Kwa muda sasa nimekuwa nikifuatilia mwenendo wa elimu nchini. Nafuatilia kilio na matangazo yanayotolewa kila pahala, yakielezea wanafunzi zaidi ya 5,000 wanaomaliza elimu ya msingi na kufaulu mtihani wa darasa la saba huku hawajui kusoma na kuandika. Si hilo tu lakini nafuatilia pia kaulimbiu kuwa ‘Ualimu ni wito’.

Nadhani nchi yetu imejaribu kufanya utafiti na kupima kama wahenga walikuwa na akili timamu waliposema kama unadhani elimu ni ghali jaribu ujinga. Tumeamua kufanya utafiti huu kwa kujaribu ujinga. Tumekiuka misingi ya utoaji elimu, uwezeshaji walimu na utamaduni wa kuwatia moyo walimu wetu kwa nia ya kuhakikisha kizazi hiki na kijacho kinarithi taifa salama.

Nasema hivyo kwa sababu mbali na mimi kuifanya kazi hii ya ualimu kabla ya kuhamia kwenye uandishi wa habari, nimelelewa katika familia iliyokuwa na historia ya ualimu. Baba yangu mzazi, Alphonce Mutalemwa Balile, aliajiriwa kama mwalimu mwaka 1952. Ameifanya kazi hii hadi mwaka 1987 alipostaafu kwa mujibu wa sheria.

Sitanii, mwaka 1963, Mwalimu Alphonce Balile alikuwa Mtanzania wa kwanza katika Kata ya Nyanga, Wilaya ya Bukoba Mjini kujenga nyumba ya bati na iliyosakafiwa kwa saruji. Wananchi walikuwa wakitoka sehemu mbalimbali kuja nyumbani kwetu kuomba ushauri kwa Mwalimu Balile. Ingawa hakuwa hakimu au wakili, kwa muda wote nilioishi naye nilishuhudia akisuluhisha migogoro kadhaa iliyoshindikana mahakamani.

Migogoro ya mashamba, ardhi, maadili na familia – mingi ilikuwa ikiletwa kwa Mwalimu Balile – kwa imani waliyokuwa nayo kwa Mwalimu, si kwa sababu ni Balile, kila uamuzi alioufikia ulihitimisha mgogoro. Hapa yapo mengi yaliyokuwa yanampa heshima Mwalimu Balile. Kwanza, alikuwa amefundishwa na mkoloni, hivyo aliweza si tu kuzungumza Kiingereza fasaha, bali alikuwa na maarifa ya ziada.

Pili, Mwalimu Balile alikuwa amepata fursa ya kusafiri mikoa mbalimbali ya nchi hii kutokana na kazi yake, kwani alipata fursa ya kufundisha Ifunda, Butimba na Rubondo kule Kigoma, Dar es Salaam, Biharamulo, Sengerema na kwingineko. Huko kote alikuwa akihamishwa vituo vya kazi na mwajiri wake aliyekuwa akiwajali walimu.

Kubwa zaidi, Mwalimu Balile alikuwa havai makubadhi, shati lenye rangi zaidi ya moja, wala suti isiyo na kizibao ndani. Kila apofika aliheshimika. Mwalimu Balile alikuwa anakunywa bia ya Kizungu, lakini pia alikuwa anakunywa pombe kali kama suna tu, kwani mwalimu wa enzi hizo ndiye pekee aliyekuwa anaweza kunywa bia, tena bia za wakati huo katika chupa iliyokuwa ikiitwa ‘gandarefu’.

Sitanii, Mwalimu Balile hakuwahi kufanya biashara ya bodaboda, hakupata kuuza ukwaju wala vitumbua, hakuwahi kufika shuleni kufundisha akiwa na fuko la pipi, kisha akawaita wanafunzi wake wateja wa bidhaa auzazo.

Mshahara wa Mwalimu Balile ulifahamika kuwa unatoka tarehe 25 ya kila mwezi. Likizo yake hata kama aliisahau alikumbushwa na mwajiri kuwa mwzi fulani ni mwezi wa kwenda likizo. Sasa yeye, mke wake Angelina na watoto wake wanane wakati huo, wote walilipiwa nauli na kusafirishwa kwenda likizo Bukoba kama walikuwa katika kituo nje ya Bukoba.

Mwalimu Balile alikuwa haruhusiwi kuuza likizo kwa mwajiri na sikupata kumsikia akilalamika kupunjwa malipo yake. Mshahara ulimtosha Mwalimu Balile kununua baiskeli (kama usafiri wa kisasa wakati huo) na kwa kuwa hakuwa na manung’uniko, kila alipoingia darasani kufundisha alikuwa na maandalizi ya somo (wenyewe wakiita lesson plan), alifuata mtaala na alifundisha wanafunzi bila kuchoka kisha alihitimisha kazi ya siku kwa kibonzo na wanafunzi wakaishia kucheka. Je, Mwalimu Balile alikuwa na fimbo mkononi? Sitanii, swali hili utalijibu wewe msomaji.

Leo namzungumzia Mwalimu Kalumekenge. Huyu anaishi kwenye nyumba ya kupanga, ilhali akina Mwalimu Balile walikuwa na nyumba za walimu zenye nyumba ndogo ya mtumishi ikimilikiwa na Serikali.

Kinyume na hivyo, Mwalimu Kalumekenge anapanga kwa Mdengereko anayeuza nazi Kariakoo na kupata fedha yake kwa wakati. Hata hivyo, Mwalimu Kalumekenge hakuwa mpangaji pekee kwa Mdengereko. Wapo vijana wauza maji, ukwaju na sidiria na kupata fedha za kutosha kwa wakati.

Ukifika mwisho wa mwezi hawa wapangaji wengine wanambembeleza Mdengereko wamlipe hata kodi ya mwaka kuepusha kusumbuliwa kila mwezi (fedha wanazo), ila Mwalimu Kalumekenge anaomba aongezewe siku saba aweze kufuatilia mshahara wake wilayani. Heshima ya wamachinga waliopanga nyumba moja na Mwalimu Kalumekenge ni kubwa mbele ya Mdengereko kwani wanalipa kodi kwa wakati.

Sitanii, ni katika mazingira hayo, Mwalimu Kalumekenge anapata vishawishi vya kuuza pipi, nyanya, vitumbua na maandazi ili aweze kusukuma maisha kushindana na machinga. Mwajiri amemsahau Mwalimu Kalumekenge, anampima mwalimu kwa wingi wa kura atakazopata wakati wa uchaguzi. Tena anadiriki kusema sizitaki kura za walimu. Mwalimu anadai haki, bosi anaihusisha haki na uchaguzi.

Tumekwenda mbali zaidi tunaiambia dunia kuwa kazi ya kufundisha imetushinda. Mitihani yote kwa sasa ni ya kuchagua. Mpaka hesabu ni za kuchagua. Hata Jiografia, badala ya kuchora ramani, watoto wetu wanachagua ramani zilizokwishachorwa. Nasikia na mwaka huu tumeendelea zaidi. Tunatoka katika usahihishaji wa hata hayo majibu ya kuchagua kwa kutumia walimu, sasa yatakuwa yanasahihishwa na mashine kama takwimu za sensa.

Nilipata kumuuliza Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa anashangaa nini watoto 5,000 kufaulu mtihani huku hawajui kusoma na kuandika, ilhali mitihani ni ya kuchagua na wapo watu wenye bahati wanashinda hadi magari kwenye michezo ya kubahatisha, hivyo wanaweza kubahatisha tu hata majibu. Pinda alisema yeye haamini kama hilo ni sahihi.

Katika hili napaswa kuwa mkweli. Tumedharau walimu na kuwaona kama matarishi wetu badala ya kuwa wawezeshaji wa uelewa katika taifa letu. Tumechagua kujenga kizazi cha wajinga. Serikali yetu sikivu imeamua kuwasiliza wafadhili wakiimbia kuwa teknolojia inasaidia kupunguza ugumu wa kazi ya kusahihisha, wakati kwao wanatumia walimu kusahihisha mitihani ya watoto wao.

Mbali na kwamba wanafunzi wanaweza kubahatisha, mwalimu anaposahihisha mtihani au jaribio alilofanya mwanafunzi, anapata fursa ya kubaini upungufu wa mwanafunzi na kumrekebisha. Leo tunatumia mashine. Walimu wanauza ukwaju wagange njaa na hawana muda wa kutoa mazoezi na kusahihisha.

Sitanii, ndugu zangu Watanzania yapo mambo tunapaswa kuyafanyia kazi. Tusipofunga breki hapa tulipofikia tutapotea njia. Kama tunaipenda nchi yetu wakati sasa umefika. Tuandamane. Tupinge mfumo wa kudharau walimu. Walimu wakiamua kulipeleka ‘chaka’ taifa letu tutapotea njia usipime. Na kimsingi tumekwishapotea kinachohitajika sasa ni mjadala wa kitaifa.

Tunahitaji mjadala usiotiliwa shaka. Mjadala utakaotuwezesha kufikia mwafaka. Tusema hapana mitihani ya kuchagua. Tusema hapana mitihani ya kusahihishwa kwa kutumia kompyuta. Tuseme hapa kunyanyasa walimu. Tuseme hapana kuchelewesha mishahara na haki za walimu.

Najua tumeelekeza nguvu kubwa katika siasa, lakini kinachotokea tunakishuhudia. Tumeanza kupata kizazi kilichokula bulga bungeni. Kizazi hiki cha facebook kipo kinafanya vituko. Sikupata kufikiri kuwa mbunge akiwa mtu anayeheshimika kwa kiwango kile angeweza hata kufikiri tu, kuchukua bendera ya chama fulani akaivalisha mbwa. Haya ni matunda ya elimu chepechepe.

Kwa vyovyote iwavyo, hatutafanikiwa katika hili bila kufanya uamuzi mgumu. Tunahitaji kiongozi asiyeogopa kushika damu. Tunahitaji Rais asiyemchekea kila anayepita mbele yake. Akicheka imaanishe anacheka kweli, na akinuna kila mtu afahamu hivyo. Hapa tutakuwa na Rais anayetabirika. Si kuendelea na utamaduni mpya tuliouibua.

Vyombo vya dola navyo vinadaiwa kutumbukia kwenye siasa. Badala ya kushughulikia wanaokalia haki za wafanyakazi kama ilivyokuwa zamani, sasa wanahangaika na Mnyika, Lowassa, Mwakyembe, Dk. Slaa, Mbowe na Hamad Rashid. Hadi Dk. Mwakyembe afike bandarini na kubaini kuwa wakubwa wanaiba mafuta awatimue ndipo wanajifanya kushituka. Zamani haikuwa hivyo.

Ingawa tumeondoa unyapara kazini, yatupasa sasa kufikiri upya. Tumezidisha uhuru kwenye vituo vya kazi. Ofisi nyingi za Serikali na sekta binafsi zimegeuka pango la kambale. Mdogo na mkubwa wote wana sharubu. Hata ukienda kwenye baa sasa hivi ni wahudumu wachache wanaowaheshimu mameneja wao. Wanabishana hadharani mbele ya wateja.

Sitanii, hayo tunayoshuhudia baa ndiyo yanayokwenda hadi kwenye ofisi za Serikali. Watendaji hawaheshimu tena utaratibu wa ‘hairakia’ (hierarchy). Mtumishi anachelewa kazini, akifika anamwambia bosi wake kuwa kulikuwa na foleni ya  kutisha huko barabarani. Huu ni utovu wa nidhamu.

Nasema tulipofika sasa yatupasa kufunga breki. Katika hili la elimu nashawishika kumshauri Gratian Mkoba kuwa badala ya kugoma, hebu itisha maandamano ya amani mkiwaomba Watanzania wawasaidie kueleza kilio cha walimu kwa amani hadi viwanja vya Uhuru vilivyopo kila kona ya nchi hii, kisha mueleze ujumbe wenu.

Maandamano haya yanaweza kuwa na tija kuliko mgomo. Weka ratiba ya maandamano mara moja kila baada ya miezi tatu kisha mnarudi kazini. Mara nne kwa mwaka wakubwa watasikia. Onyesha nguvu ya sauti ya umma ambayo ni sauti ya Mungu. Mungu ibariki Tanzania.