Wiki hii Tanzania inamkumbuka mwasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere. Tukio hili ni la kila mwaka lakini mwaka huu linafanyika ikiwa imepita miaka 20 tangu kufariki dunia kwa kiongozi huyo ambaye ndiye aliyeweka misingi ya jinsi ya kutawala na kuongoza nchi ili kujiletea maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kimsingi, Taifa la Tanzania lilivyo leo limetokana na mambo mengi, lakini juhudi za Mwalimu Nyerere wakati wa uongozi wake zina nafasi kubwa katika mambo hayo.
Kutokana na umahiri wake katika uongozi, Mwalimu anabakia kama kigezo linapokuja suala la kupima umahiri wa viongozi au hata sera ambazo zinatumika kutuongoza kuelekea katika maendeleo hayo.
Sote tunakiri kuwa Mwalimu alikuwa kiongozi wa kipekee. Na hili halionekani miongoni mwa Watanzania pekee, kwani hata viongozi wa nje ambao walimfahamu Mwalimu walipata kumsifia kwa jinsi alivyokuwa mahiri katika uongozi.
Kinachotia moyo ni kuwa hadi hii leo bado Watanzania wengi, hasa viongozi, wanapenda kujinasibisha na Mwalimu. Ingawa wapo wanaofanya hivyo kinafiki, lakini kwa kiasi kikubwa viongozi wakuu wa nchi wamekuwa wakibainisha jinsi ambavyo maono na miongozo ya Mwalimu yanavyosaidia katika uongozi wa nchi.
Lakini kujinasibisha na Mwalimu ni jambo rahisi kulifanya kwa sababu unaweza kulifanya kwa maneno tu. Kubwa ambalo wengi tungependa kuliona ni jinsi viongozi wanaojisifia kwa kumuenzi Mwalimu wakifanya hivyo kwa vitendo.
Vitendo hivyo vinapaswa kutoa mwelekeo wa nchi na kuzaa Tanzania ambayo Mwalimu aliiona ndotoni mwake.
Hilo litaonekana pia kupitia misingi ambayo viongozi wa sasa wataijenga na kuisimamia wakati wanashiriki katika kazi ya kujenga nchi. Kwa wanaomfahamu Mwalimu wanaifahamu misingi hiyo kuwa ni kujenga jamii yenye usawa, inayojitegemea na ambayo inaheshimu utu wa kila mtu.
Viongozi karibu wote waliofuata baada ya Mwalimu wanajinasibu kuwa wamekuwa wakiyafanya haya.
Umefika wakati sasa wa kuyapima mambo haya ili kuona iwapo kama ni kweli viongozi wetu wametusaidia kuijenga nchi ambayo bado inafuata misingi hiyo iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere.
Kwa kuwa bado tunakubaliana kimsingi kuwa misingi hiyo ni muhimu na inaweza kutufikisha pale tunapokusudia kufika kama taifa, umefika wakati sasa wa kujipima, hasa wakati huu tunapoadhimisha miaka 20 baada ya Mwalimu kufariki dunia. Huu ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ya kuona iwapo tunachokifanya bado kinatuweka katika mstari ule ule ambao Mwalimu angependa Tanzania ipitie katika ujenzi wa nchi inayozingatia misingi aliyoiasisi.