Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kwa kupitia Gazati hili la JAMHURI niweze kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu ambaye anatukrimia mema mengi katika maisha yetu ya kila siku.
Naamini kwamba tunaweza kuyamudu maisha yetu ya kila siku kutokana na neema yake. Hivyo hatuna budi kumshukuru Mungu na kulihimidi jina lake Takatifu kwa mema mengi anayotutendea kila siku.
Napenda pia nichukue fursa hii kushukuru uongozi mzima wa Gazeti hili kwa kunipa hisani kubwa ya kuchapa makala hii na kwa kupitia Gazeti hili kuweza kuufikisha ujumbe husika kwa baadhi ya Watanzania maana si wote wanaobahatika kulisoma Gazeti hili.
Nimeona ni vyema nitoe mchango wangu kimawazo juu ya umuhimu wa kulipa kodi (Government tax) ili kuiwezesha Serikali ya Awamu ya Tano kuweza kufanya kweli katika mikakati yake ya kutuletea maendeleo endelevu.
Watanzania tunatamani sana kupata maendeleo ya kweli, lakini maendeleo hayo hatutayapata katika misingi tunayoitarajia iwapo uwezo wa Serikali yetu utakuwa mdogo (kifedha lakini pia kiutendaji).
Nikiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Uongozi wa Taifa letu, kwa miezi kama minane ambayo imekuwa madarakani chini ya Rais Dk. John Magufuli (JPM); imeweza kuonesha dhamira ya dhati ya kutaka kuwaletea maendeleo ya kweli Watanzania wote.
Ninaposema hivyo simaanishi kuwa tangu tupate Uhuru- Desemba 9, 1961 hadi sasa Serikali zilizokuwa madarakani hazikufanya lolote kuwaletea maendeleo Watanzania.
Nathubutu kusema kuwa Serikali zilizopita zimejitahidi kufanya tunayoyaona leo. Kwa mfano, tangu Uhuru hadi sasa shule zimeongezeka mno, huduma za afya pia, na miundombinu na mengineyo mengi. Pamoja na hayo yote, kumekuwapo malalamiko kuwa maendeleo ambayo tumeyapata hadi sasa hayaendani na hali halisi ya rasilimali nyingi tulizonazo katika nchi yetu- zikiwamo za maliasili (wanyamapori, misitu, madini, ardhi yenye rutuba, maziwa, mito ukanda wa bahari) na vilevile kuwapo rasilimali watu takribani milioni 45 sasa kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Hii ni hazina kubwa kwa Taifa kuweza kujiletea maendeleo.
Serikali ya Awamu ya Tano imekuja na kaulimbiu: “HAPA KAZI TU” ikiashiria kuwa iwapo rasilimali watu itafanya kazi kadri ya uwezo wake na pia kulipa kodi ipasavyo: tukazitumia kwa weledi, hakuna kitakachotuzuia tusipate maendeleo tunayoyataka.
Huduma kwa jamii kama elimu, afya, maji, barabara, kilimo na mifugo na mazingira katika ujumla wake vitaboreshwa na kuimarishwa ipasavyo. Ndiyo maana kwa muda mfupi Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha njia kuwa inawezekana tukajiletea maendeleo endelevu iwapo tutafanya kazi kwa bidii, kujituma na kuliweka Taifa letu mbele i.e. Tanzania kwanza ubinafsi baadaye.
Wanasiasa mahiri waliotangulia akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Kwanza ya Uongozi wa nchi yetu: aliwahi kusema “unalifanyia nini taifa lako badala ya kuwa na mawazo ya Taifa linakufanyia nini”.
Iwapo tutalipa kodi kwa moyo mkuu tutakuwa tunatimiza wajibu wetu na hivyo kuwa na nguvu ya kuhoji; “taifa linatufanyia nini?” Lakini tunapokwepa kulipa kodi na wakati huo huo kulalamikia huduma mbaya kwa jamii, tutakuwa hatutendi haki kwa Serikali iliyopo madarakani. Kimsingi inatakiwa sisi tutimize wajibu wetu kwa kuiwezesha Serikali na ndipo tuhoji nini kinaendelea kuhusiana na maboresho kwa huduma za kijamii na masuala yote ya maendeleo ya Taifa letu.
Kama nikivyokwisha kueleza huko nyuma kwamba tumekuwa tukilalamikia maendeleo hafifu, lakini kila mmoja wetu ajiulize je, nimefanya nini kuliendeleza Taifa langu? Je, nimelipa kodi ipasavyo au ni katika kundi la wanaokwepa kulipa kodi? Je, nimetimiza wajibu wangu ipasavyo na kwa uzalendo mkubwa kwa nafasi niliyonayo?
Kama ni mkulima, mfugaji, kiongozi kwa ngazi zote, mfanyakazi kwa ngazi mbalimbali, mfanyabiashara mkubwa au mdogo, mjasiriamali, iwe ni mwenye kiwanda, mtoa huduma ya aina yoyote ile ofisini, hospitalini, shuleni, kwenye madhehebu ya dini, kwenye sekta ya usafirishaji, usindikaji bidhaa, katika biashara na kadhalika.
Tunaposema wananchi wanataka maendeleo ni vyema pia tukatimiza wajibu wetu na kuwajibika ipasavyo kwa kila mwenye uwezo wa kufanyakazi akafanya hivyo kwa juhudi na maarifa tukizingatia busara au hekima tunayojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa muda mfupi Selikali ya Awamu ya Tano (takribani miezi minane) Mheshimiwa Rais ameonesha kuwa inawezekana kwa Watanzania kujiletea maendeleo wanayoyataka.
Mathalani, jambo la kwanza: ndani ya muda huo mfupi tumeshuhudia madawati mengi yametengenezwa. Vilevile, unajiuliza ilikuwaje tukaacha watoto wetu wakasoma kwa kukaa chini kwenye vumbi. Je, tulikuwa tumefunikwa na wingu gani?
Isitoshe Tanzania inayo misitu ya asili mingi na mashamba ya miti yenye taribani hekta 100,000 kwa upande wa Serikali na kwa sekta binafsi takribani hekta 250,000. Je, kwa rasilimali misitu na nguvukazi tuliyonayo pamoja na rasilimali fedha zilizopo tunaweza kujitetea vipi kwa kushindwa kuwatengenezea madawati watoto wetu hadi wakawa wanasoma kwa kuketi chini kwenye vumbi?
Ni dhahiri kulikuwapo uzembe katika kutimiza wajibu wetu kama wazazi na kama Watanzania kwa ujumla. Jambo la pili; kwa muda mfupi tunashuhudia ongezeko la ukusanyaji kodi hadi kufikia fedha za Tanzania zaidi ya shillingi trilioni moja kwa mwezi. Kila jitihada zinafanyika kuziba mianya ya kukwepa kodi na kuhakikisha anayetakiwa kulipa kodi anafanya hivyo kwa mujibu wa sheria za nchi bila kushurutishwa.
Hii ni pamoja na jitihada za kutumia mashine za kielektroniki katika kutoa risiti kwa huduma au bidhaa zinazonunuliwa na mtumiaji/mlaji.
Tatu, tumeshuhudia pia mapambano ya dhati kwenye vita ya watumishi hewa ambao kila mwezi wamekuwa wakilipwa mishahara na marupurupu bila ya kuwapo kazini au kutolewa huduma husika.
Nne, kuongezeka nguvu dhidi ya maovu kama ufisadi, rushwa, biashara ya dawa za kulevya, na ujangili.
Tano, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutolipa karo; na
Sita, kuanzisha mapambano dhidi ya uchafu katika majiji, miji na vijiji.
Ukubali usikubali, ni dhahiri kuwa sasa amekuja Rais ambaye kwa kupitia kauli zake halali kama Kiongozi Mkuu wa nchi, mambo yamefanyika tena kwa muda mfupi ambao wengi wetu hatukutarajia utekelezaji uende kasi kwa kiwango hicho.
Iwapo kweli tunataka kupata huduma za kijamii zilizoboreshwa za elimu, afya, maji, miundombinu na ushauri uliotukuka kwa wakulima na wafugaji; hatuna budi kama Watanzania walio na nia njema tuiwezeshe Serikali ya Awamu ya Tano kwa KULIPA KODI ipasavyo ili iweze kufanya kweli.
Baadhi yetu Mwenyezi Mungu ametujalia vipaji mbalimbali vivyo hivyo kwa vipaji au kwa maneno mengine tunazo talanta kwa viwango tofauti. Kuna walio na talanta na karama kubwa kama wafanyabiashara na wenye viwanda wakubwa. Wapo pia wenye viwango vya kati na wapo wenye viwango vya chini.
Wapo wakulima wenye mashamba makubwa; vivyo hivyo kwa wenye mifugo mingi kwa mfano ng’ombe zaidi ya 3,000; na wapo wakulima wa viwango vya kati na wale wadogo. Vivyo hivyo kwa waajiriwa kazini: ofisini na sehemu nyingine za kazi na hao pia wako katika viwango tofauti vya mishahara na marupurupu.
Wote kwa ujumla ni Watanzania na Taifa hili ni letu sote; hivyo tujivunie kulipa kodi kadri Mwenyezi Mungu alivyotujalia kuwa na karama na talanta mbalimbali. Naamini kodi tutakayolipa itaiwezesha Serikali kutimiza malengo na dhamira yake ya kutuletea maendeleo ya kweli.
Tusiongope kulipa kodi eti Watanzania wachache watafaidika na ulipaji kodi wakati walio wengi wakibaki na hali zao za chini. Nimesikia minong’ono ya aina hiyo wakati nilipotembelea Manispaa ya Morogoro, Jiji la Mwanza, Sengerema kwa nyakati tofauti Juni na Julai, mwaka huu; na pia katika Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi yetu tunahofu kuwa bado kiwango cha ufisadi kinatisha na baadhi ya watumishi wa Serikali si waaminifu. Hivyo ukusanyaji kodi unaweza kufanyika, lakini fedha nyingi zikaishia kwenye mifuko ya wachache.
Hali ya hofu kama hii inaashiria maumivu ambayo mtu amewahi kuyapata. Hii ni kama “binadamu aliyewahi kujeruhiwa na nyoka- nyasi zikimgusa wakati anatembea atashutuka tu” akidhani ni nyoka. Kwa hali ilivyokuwa huko tulikotoka woga kama huu utakuwapo tu hadi hapo itakapothibitika kuwa sasa mambo yamebadilika kweli kweli na wakaanza kuyaona matunda ya jasho lao katika uhalisia wake.
Ni mapema mno kuweza kuwatoa hofu baadhi ya Watanzania, lakini tujipe moyo. La msingi tuiamini Serikali ya Awamu ya Tano kwamba kwa mwanzo aliouonesha Mheshimiwa Rais na kwa muda mfupi tu tuamini kwamba atafanya kweli.
Naamini haitachukua muda mrefu tutayaona mabadiliko ya kweli ikiwa ni ishara kwamba kodi tunayolipa inafanya kazi kwa faida ya Watanzania wote. Hakuna miujiza itakayofanywa na Serikali iwapo tunachenga kulipa kodi. Serikali zote duniani hutegemea kodi kuweza kuwahudumia wananchi wake.
Kwa msingi wa “Hapa Kazi Tu” na kutekeleza sheria kwa umakini na maadili ya hali ya juu pamoja na kufanya kazi kwa bidii, hakuna litakaloshindika. Wala rushwa na mafisadi pamoja na watumishi wa umma wasio waaminifu watashughulikiwa ipasavyo kwa kutowaonea aibu na bila ya hila au aina yoyote ya ukandamizaji.
Hii ni pamoja na kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kwa kuongozwa ka roho ya hekima na busara hivyo kuweza kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya Watanzania wote. Hakuna lisilowezekana, timiza wajibu wako. Lipa kodi kwa maendeleo yako na Taifa letu. Tuiwezeshe Serikali ili nayo kwa kupitia kodi zetu ituwezeshe ikiwa ni pamoja na kuzingatia umuhimu na mahitaji ya huduma za kijamii kwa nchi nzima.
Mwenyezi Mungu atujalie tuishi kwa amani, atuongezee hekima na busara ndani ya nchi yetu. Tusiwe wepesi wa kulaumu, bali tuwe wavumilivu na kwa umoja wetu na amani tuweze kulisukuma gurudumu la maendeleo bila ya woga au kuoneana haya tukiongozwa na Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chanzo cha mema yote na upendo wa kweli.
Tujitahidi kuijenga nchi yetu maana ni sisi wenye dhamana ya kulijenga Taifa letu. Nia tunayo, sababu ya kulipa kodi ipo na uwezo wa kufanya hivyo upo; hivyo tusonge mbele, kurudi nyuma mwiko.