais kama ilivyo inakwenda kuondoa kabisa uwezekano wa mtu au kampuni yoyote ya nje kurekodi filamu hapa nchini.
Utalii wa filamu ni sekta mpya inayoinukia duniani kote na kwa kutambua hilo nchi jirani zimetunga sheria rafiki ili kuvutia kampuni za nje kuja kutengeneza filamu kwenye nchi zao. Wakati kampuni kubwa za sinema zinaendelea kutafuta mandhari mpya za kuvutia, mtindo wa watazamaji wa sinema kutembelea maeneo zilikotengenezwa sinema walizozipenda unashamiri pia. Imekuwaje basi katika ushindani wa namna hii sisi tunafikiria kufanya mambo yawe magumu kwa mtu yeyote kuja kwetu?
Fikiria kwa mfano (vipengele vyenye utata):
(1) Kwamba, kampuni yoyote ya kigeni itakayotumia ardhi ya Tanzania kutengeneza filamu nzima au kipande, italazimika kukabidhi “Raw Footage” (Picha ghafi moja kwa moja kutoka kwenye kamera kabla haijahaririwa) kwa Bodi ya Filamu Tanzania.
Hili haliwezekani. Masilahi ya sinema pote duniani yanahitaji kulindwa na unyeti wa hali ya juu (hasa kabla ya sinema kuanza kusambazwa).
Kwa filamu zinazotengenezwa kwa kutumia kamera za mikanda (film cameras) ndiyo haiwezekani kabisa maana ili kuona kilichorekodiwa sharti filimu zipelekwe maabara maalumu kwa usafishaji. Tanzania haina ‘film lab’ hata moja, sharti hili litatekelezwaje?
(2) Kwamba, mara baada ya kazi yake ngumu ya kurekodi filamu, mtengenezaji atasaini waraka na kuukabidhi kwa Bodi ya Filamu Tanzania akitoa idhini kwa Serikali ya Tanzania kuitumia filamu yake ipendavyo kwa ajili ya kutangaza vivutio vyake. National Geographic wakisikia sharti hili watacheka tu!
(3) Kwamba Bodi ya Filamu Tanzania ndiyo itakayopanga na kuamua idadi ya wataalamu na waigizaji wa kigeni watakaoruhusiwa kuingia nchini. Sijui mantiki ya kipengele hiki, idadi ya wataalamu au waigizaji huamuliwa na watengenezaji kulingana na mahitaji ya filamu, kwa vipi Bodi itaamua nani aje na nani asije?
Vipengele hivi vinaletwa wakati tayari Tanzania inalalamikiwa kuwa na masharti magumu kuliko wenzetu wa Afrika Mashariki. Mfano, wakati tozo ya kupiga picha nchini Rwanda ni dola 30 za Marekani na Sh 15,000 nchini Kenya; Tanzania inatoza (bila kujali kama ni mtu binafsi au Warner Bros) dola 1,000 za Marekani ndani ya mwezi mmoja na dola 3,000 za Marekani kwa wale wanaohitaji kibali ndani ya siku 7!
Nimekutana na watu wa nje waliolalamikia kutuma maombi kwa mujibu wa fomu ya kuomba kibali na bado hawakupata majibu yoyote. Taratibu za wageni kuingia na vifaa vya kupigia picha pia ni ngumu kuliko nchi jirani.
Haishangazi basi, kwamba kila wakati, sehemu fulani katika mbuga ya Kenya kuna kampuni kubwa au ndogo inatengeneza sinema huku sisi tukiridhika na tuzo inayoitambua Serengeti kama mbuga bora kuliko zote Afrika!
Kulikuwa na kampeni mitandaoni ikikusanya sahihi ili kuwashinikiza wabunge kutopitisha mapendekezo ya muswada wa sheria nane pasipo majadiliano na tafakuri ya kutosha. Wahamasishaji walitahadharisha kuwa muswada huo, pamoja na kuathiri utalii wa filamu, utaziathiri azaki zote hata zile za kidini na hata uanzishaji wa kampuni ya kibiashara.
Yeyote anayeguswa na mustakabali wa nchi yetu anakaribishwa kuusoma na hata kuweka sahihi katika kampeni hii:http://www.changetanzania.org/petitions/ombi-kwa-bunge-na-serikali-kuongeza-muda-kwa-mchakato-wa-muswada-wa-mabadiliko-ya-sheria-mbali-mbali-8-zilizopo-bunge-kwa-hati-ya-dharura?fbclid=IwAR2fL3A-KHX6aO4oEHcuBdfqGDuY19mzhIxmmXhYnBwX3fmkMyPhMgzaxqI
Je, wajua kwamba sinema hizi zilirekodiwa nchini Kenya?
1. Gun Runners
2. Nowhere in Africa
3. The Constant Gardener
4. Cry Freedom
5. The First Grader
6. Tom Raider
7. Sense 8
8. Born to be Wild
9. The rise and fall of Idi Amin
10. The Ghost and the Darkness
11. Inception
Kwanini sisi Watanzania tujiwekee vizingiti kwenye tasnia hii ambayo ikitumiwa vema na kwa msharti yanayohimilika inaweza kuitangaza vema nchi yetu ulimwenguni kote?