Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

TUME ya TEHAMA, imeelezea kufurahishwa na uamuzi wa Serikali wa kuanzisha Maonesho ya Anuani za Makazi ikisema ni jukwaa muhimu la kufikisha elimu juu ya mchango wa anuani katika uchumi wa kidigitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya kwanza ya Anuani ya Makazi, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga alisema Mfumo wa Anwani za Makazi ni nyenzo ya utambuzi ambayo inarahisisha utoaji na upokeaji wa huduma mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya Kiuchumi na kijamii.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, DKt. Nkundwe Mwasaga akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia na Habari, Jerry Silaa jana katika Viwanja vya Maonesho ya Anuani za Makazi jijini Dodoma. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange.

Alisema katika zama hizi ambazo Mapinduzi ya 4,5 na 6 ya viwanda yanategemea matumizi ya TEHAMA, ushiriki wa Tume ya Tehama katika kutoa elimu kwa Watanzania ni muhimu kwani wao ni sehemu ya kusaidia uwapo wa mifumo thabiti ya utambuzi.

“Katika maonesho haya, ni muhimu sana kwetu sisi kama Tume, lakini kwa taifa kwa ujumla kuweza kuendelea kuwafikia Watanzania wa mijini na vijijini waweze kufahamu umuhimu wa anuani za makazi kidigitali ili kila mmoja ashiriki katika kuujenga uchumi wa kidigitali.

“Kote duniani inafahamika kuwa uchumi wa kidigitali ni uchumi wa watu. Watu ili waweze kutumia mifumo kufanya shughuli zao kidigitali, wanahitaji kupata uhakika wa kufikishiwa huduma katika maeneo yao, iwe ofisini na nyumbani. Kwa hiyo katika utambuzi wa kidigitali, anuani ni ya msingi sana,” alisema Dkt. Mwasaga huku akisisitiza wabunifu kuelekeza nguvu katika ubunifu ili kuwafikia Watanzania.

Maonesho hayo ya anuani za makazi yaliyozinduliwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa jijini Dodoma, yakiwa na kauli mbiu ya: “Tambua na Tumia Anwani ya Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma” yameshirikisha pia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa (Katikati walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa wizara na taasisi zinazoshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Maonesho ya Anuani za Makazi yanayoendelea jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto waliosimama na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga
.

Mbali ya Tume ya TEHAMA taasisi nyingine zinazoshiriki katika maonesho hayo ni Posta, RITA, NIDA, UCSAF, TTCL, TCRA, TCRA CCC,NEMC, Tume ya Taarifa Binafsi, Makampuni ya Mawasiliano kama “YAS”, NMB na TANAPA.

Serikali kupitia Tume ya TEHAMA, iko katika juhudi kubwa za uwekezaji na uendelezaji wa Sekta ya TEHAMA, ikielekeza nguvu katika uanzishwaji wa vituo vya kikanda vya kukuza bunifu za sekta hiyo nchini.

Kwa kuanzia, vinaelekezwa Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Tanga na Zanzibar.
Aidha, juhudi zinaendelea kuanzisha vituo vya kukarabati na kutengeneza vifaa vya TEHAMA kwenye mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.

Ili kuwafikia wananchi, Serikali pia inaelekeza nguvu katika ngazi za wilaya ili nako kujengwe vituo vya kukuza bunifu za TEHAMA. Baadhi ya wilaya zitakaanza kunufaika ni Masasi, Kibaha, Rufiji, Tanganyika, Bukoba na Butiama.