Leo natafakari maana isiyo rasmi ya uzungu; maana ambayo hutumika sana kwenye matumizi ya kila siku ya lugha ya Kiswahili.
Ni uzungu kama sifa ya kubainisha tabia nzuri ya binadamu miongoni mwa jamii. Siku kadhaa zilizopita, nilisimamisha gari pembeni mwa barabara nikaambiwa nina ahadi ya kizungu kwa sababu jana yake niliahidi kurudi sehemu hiyo hiyo kesho yake asubuhi na nikatimiza ahadi yangu. Wasio Wazungu hawatarajiwi kutoa ahadi na wakazitimiza.
Wezi, wabadhirifu, na mafisadi wapo katika kile pembe ya dunia na kwa sababu ya kutapakaa kwao kila mahali na kwa kushirikiana kwao ndio inawezekana kwa mabilioni ya pesa kuhamishwa kutoka Bara la Afrika na kupelekwa nchi hizo ambazo tunaweza kuziita za “kizungu”, nchi zilizoendelea.
Inakadiriwa kuwa dola zaidi ya bilioni 60 za Marekani zinahamishwa kutoka Afrika kila mwaka. Lakini tunaposikia vinara wa ufujaji na kutorosha pesa za Afrika kwenda nje ya bara hili, mara nyingi hutajwa wasio Wazungu na ni nadra kusikia ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa hao wanaoonekana kuwa vinara wa mienendo mizuri.
Uzungu una sifa nyingi zisizo rasmi. Uzunguni haiwi tu sehemu ambayo ni makazi yaliyokaliwa na Wazungu kabla ya Uhuru, bali, inakuwa sasa ni sehemu ambayo zipo nyumba bora na zenye kupendeza. Potelea mbali kuwa huko uzunguni kwa leo wasio Wazungu ni wengi kuliko Wazungu. Kule kwingine kwenye duni na ambazo hazifanani za zile za uzunguni, tunakuita uswahilini.
Kwetu sisi, mswahili ndio sura ya pili ya sarafu ambayo upande mmoja ina mzungu. Kwa wengine labda kuna Mhindi, au Mwafrika, au jamii nyingine yoyote ambayo inaonekana duni zaidi kwa mila, desturi, na tamaduni zake, na hata kwa hali ya maendeleo kwa ujumla.
Mawazo haya, kwamba yote ya Wazungu ni mazuri, na kwamba yote yasiyo ya Wazungu ni mabaya, ni matokeo ya kufanikiwa kwa muda mrefu kwa uwepo wa kile mwimbaji Bob Marley aliimba kwenye wimbo wake, Redemption Song. Ni maneno aliyoazima kutoka kwenye hotuba ya Marcus Garvey, mmoja wa watetezi wakuu wa uhuru na haki za watu wenye asili ya Bara la Afrika.
Mawazo yanarithishwa kutoka rika moja kwenda jingine, kwa hiyo ni aina ya utumwa ambao si rahisi kuumaliza. Mizizi yake imeimarika ndani ya karne za utumwa na ukoloni, vyote ambavyo vilisimika na kustawisha hoja kuwa Mzungu na tamaduni zake ni bora kuliko binadamu wengine na tamaduni zao.
Dalili za mtu kubaki chini ya utumwa wa kikoloni ni pamoja na kutopenda au kushindwa kutumia lugha ya asili na badala yake kutumia lugha iliyoachwa na wakoloni, au kuchanganya lugha ya asili pamoja na kuazima bila haya maneno ya lugha iliyoachwa na wakoloni.
Dalili nyingine ya utumwa huu ni kuonea aibu majina yetu ya asili. Kuna siku nilituma pesa kwa mtu ninayemfahamu kwa njia ya M-Pesa, lakini ujumbe uliothibitisha muamala ulitoa jina ambalo sikulitambua. Nilipomuuliza alithibitisha ni jina lake. Nilipomuuliza sababu ya kutotumia jina zuri kama hilo, akasema halipendi. Jina lake ni Bhoke.
Mavazi nayo, yanaweza kuashiria utumwa wa mawazo, ingawa hili ni suala litakalowahusu zaidi wale wenye uwezo wa kuchagua aina ya nguo za kuvaa. Kwa wanaume, unafunga tai, kuanzia Januari mosi, hadi Desemba 31 au zipo siku unavaa shati la kitenge na batiki? Kwamba kuvaa suti na tai kuanzia Januari hadi Desemba haithibitishwi kuathiriwa na utumwa wa kikoloni, lakini ni ishara nzuri kuwa kuna kuathirika.
Kwa kutaja kuwa kutimiza ahadi ni sifa ya kizungu; jamii, pengine bila kujua, inaweka msimamo kuwa katika uhusiano rasmi na usio rasmi asiye Mzungu haaminiki hata kidogo. Kama wapo majirani zetu ambao hawatuamini kwa ahadi tunazotoa, sidhani kama ni suala ambalo linapaswa kutukosesha usingizi. Lakini kama kuna asilimia 90 ya viongozi wa Tanzania ambao wanaamini kuwa Mzungu anaaminika zaidi kuliko asiye Mzungu, basi tatizo linageuka kuwa janga.
Utumwa na ukoloni umefanya kazi nzuri sana ya kutawala mawazo yetu kiasi kwamba hata rangi ya ngozi yetu hatuipendi, na baadhi ya wanawake, na hata wanaume, wanatumia dawa za kupunguza weusi wa ngozi ili wafanane na Wazungu.
Siyo yote ya Wazungu ni mazuri, kama ilivyo juu ya wale wasio Wazungu. Na siyo yote ya Wazungu ni mabaya, kama ilivyo kwa wale wasio Wazungu. Tatizo ni kuweka na kuyapima matendo ya wanajamii kwa kutumia makundi ya Wazungu na wengineo na tukiamini kuwa kigezo kilichopitishwa na TBS ni uzungu.
Nimewahi kusoma nukuu moja ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda iliyosema kuwa kujali muda ni dhana ya kizungu. Kwa bahati mbaya sikuweza kupata ufafanuzi wa chimbuko la nukuu hii na wala kubaini alitamka katika mazingira yepi. Lakini maana ambayo hakuitaja ni kuwa si dhana ambayo inaweza kuwa sahihi kwa wale wasio Wazungu. Kwa maana moja nakubaliana naye. Sehemu kubwa ya jamii zetu ni wakulima na wao hupanga mipango yao kwa kufuata misimu: msimu wa kuandaa mashamba, msimu wa kupanda, msimu wa kupalilia, na msimu wa kuvuna. Katika kutekeleza yote haya, hawapangi kwamba wataenda shambani saa 12:35:51 asubuhi, na kutoka saa 5:39:34 asubuhi. Katika jamii kama hii, muda kamili siyo muhimu sana.
Kwa upande mwingine, kwenye uwanja wa ndege ambako zinatua na kupaa ndege kila wakati, suala la muda ni muhimu ili kuepusha ajali.
Kimsingi, katika suala la muda, shughuli kuu za jamii na maendeleo ya kiteknolojia ndiyo yanapanga iwapo vipaumbele vya wanajamii vitakuwa dakika au msimu. Nilivyomwelewa Rais Museveni ni kuwa tunatumia vigezo vya waongoza ndege kupima utendaji wa jamii ambayo inazingatia misimu. Hoja yangu siyo kuwa tubaki watu wa misimu tu, ila nazungumzia hali ilivyo.
Yapo mengi ya kujifunza na kuiga kutoka kwa jamii nyingine, lakini ni muhimu kufungua macho na mawazo yetu ili tuyaone yanayofaa ndani ya jamii zetu na kuacha kuendelea kutukuza tu ya wengine.