url-2Wapo ambao hadi leo hawajamwelewa Rais Dk. John Magufuli, na staili yake ya uongozi.

Wamekuwa hawamwelewi kwa sababu ya mazoea. Hakuna dalili ya kumwelewa haraka leo au kesho! Lililo la muhimu ni kwamba muda utafika tu – watamwelewa.

Baada ya uteuzi wa nafasi mbalimbali alioufanya, walau sasa tunaweza kujitokeza kutoa mawazo yetu bila kushambuliwa. Kabla ya hapo ilikuwa wazo lolote la kumuunga mkono, aliyelitoa alionekana anafanya hivyo ili atazamwe kwenye uteuzi! 

Tumeshawapata ma-RC, ma-DC, ma-DED na ma-DAS. Ameleta damu changa yenye mawazo mapya. Hilo ni jambo jema.

Walau sasa tunaweza kusema, ingawa tena kwa wakosoaji, hasa walioonekana kuwa karibu, wanaweza kusingiziwa kuwa wanakosoa kwa sababu wameukosa huo uteuzi! Raha ya binadamu ni kuwa wana uwezo wa kupindisha maneno ili yaendane na malengo au nadharia zao.

Yapo mambo mengi ambayo nilipenda niyajadili, lakini kwa umuhimu wake ni vizuri yakawa na siku zake maalumu. Lakini itoshe kusema Rais Magufuli, na wasaidizi wake wanapaswa kung’amua staili inayotumiwa na baadhi ya wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani. Staili inayotumiwa na Tundu Lissu, sidhani kama wasomi ndani ya CCM wameshindwa kuing’amua! Miaka ya 1990 staili inayofanana na hiyo ilitumiwa na Augustino Mrema, lakini ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, aliyeitoa usingizini CCM na vyombo vya dola kwa kuwaeleza kuwa kumwandama Mrema na wafuasi wake kulikuwa hakuna tija kwa watawala wa wakati huo. Mwalimu hakuona kosa la Mrema kubebwa na wafuasi wake, hata polisi wakafikia hatua ya kuwatawanya kwa mabomu ya machozi. Walipomsikia Mwalimu, wakamwacha Mrema aendelee kubebwa. Zamu hii mabomu ya machozi hayakuwapo, kwa hiyo polepole ule umaarufu uliovunwa kwa kutumia hayo mabomu, ukapoungua na kutoweka. Public Sympathy ikawa haipo tena!

CCM na Polisi wa wakati huo sidhani kama wote wameshafariki dunia! Au sihani kama wamebadilika kabisa kiasi cha kushindwa kung’amua hiki kinachofanywa sasa kwa Lissu. Binafsi, sijaona hatari kubwa ya kiusalama inayoletwa na Lissu kwa kauli zake. San asana polisi kwa kumkamata wanampa umaarufu! Gharama kubwa inatumika kumkamata na kumsafirisha kwa misururu ya magari na zana za kivita! Polisi wanataabishwa kwa jambo ambalo ni la kawaida mno. Mahakama inakalizwa hadi usiku kwa jambo ambalo lilipaswa limalizwe bila hata kuwapo kamera za waandishi wa habari! 

Nadhani Lissu na wanasiasa wa aina yake wanapaswa wakamatwe kwa kauli ambazo kwa kweli mtu mweledi akizisikia, atakubaliana na vyombo vya dola kuwa zinahatarisha usalama wa nchi. Hizi ngonjera na mipasho ya jukwaani visipochukuliwa na CCM na dola kuwa ni mambo ya kawaida, Lissu atawasumbua vichwa kweli kweli, na kwa njia hiyo atajengwa kisiasa kwa kiwango cha juu mno. Kwenye mfumo wa siasa za ushindani, watawala sharti wawe na ngozi ngumu. Rais akisema tu kidogo, polisi wakakimbilia kukamata na kushitaki, sijui hiyo bajeti ya polisi na magereza kama vitahimilika! Lissu ana akili. Anajua anachofanya. Polisi wasipong’amua, atawasumbua, si wao tu, bali CCM na Serikali nzima.

Nikiweka kando hilo, Rais Magufuli, ametangaza uamuzi wa maana mno. Nao si mwingine, isipokuwa ule wa Serikali kuhamia Dodoma. 

Wapo wanaokosoa uamuzi huu ambao kimsingi si uamuzi wake, bali ni wa waasisi wa Taifa letu. Ni uamuzi uliotolewa wakati ambao Magufuli, akiwa bado ‘mtoto wa shule’.

Wapo walioanza kumkosoa, lakini wanashindwa kutambua kuwa anachokifanya sasa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama chake inayoamini kuhamia Dodoma ni jambo la msingi. Ilani hiyo hiyo ndiyo iliyompa ushindi, na kwa sababu hiyo hana hiari katika kuitekeleza.

Wanaopinga uamuzi huu wanapaswa warejee kujua sababu zilizowafanya wazee wetu kuamua kuchukua hatua hiyo. Bila shaka wazee wetu walikuwa na sababu za kufanya hivyo, na sidhani kama sababhu hizo zimeshatoweka. Vyovyote iwavyo, uamuzi wa kuhamia Dodoma ni uamuzi sahihi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Waswahili husema huwezi kuweka mayai yote kwenye kapu moja! Hatari ya kuweka mayai yote kwenye kapu moja ni kwamba siku likianguka, hasara yake itakuwa kubwa. 

Pamoja na sababu za kiusalama, kuhamia Dodoma kuna manufaa makubwa kiuchumi. Wanaosema Serikali isikurupuke kuhamia Dodoma, wanapaswa kutambua kuwa kama nchi, sharti tuwe na mahali pa kuanzia. Mtu aliyejenga nyumba, hasa kwa kutumia fedha halali, anajua huwezi ni vigumu kupata fedha za mkupuo za kuanza ujenzi hadi kukamilisha. Akisubiri apate Sh milioni 50 ndipo aaanze kujenga, haitashangaza kuona akiishia kwenye njiani. Ujenzi wa nyumba huanza leo kwa kuanza na sehemu ndogo. 

Vivyo hivyo, mwanaume anayesubiri ajenge nyum.

ba, anunue samani, anunue gari, akamilishe kila kinachotakiwa ndipo aamue kuoa, anaweza kujikuta akiuvuka ujana bila kukamilisha hivyo vitu. Kilicho cha maana ni kuamua kuoa, na kwa pamoja wanandoa wanaweza kupanga kujenga, kununua samani na vitu vingine kadri ya juhudi zao.

Haya hayana tofauti na kuhamia Dodoma. Kama nchi, itakuwa vigumu kukamilisha mahitaji yote kwa asilimia 100 ndipo tuweze kuhamia huko. Tunapaswa kwenda sasa ili hayo mengine yatekelezwe tukiwa tayari katika mji huo.

Pamoja na kuunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli, na wasaidizi wake wakuu, naomba kutoa angalizo. Nalo ni la kuhakikisha Dodoma haigeuzwi na kuwa ‘zizi’ badala ya ‘jiji’. Makao Makuu ya nchi yanapaswa kuwa katika mpangilio mzuri wenye kuvutia wenyeji na wageni.

Litakuwa jambo la fedheha kweli kweli kuiona Manzese au Kwa Mtogole za Dar es Salaam zikihamishiwa Dodoma! 

Hatari ya Dodoma kuwa mji mbaya pengine kuliko Dar es Salaam zimeanza kuonekana. Yale maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya huduma mbalimbali yameshavamiwa na kujengwa nyumba kwa namna isiyovutia. Mitaa haijulikani.

Dodoma itavurugwa kama mamlaka husika zitanyamaza na kuwaacha wananchi wanunue na hatimaye wajenge kiholela. Mamlaka zinazohusika zinapaswa zipige marufuku ujenzi wowote ambao haupo kwenye ramani za mpango miji.

Hilo litawezekana endapo Serikali itatwaa maeneo yote ya mashamba yanayokusudiwa kuwekwa mji; na kwa kwa kasi ya aina yake yapimwe viwanja.

Lakini si hivyo tu, bali kutolewe maelekezo ya namna ya ujenzi, kwa maana kwamba kama eneo fulani ni kwa ajili ya ujenzi wa ghorofa tano, basi iwe hivyo. Kama eneo fulani linapendekezwa liwe la nyumba za kawaida, basi iwe hivyo. Yatakuwa machukizo kama eneo linalopaswa kujengwa nyumba za kawaida, watajitokeza wenye fedha na kujenga ghorofa 10 au zaidi! Miji ya wenzetu huko ughaibuni inajengwa kwa staili hiyo na kuifanya ivutie machoni kweli kweli.

Rais Magufuli huwa hashindwi jambo alilokusudia kulifanya. Bila shaka atatumia mamlaka aliyonayo kuhakikisha kuwa Dodoma inajengwa vilivyo. Hilo litawezekana akianza sasa kwa kuhakikisha wote waliojitwalia au kumilikishwa maeneo ya wazi na ya shughuli nyingine, wanayarejesha kwenye mamlaka husika, sasa.

Wapo wanaomshutumu Rais Magufuli, kwa staili yake ya uongozi, lakini historia ndio mwamuzi sahihi. Kuwatoa watu kwenye mazoea na kuwaweka katika njia nyingine ni kazi ngumu mno.

Hili la kuhamia Dodoma ni miongoni mwa mambo mazito ambayo hatuna budi kuungana kama nchi kuona linafanikiwa. Mamlaka zinazohusika zimsaidie Rais ili Dodoma iwe ‘jiji’ la kweli badala ya ‘zizi’ lenye mkusanyiko wa watu usiokuwa kwenye mpangilio.