Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
 
Wiki iliyopita nimeandika kuhusu mfumo wa utozaji kodi. Nimeeleza utitiri wa kodi na utaratibu unaotumika kuzitoza, ambapo wengi wa wanaotoza kodi hawajawahi kufanya hata biashara ya kuuza kuku, hivyo kufahamu ugumu wa kulipa huo mkululo wa kodi uliowekwa. Nimezungumzia Kodi ya Huduma, ambayo watu wanadaiwa asilimia 0.3 ya mapato ghafi.

Sitanii, wengi wamenipigia simu wakisema kodi hii inawaua. Kimsingi kodi hii ya huduma (service levy), ilipaswa kuwa asilimia 0.03 ya mauzo ghafi. Haijulikani kosa lilitokea wapi, hadi hivi tunavyozungumza likiwamo Jiji la Dar es Salaam, wafanyabiashara wanadaiwa asilimia 0.3 ya mauzo ghafi, ambayo ni asilimia 30 ya mtaji wote na faida. Hii inaua biashara. Irekebishwe.

Nimeangalia mifumo ya kodi katika nchi mbalimbali. Nigusie mfano wa Uingereza. Nimepata fursa ya kuishi Uingereza. Hii ni moja ya nchi inayotoza kodi kwa uangalifu, lakini inawafahamu watu wake. Maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu yana maana yake. Mchungaji mwema huwajua kondoo wake na kondoo huijua sauti yake. Bahati mbaya baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni wachungaji wa mshahara.

Wakati ninasoma Uingereza nilishuhudia na hadi sasa hali hii inaendelea kuwa kuna masoko yanayoitwa ‘Sunday Market’. Masoko haya yapo mara mbili kwa wiki; Jumatano na Jumapili. Hawa tunaowaita wamachinga kwetu au sawa na minada inayozunguka sehemu moja hadi nyingine, ‘Sunday Market’ ndiyo siku yao ya kuuza. Haukuti mtoza ushuru kwenye ‘Mnada’ wa Jumatano na Jumapili (Sunday Market). Hapa kwetu vipi?

Wanafanya makusudi, wamachinga wao wadogo wapate kuuza na kupata fedha za kujikimu. Ndiyo, katika kujikimu wachache watapenya na kuwa matajiri, lakini kwa Uingereza mtu kuwa tajiri si kero. Hapa kwetu kuna wasiowapenda matajiri. Ukimwachia machinga akapata utajiri kupitia kwenye minada, miaka michache baadaye huyu anaacha kukimbizana na minada anajenga kiwanda cha moja ya bidhaa anazouza minadani. Anahitimu, anazalisha matajiri wengine, analipa kodi.

Sitanii, dhana hii ndiyo nitakayotaka Tanzania tuiazime. Makala ya wiki iliyopita nimemwomba Rais Samia Suluhu Hassan aunde Kikosi Kazi cha Kodi kichunguze mambo mbalimbali kama alivyofanya kwenye Hali ya Siasa Nchini, Haki Jinai, Uviko – 19, Mambo ya Nje na kwingine. Kodi ni mfupa mgumu. Julai 1, 1996 hayati Rais Benjamin Mkapa alianzisha TRA. Sina uhakika tangu TRA imeanzishwa iwapo imewahi kufanyiwa mapitio makubwa kupima utendaji wake, ufanisi na sehemu zenye kuhitaji maboresho.

Mwezi uliopita nilikuwa Korea Kusini. Nilibaini utajiri walionao leo kama nchi haukuja kwa bahati mbaya. Kuna familia zinaitwa Chaebols. Mwaka 1963, Rais Park Chung Hee, aliamua kuzipatia mtaji familia 15 zifanye biashara. Familia hizi ndizo zinaitwa Chaebol. Familia hizi alikuwa anakutana nazo mara mbili hadi nne kwa mwezi zitoe taarifa juu ya maendeleo yao ya biashara. Matokeo yake, leo familia hizi ndizo zinashikilia asilimia 80 ya uchumi wa Korea wenye thamani ya dola trilioni 1.6.

Kampuni ya kwanza kwa ukubwa nchini Korea Kusini ni Samsung ambayo ina thamani ya dola bilioni 341.1, japo baadhi ya mitandao inaonyesha kuwa thamani yake ni dola bilioni 480.

Kampuni hii inamiliki jumla ya kampuni 60 zinazofanya biashara ndani na nje ya nchi hiyo. Inauza simu, radio, TV, inatengeneza magari na ina viwanda vinavyozalisha silaha za kivita, na kila bidhaa unayoiwaza, Samsung inaitengeneza.

Kampuni ya pili ni SK Group yenye mtaji wa dola bilioni 205.8. Kampuni hii inamiliki kampuni tanzu zaidi ya 200 ndani na nje ya nchi.

Mwaka 2021 ndipo imeshika nafasi ya pili kitaifa kwa uchumi mkubwa ikiiondoa Hyundai ambayo sasa inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa. Hii Hyundai ambao ni watengenezaji wakubwa wa magari, inatajwa kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa katika uzalishaji wa magari duniani baada ya Volkswagen ya Ujerumani.

Sitanii, nafasi imekuwa finyu. Je, unajua kwa nini Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete alianzisha mpango wa ‘Mabilioni ya Kikwete?’ Unafahamu kwa nini hayati Dk. John Pombe Magufuli alikuwa amesema anataka kujenga mabilionea 100? Unafahamu kwa nini Afrika Kusini walianzisha sera ya Kuwezesha Wazawa (Indigenization)? Narudia, safu hii imekuwa fupi. Tukutane wiki ijayo. Hatuwezi kuendelea bila serikali kujenga matajiri. Nitaeleza tufanye nini. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827