Rais Barack Obama wa Marekani aliingia Tanzania Jumatatu Julai 1, mwaka huu, akaondoka Jumanne Julai 2. Mambo mengi yalitokea wakati wa ziara yake. Mengine ni mazuri tuyaendeleze, mengine ni mabaya tujisahihishe. Yote hayo ni mafunzo tuliyopata kutoka ziara ya rais huyu wa Marekani mwenye asili ya Afrika.
Kwanza kabisa ziara ya Rais Obama imetufunza kwamba misingi muhimu ya Taifa hili aliyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere bado ipo. Ziara yake imetudhihirishia kwamba bado Watanzania wana umoja, wanapenda amani na ni wakarimu.
Halafu tumejifunza kwamba wanajua kwamba serikali yao ina upungufu wake, lakini wakati huohuo inafanya mambo mengi mazuri, kwa hiyo hawakuiachia serikali peke yake mzigo wa kumpokea Obama.
Hii ni kusema kwamba juhudi zozote zinazofanywa na watu wachache za kuwatenganisha wananchi na serikali yao hazijafanikiwa na hazitafanikiwa. Kisha tumejifunza kwamba hakuna uhusiano mzuri kati ya serikali na vyama vya upinzani. Kwa hiyo, tayari wapinzani wamelalamika kwamba serikali imewatenga katika ziara ya Rais Obama.
“Mpaka sasa hatujapata mwaliko lakini hatuwezi kupigania kwani kuna mambo mengi ya kufanya kama kupigania upatikanaji wa huduma za afya na matatizo ya wananfunzi wa vyuo vikuu, na hilo la ziara si jambo kubwa,” ndivyo alivyojifariji Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Julius Mtatiro.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ofisa Habari wake, Tumaini Makene, alidai kuwa serikali ilishindwa kuwaalika wapinzani kukutana na Rais Obama kutokana na kuwaogopa kumwambia ukweli kuhusu unyonyaji unaofanyika nchini.
“Kama tungealikwa wapinzani na kupata wasaa wa kuzungumza na Obama, tungemwambia jinsi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyoitumia demokrasia vibaya,” alisema Tumaini.
Yote hayo ni matokeo ya uhasama uliopo kati ya chama tawala na serikali yake kwa upande mmoja, na vyama vya upinzani kwa upande wa pili. Katikati ya uhasama huu hapana shaka wa kulaumiwa ni wapinzani.
Wakati wote wako katika mapambano ya kupambana na CCM na serikali yake. Hakuna wakati wapinzani wanakaa kuisifu na kuipongeza serikali kwa jambo lolote zuri. Ni uhasama tu wakati wote.
Kwa hivyo, Makene hakukosea aliposema kwamba wapinzani wangepata nafasi ya kukutana na Rais Obama wangeisema vibaya CCM. Na serikali ilijua hilo mapema. Kwa hivyo, haikutoa nafasi kwa wapinzani kukutana na Rais Obama.
Ni vyema vyama vya upinzani vijifunze kujenga uhusiano mzuri kati yao na serikali wasijifanye tayari nao ni serikali, matokeo ya fahali wawili kukaa zizi moja ndiyo haya tunayoyashuhudia sasa. Vyama vya upinzani vinatengwa katika masuala muhimu.
Vile vile ziara ya Rais Obama imetufunza kwamba baadhi ya viongozi waliopo serikali wanajua kinachotakiwa kifanyike, lakini ni wazembe. Kwa mfano, waandishi tumeendelea kulipigia kelele suala la ombaomba linavyotia aibu na kadhalilisha taifa letu. Hata watoto wadogo hawaendi shule wanashinda barabarani wakiomba na kusumbua wenye magari.
Basi watu wa serikali waliposikia kwamba Obama anakuja, walianza kuwasaka na kuwakamata ombaomba eti Obama asiwaone! Uzembe usioneneka.
Katikati yetu tuna Wamarekani ambao wamemwambia Obama kwamba ombaomba waliondolewa barabarani kupisha ziara yake, ukweli ni kwamba watu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wameshindwa kufanya kazi yao, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ijue hilo.
Lakini pia Rais Obama ameambiwa kwamba kwa kawaida Dar es Salaam ni jiji chafu sana. Usafi umeonekana wakati wa ziara yake, yote hayo ni matokeo ya Serikali za Mitaa za Dar es Salaam kushindwa kutimiza wajibu wa kuliweka jiji katika hali ya usafi wakati wote. Obama amekwenda zake, turudini kwenye uchafu.
Halafu tumejifunza kuwa ziara za marais wa Marekani nchini, zinaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi. Tazama! Vibanda vya biashara hubomolewa ili kupisha ziara ya Rais wa Marekani, biashara ndogo ndogo zinapigwa marufuku, biashara zinafungwa na kadhalika. Mambo haya yote yanasababisha wananchi waichukie serikali yao na wachukie pia ziara zenyewe.
Wakati umefika wa Manispaa zote za Dar es Salaam kukutana na wafanyabiashara ndogo ndogo, kuwaambia kwamba maeneo yote ya Dar es Salaam hayaruhusiwi kufanya biashara, na kama inawaacha makusudi wafanye biashara maeneo hayo kwa kuwahurumia basi huruma hiyo waoneshwe kabla ziara ya rais yeyote haijaanza.
Kitendo cha serikali kuwabomolea wafanyabiashara hawa maskini na kuvuruga mitaji yao na malengo yao, kinalaaniwa sana hata na wananchi wasiojihusisha na biashara ndogondogo, yote hayo ni makosa ya maofisa mipango miji wanaolipwa mishahara kwa kusumbua na kunyanyasa vijana maskini wa Tanzania.
Kisha tumejifunza kwamba polisi wachache na watu wachache wa usalama hupenda kunyanyasa waandishi wa habari na wananchi kwa jumla, mbele ya maofisa usalama wa Marekani katika kujipendekeza. Hawajui kama wanajidhalilisha na wanaidhalilisha Tanzania.
Chukua, kwa mfano, Ofisa Usalama wa Tanzania aliyekataa kumruhusu mwandishi wa habari wa Gazeti la Uhuru, Selina Wilson, kuingia eneo la shughuli ya wake wa marais ingawa mwandishi alikuwa na kibali cha kuingia eneo hilo. Kitendo hicho liliwakera sana na kuwashangaza walinzi wa Marekani, wakawasiliana na uongozi wa juu kuhusu kitendo hicho cha Ofisa Usalama wa Tanzania.
Kuna watu wanalaumu hatua ya serikali ya kutoa mwito kwa wananchi kujitokeza barabarani kwa wingi kumpokea Rais Obama, lakini wanadai serikali iliwasumbua kuwaita barabarani huku ikijua kuwa ingemficha Rais Obama garini asionekane kwa wananchi.
Suala la kufichwa Rais Obama garini kwa vyovyote lilikuwa nje ya serikali, ulikuwa uamuzi wa maofisa usalama wa Marekani. Kilichobaki ni wananchi kuona fahari kwamba walishiriki mapokezi ya mgeni wa nchi yao.
Halafu kulikuwa na tatizo la kutokuwapo viongozi mbalimbali wa serikali katika ofisi zao na majaji mahakamani, kwa madai kwamba wamekwenda kwa Obama, lakini halikubandikwa tangazo lolote kuwasaidia wananchi wasipoteze wakati wao kuwasubiri watu ambao hawakuwapo. Hilo ni funzo jingine kuwa tusisumbue wananchi.
Haiwezekani kutaja mafunzo yote tuliyopata kutoka ziara ya Rais Obama nchini Tanzania, lakini funzo kubwa zaidi tulilopata ni kwamba ziara za Rais Kikwete za kwenda Marekani hazikuwa za bure, zimejenga na zimeimarisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani kwa manufaa ya pande zote mbili.