MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchuguzi (NEC), Ramadhani Kailima

Februari 15, 2018 baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, walifika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwasilisha malalamiko yao kadhaa ambayo walikuwa wanahitaji ufafanuzi kutoka NEC kuhusu uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya kupitia hoja za CHADEMA, inapenda kutoa ufafanuzi wa hoja hizo:

Hoja ya kwanza, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Uchaguzi la Kinondoni amekataa kuwaapisha mawakala wa ziada wa upigaji kura kutoka CHADEMA ambao ni asilimia kumi na tano (%15) ya mawakala wote wanaohitajika kwenye vituo 613, na kuwa utaratibu huu umekuwa unatumiwa katika chaguzi zilizopita.

Ufafanuzi, kwa mujibu wa kifungu cha 57(1)(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kila Chama cha Siasa kilichopata ridhaa ya kuweka wagombea, kinaweza kuteua wakala mmoja wa upigaji kura kwa kila kituo ndani ya jimbo.

Aidha, Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 inakitaka kila Chama cha Siasa kinachoshiriki katika Uchaguzi siyo zaidi ya siku saba (7) kabla ya siku ya Kupiga Kura kiwe kimewasilisha kwa maandishi kwa Msimamizi wa Uchaguzi majina ya Mawakala, anwani zao na vituo walivyowapangia.

Vilevile, kifungu cha 57(3) cha Sheria tajwa, kimeweka utaratibu na mazingira ambayo wa chama kilichosimamisha mgombea kuweka wakala mbadala wa upigaji kura.

Tunashauri CHADEMA kuzingatia matakwa ya kifungu cha 57(3) cha Sheria husika pale patakapohitajika uwepo wa mawakala mbadala.

Hoja ya pili, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi amekataa kuwaruhusu na Viongozi wa CHADEMA kuwa Mawakala wa upigaji kura, kwa maana hiyo atakichagulia chama mawakala wa upigaji kura, na kwamba, orodha ya viongozi hao watambuliwe na kuapishwa kuwa Mawakala wa upigaji kura.

Ufafanuzi, kifungu cha 57(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kikisomwa pamoja na Kanuni ya 48(2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 vimeweka utaratibu wa muda wa kuwasilisha orodha ya mawakala na muda wa kuwaapisha kuelekea siku ya Uchaguzi.

Kwa maana hiyo, siku ya kuwasilisha na kuapishwa mawakala ilikuwa tarehe 10 Februari, 2018. Hivyo, kupokea na kuwaapisha mawakala wengine itakuwa ni kinyume cha masharti yaliyowekwa chini ya kifungu na kanuni niliyoitaja.

Hoja ya tatu, kwamba, Mawakala wa upigaji kura wa CHADEMA hawajapewa nakala za hati zao za kiapo cha kutunza siri.

Ufafanuzi, kwa mujibu wa Kanuni ya 48(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 kila Wakala wa Upigaji kura anapaswa kuapa kiapo cha kutunza siri katika Fomu Na. 6 kabla ya kutekeleza wajibu wake katika kituo cha kupigia kura.

Kwa takwimu zilizopo jumla ya vituo vya kupigia kura ni 613 na jumla ya Vyama vya Siasa 12 vinashiriki katika uchaguzi huo. Kwa kuwa kila Wakala mmoja alijaza nakala mbili ya Kiapo cha kutunza siri, hapo unazungumzia uwepo na viapo 14,712.

Kanuni ya 48(3) ya Kanuni tajwa, Wakala wa Upigaji Kura atapaswa kupewa barua na Msimamizi wa Uchaguzi ya kumtambulisha kwa Msimamizi wa Kituo cha kupigia kura. Hapa unazungumzia nakala 22,068 kwa sababu, nakala moja atapewa wakala, nakala itabaki kwenye jalada kwa kumbukumbu na nakala itapelekwa kwa Msimamizi wa Kituo kwa urahisi wa rejea.

Hata hivyo, taarifa tulizonazo ni kuwa, Msimamizi wa Uchaguzi ameanza kutoa nakala hizo za Viapo kwa Wawakilishi wa Vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi mdogo ili wawapatie Mawakala wa Vyama husika. Utaratibu huu nidyo uliokubaliwa kwenye vikao vya Msimamizi wa Uchaguzi na Wawakilishi wa Vyama.

Hoja ya Nne, kwamba, Msimamzi wa Uchaguzi ametoa maelekezo kuwa Mawakala wawe na utambulisho wa kumtambulisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi mbali ya barua kutoka kwa Msimamizi wa Uchaguzi. Utambulisho huo ni Vitambulisho vya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Hati ya Kusafiria na Kitambulisho cha Kitaifa.

Ufafanuzi, kwa kuzingatia matakwa ya vifungu vya 13(2) na 61(3)(a) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume imeruhusu wapiga kura walioandikishwa kwenye Daftari ya Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2015 na ambao wamepoteza kadi za kupigia kura au zimechakaa au zimeharibika, watumie Kitambulisho cha Taifa, Hati ya Kusafiri na Leseni ya Udereva kupiga kura.

Kwa kuwa Wakala wa upigaji kura aliyeandikishwa ndani ya Jimbo la Kinondoni anayohaki ya kupiga kura, na kwa kuwa inawezekana wakawa wamepoteza kadi za kupigia kura au zimeharibika au kuchakaa. Hivyo, mahitaji ya vitambulisho hivyo ni kuwezesha utekelezaji wa matakwa ya vifungu vilivyonukuliwa.

Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa, siku ya upigaji kura, baadhi ya mawakala wanao kwenda vituoni siyo Mawakala waliokura kiapo cha kutunza Siri katika Fomu Na. 6 na siyo waliotambulishwa na Msimamizi wa Uchaguzi kwa Msimamizi wa Kituo.

Hivyo, tunapenda ieleweke kuwa, endapo itatokea wakala wa upigaji kura aliyepo katika kituo cha kupigia kura siyo aliyeapa kiapo cha kutunza siri na siye aliyetambulishwa na Msimamizi wa Uchaguzi, utakuwa ni ukiukwaji wa Sheria, na atachukuliwa hatua za kisheria mara moja.

Hoja ya Tano, kwamba, Msimamizi wa Uchaguzi hajatoa na kuweka wazi kuhusu kituo kikuu cha majumuisho.

Ufafanuzi, Tume imejiridhisha kuwa Msimamzi wa Uchaguzi kupitia barua yenye Kumb. Na.KMC/U.21/06/119 ya tarehe 14 Februari, 2018 alivijulisha Vyama vyote vya Siasa vinavyoshiriki Uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Kinondoni eneo na muda wa kuanza kujumlisha hesabu za kura. Kwa mujibu wa barua hiyi ambayo CHADEMA walipatiwa, Kituo cha majumuisho ya hesabu za kura ni Biafra na zoezi la majumuisho ya hesabu za kura litaanza majira ya saa kumi na mbili jioni (12:00) siku ya Uchaguzi.

Aidha, kupitia barua hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi alivitaka Vyama vya Siasa vyenye wagombea kuwasilisha majina ya Mawakala wa Kujumlisha Kura.

Hoja ya Sita, kwamba, Uteuzi wa Wasimamizi wa Vituo ambao ni Makada wa Chama cha Mapinduzi kutoka Temeke, Ilala na Kinondoni na majina yao kutowekwa hadharani.

Ufafanuzi, Kifungu cha 7(4)(5) 2015 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343, ikisomwa pamoja na Kanuni ya 14 na 15 ya Kanuni cha Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani za mwaka 2015 na kipengele cha 10.1.(ii) cha Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea ya mwaka 2015 kwa pamoja umewekwa utaratibu wa namna ya kuwapata Wasimamizi wa Vituo na Wasimamizi Wasaidizi wa Vituo na namna Vyama vinavyoshiriki uchaguzi vinavyoweza kuhusishwa katika utaratibu wa kuwapata Watendaji hao.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Tume inazo, taratibu zote za kuwapata watendaji hao zilizingatiwa ikiwa ni pamoja na kutangaza nafasi za kazi, waliohitaji kuomba, kuchujwa waliokuwa na sifa zinazohitajika, kufanyika usaili na majina ya walioteuliwa kuwa Wasimamizi wa Vituo na Wasimamizi wa Vituo Wasaidizi kubandikwa kwenye mbao za matangazo katika Ofisi za Kata zote kumi katika Jimbo la Kinondoni.

Hata hivyo, kwa mujibu wa barua yenye Kumb. Na. KMC/U21/06/12 ya tarehe 11 Februari, 2018 Msimamzi wa Uchaguzi aliwasilisha orodha ya Watendaji hao kwenye Vyama vinavyoshiriki katika Uchaguzi.

Kuhusu, kuwepo kwa wapiga kura 3065 watakaopiga kura na ambao hawakuadikishwa katika Jimbo la Kinondoni. Tunapenda kuwakumbusha kuwa, kifungu cha 63(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kimeweka utaratibu wa nani anayeruhisiwa kupiga kura. Hivyo, hakuna atakayeruhusiwa kupiga kura iwapo hajaandikishwa na jina lake halipo katika orodha ya wapiga kura waliopo katika daftari.

Nashukuru kwa ushirikiano wako.

Kailima, R.K

MKURUGENZI WA UCHAGUZI