Na Immaculate Makilika- MAELEZO

Tume ya Ushindani (FCC) imeendelea kupata mafanikio katika kutekeleza lengo lake kuu la kuongeza ufanisi katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa bidhaa na huduma katika kuhakikisha mazingira sawa ya ushindani wa soko baada ya nchi kuondokana na mfumo wa uchumi hodhi na kuhamia katika mfumo wa uchumi wa soko huria kwa maslahi mapana ya Taifa.

Hayo yameelezwa leo Agosti 2, 2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Bw. William Erio wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

“Katika kipindi cha miaka mitatu yaani mwaka 2020 hadi 2023, FCC iliridhia kununuliwa kwa kampuni 14 zenye jumla ya thamani ya bei ya mauziano inayofikia shilingi bilioni 49.4 katika sekta ya kilimo kwa lengo la kuruhusu kampuni hizo kuongeza wigo zaidi sokoni, kuongeza mitaji na kupunguza uwezekano wa kampuni hizo kuondoka sokoni”, alisema Bw. Erio.

Amezitaja Kampuni hizo kuwa ni pamoja na Mtanga Foods Limited (yenye biashara zake Iringa), kampuni ya uzalishaji wa Parachichi ya Rungwe Avocado Company Limited na kampuni ya uchenjuaji mpunga (mchele) ya MW Rice Millers Limited na Mring’a Estates Limited.

Erio alifafanua “Miungano ya makampuni iliyoidhinishwa na FCC ya AMY Holdings Limited kununua kampuni mbili za Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL) na Tanzania Leaf Tobacco Company Limited (TLTC) zilizokuwa zimefungwa kwa zaidi ya miaka minne ilisababisha mafanikio katika Sekta ndogo ya Tumbaku nchini.

Ambayo ni kupatikana kwa ajira zaidi ya 3,000, kupanda kwa bei ya tumbaku ghafi kwa kilo kutoka shilingi 3,762 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 4,616 mwaka 2022”.

Aidha, mafanikio mengine yanatajwa kuwa ni kuondoshwa kwa zuio la kuzalisha tumbaku ya ziada lililokuwepo kwa wakulima waliokuwa wakizalisha kwa utaratibu wa kilimo cha mkataba na wenye viwanda kutoka hatua iliyoongeza uzalishaji wa tumbaku kutoka tani 65,0000 (2021) hadi kufikia tani 138,000 (2022).

Hali hii inaashiria kufikiwa kwa lengo la kuzalisha tani 200,000 kufikia mwaka (2025) kama ilivyobainishwa na kuelekezwa na Ilani ya Chama Tawala.

Vilevile katika sekta ya mawasiliano, FCC iliidhinisha jumla ya kampuni 26 zilizonunuliwa na wawekezaji mbalimbali katika kipindi cha mwaka 2020 na 2023 kwa thamani ya shilingi bilioni 653.