Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Pwani

Daraja jipya la kisasa Wami ambalo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na mikoa ya Kaskazini limeanza kutumika rasmi oktoba 27, mwaka huu ambapo linakwenda kuwa tija kwa takriban miaka 120 ijayo.

Aidha daraja hilo, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 96 kwa ujumla asilimia 99 kwa Maendeleo ya kazi za Daraja na asilimia 93 kwa Maendeleo ya kazi za barabara unganishi.

Akikagua daraja hilo lenye M 513.5 na barabara unganishi km.3.8 ,lililoanza kutumika na magari kuruhusiwa kutumia daraja hilo ,Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alieleza ,daraja hilo litafungua uchumi na maendeleo ya wilaya ya Bagamoyo , mkoa wa Pwani na nchi kijumla.

Hata hivyo,ameeleza daraja hili linategemewa kupunguza kwa asilimia kubwa ajali za mara kwa mara zilizokuwa zinatokea kwenye daraja la zamani ambalo lilikuwa jembamba na lenye barabara zenye miiinuko mikali.

Ameeleza Ujenzi wa daraja jipya una lengo la kutatua changamoto zitokanazo na daraja la zamani ambalo kwa sasa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita (mwaka 1959) .

Mbarawa amefafanua, ujenzi ulianzishwa na Serikali ya awamu ya tano oktoba ,mwaka 2018 chini ya hayat John Magufuli na kuacha ujenzi kwa asilimia 44 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekamilisha kwa asilimia 52.

“Sikuja kuzindua nimekuja kupitisha magari katika Daraja hili la WAMI ,wajibu wetu mkubwa kumshukuru Rais kwa utekelezaji wake na kujivunia Daraja kukamilika” amesema.

“Wapo waliosema miradi inasuasua ,haitaendelezwa ,Lakini leo sisi tunashuhudia utekelezaji wa mradi huu mkubwa,mradi huu ulikuwa ikamilike Novemba mwaka huu lakini Oktoba 27,tunashuhudia daraja limekamilika kabla ya muda, Nani Kama Samia ,” amefafanua Mbarawa.

Amewataka wananchi walilinde na kulitunza daraja ili liweze kudumu kwa muda mrefu Kama lilivyosanifiwa kufikia miaka 120 ijayo.