Nimewahi kuandika kwenye safu hii kuhusu hitilafu ambazo nimeziona kwenye Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015. Zipo taarifa kuwa sheria hii sasa itaanza kutumika Septemba mosi, mwaka huu. Kama unayo hofu niliyonayo mimi utakubaliana nami kuwa wapo watu wengi wataathirika na sheria hii pamoja na kuwapo kwa taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari na majadiliano mbalimbali kuhusu sheria yenyewe na athari zake.
Kwanza, kuna kundi kubwa la watu ambao wanaendelea kutumia simu na mitandao ya kompyuta kwa namna ambayo itawaweka hatiani kwa mujibu wa sheria hii. Ni kama vile hawajui kama watakuwa wanafanya makosa chini ya sheria hii au hawajali kama yale wanayofanya yanaweza kuwatia hatiani.
Matumizi haya tumeyashuhudia kwa muda mrefu, lakini sasa hivi kuna kichocheo cha ziada. Jipya lililotokea tangu Rais Jakaya Kikwete kuweka sahihi kwenye muswada wa sheria hii ni kuwa Mheshimiwa Edward Lowassa amehama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na amejiunga Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na hatimaye kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kitendo hiki siyo tu kimeongeza uhasama wa kisiasa baina ya wafuasi wa CCM na wale wa vyama vinavyounda UKAWA, bali pia kumeongeza wimbi la viongozi na wafuasi wa pande zote mbili ambao wameendelea kutoleana maneno ya ushabiki kuunga mkono upande wao na kuuponda upinzani.
Ingekuwa ni ushabiki ule wa kawaida tu wa vikundi vya ngoma ya asili usingekuwa na madhara sana kwa washabiki hawa wa siasa. Tatizo la ushabiki wa kisiasa tunaoshuhudia sasa ni watu na makundi kuvuka hatua ya kupenda upande wao na kufikia hatua ya kuchukia kwa dhati wapinzani wao. Na hizo chuki zinapenya kwenye taarifa na majibizano yanayoonekana kwenye mitandao ya simu na mawasiliano kupitia kompyuta.
Hata bila kuwapo kwa sheria hii tumeona ongezeko kubwa la matusi, kejeli, vijembe, na kila aina ya maneno na picha ambazo haziwezi kuitwa za staha kwa mujibu wa kanuni zozote utakazobuni. Ukweli ni kuwa kwa baadhi ya matusi ambayo yanarushwa hewani haihitaji hata kuwapo kwa Sheria ya Mtandao kuweza kuwatia hatiani baadhi ya watu wanaotumia simu na kompyuta.
Nimewahi kufanya utafiti usiyo rasmi kwenye mtandao wa jamii kwa kuuliza umri wa wale ambao walikuwa kwenye jukwaa mojawapo la majadiliano kwa wakati ule. Wengi waliojibu walikuwa watoto ambao wastani wa umri wao ulikuwa miaka 15. Baadhi ya maandiko ambayo yanaonekana kwenye ujumbe wa maandishi kwenye simu na kwenye mitandao ya jamii yanaashiria kuwa watumiaji wengi ni vijana au watoto ambao hawafahamu athari za kisheria za wanayotenda.
Lakini wapo watu wazima ambao katika matumizi yao ya mitandao, unaweza kuwapima kwenye mizani ile ile inayotumika kwa watoto ambao bado wanajifunza tofauti ya baya na zuri. Hakuna sababu yoyote ya msingi ya kumtukana mtu matusi ya nguoni kwa sababu tu haungi mkono CCM au haungi mkono UKAWA. Hii sheria ina hitilafu nyingi, lakini kama zipo sehemu kwenye sheria ambazo naziafiki ni pamoja na kipengele kinachomtia hatiani mtu anayetumia mtandao kutukana watu wengine.
Lakini hata kwa wale wanaofahamu athari za matumizi ya mtandao yanayokatazwa na sheria hii wanaweza kujikuta wameingia mtegoni kwa sababu joto na ushindani wa siasa umepanda sana kiasi ambacho kuna watu ambao, katika hamasa ya kuzitetea hoja zao, wataandika yasiyopaswa kuandikwa.
Wapo wale ambao inaelekea wamepitia kwa kina maudhui ya sheria hii mpya na wamebaini athari za kuanika kila wazo linaloibuka kichwani. Matokeo yake ni kuwapo kwa kundi la watu ambalo limejiwekea mipaka ya uhuru wa kutoa mawazo. Nimeanza kushuhudia watu ambao zamani walikuwa wanaandika kwa uhuru mawazo yao, lakini siku hizi wamekuwa wanayatoa mawazo hayo kwa mafumbo kiasi kwamba wakati mwingine msomaji hawezi kubaini kwa urahisi ujumbe ambao mwandishi anataka kuufikisha kwa jamii.
Sina shaka kama ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) itafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria hii, na iwapo baadhi ya watumiaji simu na mitandao ya kompyuta hawatabadilisha matumizi yao ya simu na mitandao, basi kuna watu wengi watahamia gerezani kutumikia vifungo kwa makosa ya matumizi ya mitandao.
Kwa upande wa Serikali, ijiandae kujenga magereza kupokea ongezeko hili la wafungwa, au ijiandae kutoa misamaha kwa wafungwa waliomo gerezani ili kupisha kundi la watu ambao watafanya makosa bila kutambua au watafanya makosa bila kujali yatakayowakuta.