Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Msalala
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba amesema, wananchi wakilipa tozo na kodi vizuri, wanakuwa wameishaidia serikali kutekeleza majukumu yake kwao.
Hivyo, amewataka wananchi wa Msalala kuhakikisha wanalipa tozo na kodi mbalimbali katika halmashauri hiyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Katimba ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa ufunguzi wa stendi mpya ya Isaka ambapo amesema, Serikali inajitahidi kutekeleza malengo yake kama ilivyoahidi hivyo, wananchi nao wajitahidi katika ulipaji tozo na kodi mbalimbali za serikali.
“Serikali ni ya wananchi, tunapaswa kulipa tozo mbalimbali za serikali na kujiepusha na utoroshaji au ukwepaji wa kulipa kodi kwa kuwa, fedha zinazokusanywa hutumika kwa shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi huu wa tendi,” amesema Katimba.
Kwenye ufunguzi huo, mkurugenzi huyo amesema, stendi ya Isaka ni moja ya mipango ya muda mrefu ya serikali na kwamba, ufunguzi wake utaeleta afueni pia utaongeza wigo wa uchumi kwa wananchi na serikali.
“Natoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Msalala na maeneo jirani kuitumia stendi hii kwani uwepo wake ni moja ya sababu za ukuaji wa mji wa Isaka.
“Pia changamkieni viwanja kwani halmashauri imevipima karibu na stendi pembezoni mwa Barabara ya Isaka – Rwanda,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema, pamoja na mambo mengine, stendi hiyo imelenga kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji pia halmashauri hiyo kuongeza kipato kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwani ni chanzo cha uhakika.
Ameahidi kuwa, yeye na timu yake ya wataalam wataendelea na jitihada za kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika kama inavyoelekezwa na serikali.
Pia amesema, hadi kufika Machi 31, 2024 halmashauri hiyo tayari imekusanya asilimia 91 ya makusanyo ya Mfuko Mkuu ambayo ni sawa na 4.6 Bilioni.
Ofisa Mapato wa Halmashauri hiyo, Salehe Msosole ameishukuru uongozi wa halmashauri kwa kuweka msisitizo utendaji uliotukuka kwa watumishi wake ambao umesaidia kuongeza mapato ya halmashauri.
“Ukweli ulio wazi ni kuwa, ushirikiano wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mibako Mabubu na mkurugenzi wetu (Katimba) pamoja na watumishi umesaidia sana halmashauri hii.
“…hasa kuweka kipaumbele cha kwanza katika utendaji kazi wa kila siku, jambo ambalo limesababisha usimamizi mzuri wa mapato hasa msisitizo wa kila diwani katika eneo lake huhakikisha tozo za serikali zinalipwa kama inavyotakiwa,” amesema Msosole.
Ofisa mapato huyo alisema, mkurugenzi wa halmashauri hiyo aliunde kikosi kazi ambacho anakisimamia.
“Mimi nasimamia kikosi hicho, tunafanya doria usiku na mchana kuhakikisha tunadhibiti utoroshaji wa mapato, tangu tuanze usimamizi huu kila siku tunakamata magari yasiyopungua manne na Bajaj mbili.
“Natoa wito kwa wafanyabiashara kulipa tozo za halmashauri kwa hiari ili kujenga uchumi wa nchi yetu na kumuunga mkono Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa stendi hiyo, Majuto Pazi ambaye ni Diwani wa Kata ya Isaka amewaomba wananchi hasa wana Isaka kutumia fursa ya stemndi hiyo hiyo kujiongezea kipato.
Ofisa Mipango wa halamahauri hiyoi, amesema kukamilika kwa stendi hiyo, ni jitihada za pamoja za mkurugenzi mtendaji, madiwani, wataalam wa halmashauri ngazi za vijiji, kata, wenyeviti wa vijiji na wananchi wote.
“Namshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za kuwezesha kujenga stendi hii sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala, Idd Kassim Idd kwa ushawishi, kusimamia na kuhakikisha serikali na wawekezaji wanatoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ndani ya halmashauri.
Wananchi wanaozunguka stendi hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na ufunguzi huo kwani, uongozi wa kijiji umetangaza kugawa maeneo ya biashara ndani ya stendi hiyo.