Wiki iliyopita Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na wahariri na waandishi walikutana mjini Mtwara. Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Emmanuel Humba, na maafisa waandamizi wa mfuko huu wameeleza vyema mafanikio chini ya mfuko huu.

Nafahamu kuwa kwa wiki nzima magazeti yameandika vilivyo juu ya suala hili. Yamegusia pia nia ya baadhi ya wana-Mtwara waliopanga kuwateka wahariri na waandishi tukaamshwa na polisi vyumbani saa 9 usiku kuwahishwa nje ya miji ya Mtwara na Lindi.


Sitanii, wakazi wa Mtwara waliahirisha maandamano yao baada ya kuambiwa tumeondoka alfajiri. Ninaloweza kusema kuna tatizo kubwa Mtwara. Mkuu wa Wilaya ya Mtwara naye anahitaji semina elekezi. Wananchi niliozungumza nao hawajafafanuliwa vyema gesi inavyochimbwa, faida ya kuipeleka Dar es Salaam na kuwaandaa kwa ajili ya kupokea maendeleo yatokanayo na gesi.


Wananchi wanapaswa kuandaliwa kwa uwekezaji. Kuwajulisha kuwa maandamano hayatawasaidia. Kuwa hata kama gesi yote itabaki Mtwara halitafunguliwa dirisha la kuwalipa mishahara wana-Mtwara bila kufanya kazi. Serikali iwaandae wananchi kukopesheka kwa kuwapimia viwanja vyao, kuwafundisha ujasiriamali na ukarimu jinsi ya kupekea wageni kibiashara. Ikiwa haya hayajafanyika, hata kama viwanda vyote vitajengwa Mtwara ni bure.


Narejea Bima ya Afya. Nasema Watanzania tusifanye mchezo. Hakuna mwenye kinga dhidi ya magonjwa milele. Serikali imeanzisha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF). Wananchi wanachangia kati ya Sh 5,000 na 10,000 kulingana na uwezo wa wilaya husika.


CHF imefanya kazi nzuri Igunga na Iramba. Bima ya Afya inakupa uhakika wa kutibiwa muda wowote na saa yoyote unapopatwa na ugonjwa. Inawezekana huu ni utamaduni mpya kwa Watanzania, lakini kwa yeyote anayefahamu faida ya uhakika wa matibabu, hawezi kuupuuza. Nashauri kila wilaya, kila kaya kuhakikisha inajiunga katika moja ya mifuko hii.


Hata hivyo, utafiti uliofanywa na wanahabari umebaini mambo kadhaa. Kwamba baadhi ya wenye bima wamepata kero kubwa wakifika hospitali. Wanaambiwa dawa hazipo au wahudumu wanawahudumia kama vile wanawasaidia bure, hawawajali.


Sitanii, watumishi wa afya na madaktari badilikeni. Dunia ya sasa inaondokana na utaratibu wa kutembea na maburungutu ya pesa. Hata Hospitali ya Taifa Muhimbili imefikia uamuzi wa kuitumia Benki ya Makabwela (NMB) kupokea malipo ya matibabu.


Kwa nchi zilizoendelea malipo hufanywa kwa kadi. Ukifika ama unajaza fomu kama wanavyofanya kwa ajili ya Bima hapa kwetu, au unaweka kadi yako ya benki kwenye mashine maalum fedha zinakatwa. Tusirudi nyuma, Watanzania tujiunge na bima.


Baada gesi Mtwara na Bima ya Afya, nizungumzie elimu hata kama ni kwa ufupi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, asilimia 60 ya wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 wamepata daraja sifuri. Asilimia 33 wamepata daraja la nne na asilimia saba tu, ndiyo wakagawana daraja la kwanza hadi la tatu.


Zipo shule zilizopata daraja sifuri wanafunzi wote. Hata shule zilizozoeleka kupanga misonge (A), zamu hii zimeambulia makarai (C). Hili si suala la kuchekea. Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameunda Tume inayoongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Paniel Lyimo.


Sitanii, hili ni janga la kitaifa. Serikali ilipaswa kutoa amri ya kushusha bendera nusu mlingoti kwa siku zaba kuomboleza elimu nchini. Napendekeza suluhisho la matatizo haya kwanza ianzishwe Mamlaka ya Kudhibiti ada Shuleni.


Haiwezekani baadhi ya shule zikatoza hadi milioni 10 sekondari na msingi, ilhali za Serikali zinatoza 20,000. Hapa kutakuwa na tofauti kubwa ya mishahara na walimu wataishia kwenye tuisheni na kuuza vitumbua ili waishi maisha sawa na wenzao wa shule binafsi.


La pili tuisheni zipigwe marufuku na walimu walipwe sitahiki zao. Hatua yoyote ya kuwapuuza walimu, majibu tutayapata kwa walimu kuwapuuza wanafunzi. Tutaishia kujenga Taifa la mazezeta, ambapo kina James Mbatia na Edward Lowassa watakesha wakiimba wimbo wa elimu, ila hatutaona mabadiliko.


Sitanii, elimu ni gharama, lakini si ghali kwa kiwango cha kutufanya tuchague mkondo wa kujaribu ujinga kama taifa. Tuamke kutoka usingizini.