Dodoma

Leo Februari 11, 2025 Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janet R. Lekashingo ameongoza kikao cha Kamisheni ya Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Madini kwa kipindi cha miezi mitatu sambamba na kuweka mikakati ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kikao hicho kilichoshirikisha Makamishna wa Tume na Menejimenti kimeendelea kuweka mikakati mipya ya kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kuwa na mchango kwenye Pato la Taifa kupitia uboreshaji wa usimamizi kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini, ukusanyaji wa maduhuli na masoko ya madini na udhibiti wa utoroshaji wa madini.

Akielezea mafanikio ya Tume ya Madini tangu kuanzishwa kwake, Katibu Mtendaji wake, Mhandisi Ramadhani Lwamo ameeleza kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa 30 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Ofisi za Maafisa Migodi 13 kwa Migodi Mikubwa na baadhi ya Kati; Masoko ya Madini 43 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 108.

Ameeleza mafanikio mengine kuwa ni pamoja na Uboreshaji wa Huduma za Maabara kwa Wachimbaji na Wafanyabiashara wa Madini; Uwepo wa mifumo thabiti ya kieletroniki ya ukusanyaji wa mapato pamoja na utoaji wa leseni; Ushirikiano thabiti wa ndani na nje ya Tume ya Madini dhidi ya Mamlaka nyingine za Serikali na kuendelea kukua kwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali na maboresho ya Sheria, Kanuni na Taratibu na miongozo inayosimamia Sekta ya Madini.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mwenyekiti wake, Janet Lekashingo amepongeza kazi nzuri inayofanywa na Tume ya Madini hasa kwenye eneo la ukusanyaji wa maduhuli, usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa nchini, kuimarika kwa usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na mchango wa kampuni za madini kwa Jamii.

Kupitia kikao hicho mikakati mbalimbali imewekwa kupitia Kamati za Ufundi, Rasilimaliwatu, Fedha na Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.