Waasisi wa taifa la Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, mwaka huu watafanyiwa kumbukumbu mbili tofauti; lakini zote zikiwa na umuhimu mkubwa.

Kumbukumbu hizi zitafanyika kwa kufuatana; Aprili mwaka huu, ambapo kwa Sheikh Karume itakuwa ni kumbukizi ya kutimiza miaka 50 tangu alipouawa, huku Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere atafanyiwa kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwake.

Sheikh Karume aliuawa kwa kupigwa risasi jioni ya Ijumaa, Aprili 7, 1972 katika Ofisi za ASP, Kisiwandui, Zanzibar wakati kumbukumbu zinaonyesha kwamba Mwalimu Nyerere alizaliwa Alhamisi ya Aprili 13, 1922 Butiama mkoani Mara.

Wazee hawa watakumbukwa kwa mengi na vizazi vyote vya Tanzania, kwa kuwa ni wao ndio waliopambana kuondoa utawala wa kikoloni na kisultani katika mataifa ya Tanganyika na Zanzibar, hivyo kutupatia Uhuru.

Ni wazee hawa kwa kushirikiana na wengine ambao wengi kama si wote tayari wamekwisha kutangulia mbele ya haki, walifanya uamuzi wa kuyaunganisha mataifa haya huru na kuzaa nchi mpya duniani inayofahamika leo kwa jina la Tanzania.

Ni uongozi na misimamo yao thabiti ambayo imeacha urithi wa amani, upendo, mshikamano na udugu miongoni mwa Watanzania takriban milioni 60 tuliopo sasa nchini, tukifurahia matunda ya Uhuru na Mapinduzi kwa namna mbalimbali.

Kwa maana hiyo, Aprili mwaka huu inapaswa kuchukuliwa na kuenziwa kwa namna ya kipekee kwa kukumbuka miongozo, michango, hekima na mengine mengi yaliyotendwa na Sheikh Karume na Mwalimu Nyerere.

Huenda kuna wanaoamini kuwa wazee hawa wameenziwa kiasi cha kutosha, lakini kwa uhakika kwa namna walivyojitoa kwa taifa hili, wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi; ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoto na wajukuu wa Tanzania wanaelewa falsafa zao na nia yao katika kuleta maendeleo ya Tanzania.

Kulinda na kuuheshimu Muungano ni moja kati ya ahadi zinazotajwa kila siku na viongozi waliopita, wa sasa na hata wajao wa Tanzania, lakini sisi tunaamini kuwa Muungano unapaswa kuboreshwa zaidi kama sehemu ya kuwaenzi wazee hawa wawili.

Miaka 100 ya kuzaliwa ya Mwalimu Nyerere na 50 ya kifo cha Sheikh Karume iwe chachu ya kuondoa madoa yote yaliyopo miongoni mwa Watanzania. Itumike kama chachu ya kujenga madaraja miongoni mwa jamii ya Kitanzania na iwe chachu ya kudumisha mshikamano wetu.

Mungu awalaze mahala pema peponi Sheikh Karume na Mwalimu Nyerere. AMINA.