Na Mwandishi Wetu, JamburiMedia, Dar es Salaam

WATUMISHI wa Tume ya Tehama nchini, wamepatiwa mafunzo juu ya mifumo mipya ya kielektroniki ya Upimaji Utendaji Kazi kwa Taasisi za Umma (PIPMIS) na Mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS).

Mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, yamelenga kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Upimaji wa Utendaji Kazi (OPRAS) na mfumo wa PIPMIS umeundwa kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye mfumo wa Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma (IPCS).

Kwa mujibu wa Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jonas Chacha kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, mfumo wa PEPMIS utapunguza na kuondoa matumizi ya karatasi, kuongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji na utendaji kazi kwa watumishi.

“Mfumo huu mpya wa PEPMIS ni matunda ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassana aliyetaka upatikane kupata mfumo sahihi wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma na taasisi zake ili kuondokana na kero za usimamizi wa utendaji kazi zilizojitokeza katika utekelezaji wa mfumo wa awali wa OPRAS, ambao haukuakisi hali halisi ya utendaji kazi wa watumishi hali iliyoleta hisia za kupendeleana au kuoneana.


“Mfumo mpya wa PEPMIS utakuwa ni wa kielektroniki na utaondokana na matumizi ya makaratasi, pia utaongeza uwazi katika usimamizi wa watumishi na kuondoa upendeleo na uonevu katika upimaji wa utendaji wa watumishi,pia mfumo huu pia utahamasisha uwajibikaji wa hiari na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za utendaji kazi wa watumishi,” alisema Chacha.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Williard Kalulu akifungua mafunzo hayo ameishukuru Ofisi ya Rais – Utumishi kwa kuwafikia watumishi wa Tume ya Tehama kwa lengo la kutoa mafunzo ya namna ya kutumia mifumo hiyo ya kidigitali kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa watumishi wake ambapo ameihakikishia ofisi hiyo kupata ushirikiano wa kutosha.

Aliwataka pia watumishi kuzingatia mafunzo hayo kwani ni fursa muhimu katika kupima utendaji kazi kwa watumishi.

Sehemu ya viongozi na watumishi wa Tume ya Tehama nchini, wakifuatilia kwa umakini mafunzo juu ya mifumo mipya ya kielektroniki ya Upimaji Utendaji Kazi kwa Taasisi za Umma (PIPMIS) na Mfumo wa Upimaji Utendaji Kazi kwa Watumishi wa Umma (PEPMIS) yanayoendeshwa na Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliyoundwa kwa lengo la kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye mifumo ya awali ya OPRAS (Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Upimaji wa Utendaji Kazi) na ule wa IPCS (Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi za Umma).

Tume ya TEHAMA ni taasisi ya serikali iliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ilianzishwa ikiwa na jukumu la kuwezesha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA pamoja na sera nyingine zinazohusiana na kuendeleza matumizi ya TEHAMA nchini; kukuza na kuvutia uwekezaji wa TEHAMA nchini ili kuwezesha kutengeneza ajira na kuchangia katika shughuli za kiuchumi na kijamii; pamoja na kuimarisha uratibu wa shughuli za TEHAMA ili kuongeza mchango wa TEHAMA katika uchumi wa taifa.

Katika Kutekeleza malengo yake, Tume ya TEHAMA inatoa ushauri kuhusu mipango ya kimkakati, utekelezaji na uwekezaji katika TEHAMA, kufuatilia na kuratibu TEHAMA nchini, pamoja na kutoa mwelekeo kuhusu mienendo na fursa za TEHAMA kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi.

Kwa Tume, utekelezaji wa majukumu hayo hufanyika kupitia, kukuza uwekezaji katika TEHAMA, kujenga uwezo na kukuza taaluma na viwango katika TEHAMA, kushauri na kushirikiana na wadau wengine kuhusu tafiti, kuweka viwango na mwelekeo katika TEHAMA na kuandaa na kuimarisha miundombinu na programu za kitaifa za TEHAMA.