NA MWANDISHI MAALUMU, DAR ES SALAAM
Kwenye gazeti la The Citizen la Ijumaa, Februari 16, 2018 kulikuwa na
stori ambayo pengine kutokana na hekaheka za uchaguzi wa marudio
wa majimbo ya Kinondoni na Siha, watu wengi hawakuipa uzito
unaostahili.
Stori inasema, eti Amerika imezitahadharisha nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) kwamba zitashikishwa adabu endapo zitaendelea na
mpango wake wa kuacha kuagiza mitumba,maarufu kwa jina la “kafa
Ulaya” kutoka Amerika.
Kwa mujibu wa stori hiyo, Harry Sullivan, aliye Kaimu Mkuu wa Idara ya
Uchumi na Mambo ya Kikanda katika Idara ya Mambo ya Afrika,
alinukuliwa na gazeti la Business Daily kwamba Tanzania, Uganda na
Rwanda zilikuwa na muda mfupi wa kujirudi na kusudio lao la kuachana
na uagizaji wa mitumba kabla hazijaadhibiwa!
Viongozi wa nchi hizi tatu wanatarajiwa kuamua kama waendelee na
uamuzi wa kupiga marufuku uagizaji wa mitumba kutoka Amerika au la!
Uamuzi wa nchi hizo tatu wa kuacha kuagiza mitumba kutoka Amerika
unachukulia na nchi hiyo kama kitendo cha kuzuia biashara huria na
halali.
Inaelezwa kwamba nchi wanachama wa EAC zilikubaliana miaka miwili
iliyopita kuacha hatua kwa hatua uagizaji wa mitumba kwa kipindi cha
miaka mitatu kuanzia mwaka ujao wa 2019.
Hata hivyo, Kenya ilijiondoa katika mpango huo mapema baada ya
kutishwa na Amerika kwamba ingezuiwa kuingiza pasipo ushuru bidhaa
zake nchini Amerika chini ya mpango wa AGOA (Africa Growth and
Opportunities Act).
Msimamo wa Amerika ni kwamba kuzuia uagizaji wa mitumba
kunakiuka makubaliano ya AGOA yanayotaka washirika kuondoa
vikwazo vya biashara na Amerika.
Rwanda, Tanzania na Uganda zote zinauza bidhaa kidogo nchini
Amerika ukilinganisha na Kenya. Hoja ya Tanzania, Rwanda na Uganda
ni kwamba kuzuia mitumba kutasaidia kuimarisha uchumi wa viwanda
nchini mwao hasa ule wa viwanda vya nguo. Lakini utawala wa Rais
Donald Trump unapinga hoja hiyo. Sullivan anakiri kwamba, ni kweli
Tanzania, Rwanda na Uganda zimedhamiria kujenga uchumi wa
viwanda kwa kuanza na viwanda vya nguo, lakini anadai mpango huo
hautafua dafu!
Kuzuia mitumba ya bei rahisi, kwa maelezo yake Sullivan, kutawanyima
watu wengi nguo za kuvaa.
Sullivan anadhani watu wa Afrika Mashariki wanafurahia kuvaa ‘kafa
ulaya’! Anasema eti, kwa Kenya kuacha kuagiza mitumba kutoka
Amerika kutasababisha kutetereka kwa soko la bidhaa zake huko
Amerika ambalo anadai liliingizia nchi hiyo dola milioni 400 za Marekani
mwaka jana.
“ Viongozi wa EAC wanawaambia watu wao kwamba tunaondoa
mitumba hii kutoka kwenu na kamwe hamtaipata,” anasema na
kuongeza kwa mshangao: “Tunajiuliza wananchi waliozoea kuvaa ‘kafa
ulaya’ wataweza kumudu nguo zilizozalishwa kwenye soko la Afrika
Mashariki!”
Kwake yeye Sullivan, njia rahisi kuendeleza viwanda vya ndani kwa soko
la nguo ni kuwashawishi wenye uwezo kununua vitu vya ndani.
Anasema kutengamaa kwa bidhaa za mavazi ya Afrika Mashariki ndio
njia sahihi kuinua bidhaa za viwanda vya nguo Afrika Mashariki.
Anachosema, Sullivan ni sawa na kusema kama nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki watafanikiwa kuja na bunio la nguo
tuseme ‘jeans’ za Afrika Mashariki au “madela” ya Afrika Masharika na
kuyauza kwenye maduka makubwa ya nguo (shopping malls), basi
uingizaji wa mitumba kutoka Amerika na Ulaya Magharibi utakoma
wenyewe.
Hayati Mahatma Gandhi wa India anakumbukwa sana na Wahindi kwa
jinsi alivyohimiza uzuiaji wa nguo za viwanda kutoka Ulaya Magharibi
hususan vile vya kutoka miji ya Liverpool na Manchester nchini
Uingereza na kuwataka watengeneze nguo zao.
Yeye mwenyewe akawa mstari wa mbele katika kutengeneza nguo
akianza na shuka lake mwenyewe maarufu kama ‘kikoi’. Siyo nguo tu,
Gandhi alikwenda mbali kuwazuia Wahindi wasinunue sukari kutoka
kwenye viwanda vya kampuni za kigeni. Badala yake akawahimiza
kutengeneza sukari yao (maarufu kama sukari guru) kwa mahitaji yao.
Watu walimsikiliza na kujitengenezea sukari kwa ajili ya matumizi yao
ya nyumbani. Haishangazi kwamba hadi leo, maeneo mengi ya vijijini
nchini India watu bado wanatengeneza sukari guru kwa matumizi ya
nyumbani, na ni nadra sana kukuta duka maeneo ya vijijini ambalo
linauza sukari kutoka viwandani!
Mawazo ya Gandhi yalichukuliwa kwa uzito mkubwa na kufanyiwa kazi.
Hata sera ya viwanda vidogo iliyohimizwa na Mwalimu Julius Nyerere
katika uhai wake nchini Tanzania, ilitokana na mafanikio waliyopata
Wahindi katika kujenga uchumi wa viwanda kwa kuanza na viwanda
vidogo na kisha viwanda vikubwa.
Juhudi za serikali za Afrika Mashariki kujenga uchumi wa viwanda
hazina budi kuungwa mkono na wana wa Afrika Mashariki wote.
Viwanda vya aina zote- vikubwa kwa vidogo – vinayo nafasi kubwa sana
katika kujenga uchumi na kutoa ajira kwa wananchi wake. Ni makosa
kuacha kuwasaidia wakulima wa pamba kwa kuanzisha viwanda vya
nguo na badala yake kuruhusu ‘kafa ulaya” eti kwa vile wananchi
wanapenda!
Ni upuuzi kusafirisha korosho za Mtwara, Lindi na Ruvuma kwenda
kuzibangua Jaipur, India na kisha kuzirejesha na kuziuza kwenye hoteli
zilizo karibu na miti zilikozalishwa kwa bei ya juu, eti tu kwa sababu
India wanabangua vizuri zaidi kuliko Nachingwea! Huo ni ujinga.
Laiti kama viwanda vya nguo vilivyojengwa wakati wa kipindi cha
Awamu ya Kwanza, vingesimamiwa vizuri na kuendelezwa, hakuna
mwana wa Afrika Mashariki ambaye angekuwa anavaa mitumba
anayoipigia upatu Sullivan.
Hukuna binadamu anayependa kuvaa nguo kuukuu iliyokusanywa
kusikojulikana kwa madai tu kwamba inauzwa kwa bei anayoweza
kuimudu!
Anachofanya Sullivan ni kujenga hoja ya kwamba Afrika Mashariki
iendelee kuwa soko la mitumba kutoka Amerika na Ulaya Magharibi
kama kwamba watu wa ukanda huu wa Afrika wanapenda kuvaa
mitumba ya watu waliokufa Ulaya na Amerika.
Hakuna ubishi kwamba Amerika ilichangia kwa kiasi kikubwa
kupatikana kwa uhuru kwa makoloni yaliyokuwa chini ya utawala
himaya ya nchi za Ulaya barani Afrika, Asia na Amerika ya Kusini.
Amerika ilizishinikiza nchi za Ulaya kuyaachia makoloni yake Afrika, Asia
na Amerika Kusini kwa minajili ya kuyageuza maeneo huru kwa biashara
hususan baada ya kumalizika Vita Kuu ya Pili ya Dunia na kuanzishwa
kwa Umoja wa Mataifa (UN).
Amerika ilifanya hivyo si kwa sababu ya huruma, bali ni sababu
Amerika haikuwa na makoloni hadi wakati huo. Ikaona njia rahisi kwa
upande wake kupata vyanzo vya kuaminika vya mali ghafi za viwanda
na pia masoko kwa mali zake, ilikuwa ni kuzishinikiza nchi zenye
makoloni kuyapa uhuru na kuruhusu biashara huria ili mwenye kuuza
au kununua aweze kufanya hivyo popote pasipo kuwa na vikwazo.
Kwa sababu hiyo, Amerika haipaswi kugeuka na kuzifanya nchi za Afrika
Mashariki eneo lake la biashara ya ‘kafa ulaya’ badala ya kujenga
uchumi wake wa viwanda, huko ni kurejesha ukoloni.
Rene Dumont, Profesa wa uchumi wa kilimo katika Chuo Kikuu cha
Uchumi wa Kilimo cha Paris, aliwahi kuonya katika kitabu chake cha
“Afrika inakwenda Kombo” kuhusu athari za kuwasikiliza wale wale
waliokuwa chanzo cha kukandamizwa kwetu.
Akasema Wazungu waliokuwa ndio chanzo kwa Afrika kukwama au
kujikanyaga kanyaga pasipo kusonga mbele hawawezi kugeuka na kuwa
washauri wake. Akaonya kwamba maendeleo ya viwanda na kilimo,
yote ambayo ni muhimu kabisa kwa wana Afrika, yalikuwa
yameandamwa na vikwazo kadhaa baadhi yake vikiwa ni kuwasikiliza
wale wale waliokuwa chanzo cha umaskini wetu au kutishwa na kauli
zao.
Profesa Dumont akabainisha pia kuwa kwa nchi za Afrika, nguo za
pamba ni mojawapo ya vitu vinavyoagizwa kwa wingi zaidi kutoka nje,
ingawaje vilikuwa ni moja ya bidhaa zinazoweza kutengenezwa barani
Afrika tena kwa urahisi sana.
Kwa maana hiyo dhamira ya viongozi wa Rwanda, Uganda na Tanzania
kuachana na mitumba na badala yake kujenga viwanda vya nguo
inapaswa kuungwa mkono, kwani mbali ya kuzalisha mavazi, pia
inapanua ajira kwa wakulima mashambani pamoja na wafanyakazi
viwandani na hivyo kuondoa umaskini.
Sullivan, ni kielekezo cha wakala wa ukoloni unaorudi Afrika baada ya
miaka 50 ya uhuru wa bendera kwa mlango wa nyuma. Watanzania na
wana wa Afrika Mashariki kaeni chonjo.
Mwandishi wa makala hii ni msomaji mahiri wa JAMHURI.
Anapatikana kupitia simu 0754 321308