Zipo njia nyingi za kutuma ujumbe kutoka upande mmoja kwenda wa pili. Njia hizo ni kama vile barua, shairi, wimbo na nyinginezo. Kila ujumbe una madhumuni na malengo yake. Mathalani kuelimisha, kuhamasisha, kutoa taarifa fulani na kadhalika.
Wimbo ni tungo fupi ya muziki wenye maneno yaliyopangwa ambayo hunenwa kwa mpangilio maalumu pamoja na ala au vyombo mbalimbali vya muziki. Ziko aina tofauti za nyimbo ambazo watu huzitumia katika mambo yao.
Baadhi ya aina za nyimbo ni zile za kuhimiza kufanya kazi, kusifu na kupongeza viongozi au mashujaa, kubembeleza watoto wadogo, kuomboleza na zile za kutoa hekima na mafunzo.
Leo katika fasihi hii ninaangalia wimbo uliopewa jina la Tamaa Mbaya uliotungwa na kuimbwa na msanii Abbas K. Kinzasa, maarufu 20% (twente pa senti). Ni kijana mkazi wa Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.
Ni wimbo wa siku nyingi kidogo, wenye melodi nzuri na kuvutia msikilizaji, ridhimu yenye kusisimua akili na midundo yenye kuchangamsha mwili wa mchezaji. Lakini hilo si lengo langu la kuusifu muziki wenyewe. Nia ni kuangalia hekima na falsafa zilizotumika katika maneno yaliyounda wimbo huu.
Baadhi ya mistari katika wimbo imebeba maneno yafuatayo: “Tuliza moyo wako, kubali mapungufu yako, rahisisha mahitaji yako, ongeza kipato chako, chunga tamaa yako.” Mistari yote imebeba hekima na kuonyesha upevu wa falsafa ilivyotumika.
Moyo wa binadamu una sifa nyingi, ikiwemo ya kupenda kitu au jambo kutokana na ubora au uzuri wake, ikifuatiwa na tamaa.
Tamaa ni hamu kubwa ya kufanya jambo na kujawa matarajio ya kupata kitu. Moyo una tabia ya kumshawishi na kumsukuma binadamu kupata mambo mazuri.
Moyo una tamaa ya kupata mazuri au kufanya mabaya kukidhi haja. Moyo humtia binadamu matatani na furahani, iwe katika kazi au mapenzi. Ndipo msanii 20% anaponena: “Tuliza moyo wako na kubali mapungufu yako.” Usiuendekeze moyo. Ni hatari. Tumia kilicho ndani ya uwezo wako.
Binadamu anayo mahitaji mengi na kamwe hawezi kuyatimiza yote katika uhai wake hapa duniani. Ni busara kutimiza yaliyo ndani ya kipato chake. Si kutimiza utakavyo moyo wake. Watumishi wa umma na wa watu binafsi watambue hali hiyo. Kumbuka kurahisisha mahitaji yako.
Moyo unapoutuliza na ukakubali mapungufu yako, utarahisisha mahitaji. Unapodhibiti mahitaji unapata nguvu na fikra pevu kutafakari mustakabali wa mwenendo wa maisha yako. Na hapo utawaza kuongeza kipato chako na kuchunga tamaa isikupuruchuke na ukaingia hatiani.
Kipato cha binadamu kinapatikana na kuongezeka kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, si kwa kuweka tamaa mbele. Binadamu wanaofanikiwa kuongeza vipato vyao ni wale wanaochapa kazi. Vipato vyao ni vya halali na vya kudumu. Msingi wamechunga tamaa zao.
Wimbo Tamaa Mbaya umemgusa Waziri wa Madini, Doto Biteko na watu wengine wengi. Waziri Biteko alitumia maneno ya wimbo huu kuwa kielelezo cha nasaha, alipokuwa akizungumza na maofisa Madini hivi karibuni katika ziara yake mkoani Mwanza.
Maofisa Madini hao wametakiwa kufanya kazi kwa ari, utii na uaminifu. Walinde na kudhibiti madini yasiibwe, yasitoroshwe na taifa letu lisihujumiwe kupitia madini. Waziri alikariri baadhi ya mistari na kuwaambia maofisa hao. Alisema: “Kubali mapungufu yako, ridhika na ulichonacho, ongeza kipato chako na chunga tamaa mbaya.”
Ninawaomba Watanzania wenzangu tuupokee, tuukubali na tuuzingatie ujumbe huu muhimu. “Tamaa mbaya.” Watu waadilifu na waaminifu tunasema: “Tamaa mbele, mauti nyuma.” Ukiiruhusu tamaa ikuongoze, mwisho wake utajiingiza katika matatizo makubwa.
Mwisho