Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Tume ya Utumishi wa Walimu na Tume ya Utumishi wa Mahakama zimekubaliana kuwa na ushirikiano wa karibu, kukutana mara kwa mara na kupeana uzoefu kwani zote mbili zinatekeleza majukumu yanayofanana.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Paulina Nkwama alitoa kauli hiyo alipotembelewa kwenye tume hiyo na ujumbe wa viongozi kutoka Tume ya Utumishi wa Mahakama kuja kujifunza namna tume hiyo inavyofanya kazi.

Paulina alisema pamoja na kwamba TSC na Tume ya Mahakama kila moja inatekeleza sheria yake, taasisi hizo kuna wakati hulazimika kutumia Sheria ya Tume ya Utumishi wa Umma sura 298 ambayo ndiyo sheria mama kusimamia utumishi wa umma.

“Ni muhimu kwa Tume ya Utumishi wa Walimu na Tume ya Utumishi wa Mahakama kukutana na kupeana uzoefu kwa kuwa tunatekeleza majukumu yanayoendana. Ni vema kukutana ili kubadilishana uzoefu na kutoa fursa ya kila upande kujifunza kutoka kwa mwenzake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa wetu,” alisema.

Katika Kikao hicho cha pamoja, TSC iliwasilisha mada juu ya muundo na majukumu ya tume ya utumishi wa walimu, taratibu za uendeshaji wa vikao vya tume na kamati za tume za wilaya na mchakato wa nidhamu kwa walimu.

Akizungumza baada ya kutembelea TSC, Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Alesia Mbuya alisema wametembelea makao makuu ya tume hiyo ili kujifunza namna TSC inavyotekeleza majukumu yake katika kusimamia walimu.

Alesia alisema lengo la kufanya ziara hiyo ni kujifunza namna ambavyo TSC inatekeleza majukumu yake ikiwa ni mamlaka ya ajira na nidhamu kwa walimu kwa kuwa majukumu yake yanaendana na yale ya Tume ya Utumishi wa Mahakama ambayo ni mamlaka ya ajira na nidhamu kwa watumishi wa mahakama.

Tume ya Utumishi wa Mahakama pamoja na mambo mengine ilihitaji kufahamu kwa kina muundo wa tume ya utumishi wa walimu, namna mashauri ya nidhamu yanavyoendeshwa na sheria ya tume ya utumishi wa walimu sura 448 kwa ujumla wake.

Please follow and like us:
Pin Share