Kuna huu mgogoro wa Zanzibar. Mtu akiuangalia juu juu mgogoro huu atauona kwamba ni mwepesi na atashangaa kwa nini haumalizwi mara moja.
Wapo watu watakaokwenda mbali zaidi (na kwa kweli tayari wameshakwenda mbali zaidi), wanajiuliza kwa nini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, anashindwa kuumaliza mgogoro wa Zanzibar?
Hakuna mwenye lengo la kumdharau Dk Magufuli lakini tukitaka kusema ukweli (na ni lazima tuseme ukweli), Dk. Magufuli ni mtu wa kuhurumiwa. Ameingia wakati mbaya na hawezi kumaliza mgogoro huu wa Zanzibar kama tunavyotaka sisi.
Kwa ujumla mgogoro wa Zanzibar si mgogoro wa kisiasa kama unavyoonekana. Huu si mgogoro kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF). Huu ni mgogoro wa kihistoria kati ya Mwarabu na Mwafrika au mtu mweusi.
Zanzibar ina historia ndefu ya maisha ya wakazi wake ya chuki, ubaguzi na kudharauliana pia kutoaminiana. Na hii ni tangu enzi za biashara ya watumwa na utumwa wenyewe. Wakazi wa Zanzibar wanaishi kwa misingi ya ubaguzi, hata vyama vyao vya mwanzo vilianzishwa kwa misingi ya ubaguzi na makundi.
Mwaka 1900, Waarabu walianzisha chama chao, Arab Association, ambacho lengo lake lilikuwa kupigania maslahi ya Waarabu. Waarabu walidai fidia kwa Waingereza kwa kukomesha biashara ya watumwa.
Mwaka 1910, Wahindi walianzisha Indian Association yaani Chama cha Wahindi. Lengo lao lilikuwa kusimamia madeni yao yalipwe na Waarabu waliokuwa wamekopa fedha nyingi kutoka kwa Wahindi. Wakakataa kulipa madeni yao wakidai kwamba wao walikuwa watawala.
Wahindi wakaomba msaada wa Serikali ya kwao India, Serikali ya India ikaacha kununua karafuu za Zanzibar, Waarabu wakalipa madeni yao.
Mwaka 1934, Waafrika walianzisha chama chao African Association yaani Chama cha Waafrika. Chama hiki kilipigania maslahi ya Waafrika. Nao Washirazi wakaanzisha Shirazi Association mwaka 1938 ili kipiganie maslahi yao.
Basi, maisha ya watu wa Zanzibar yakatawaliwa na chuki, ubaguzi na utengano. Makundi hayo ya watu yakasusiana ibada za dini na hata mazishi.
Ukaja wakati wa vyama vya siasa. Navyo pia vilianzishwa kwa misingi ya ubaguzi na utengano. Mwaka 1955 kilianzishwa chama cha kwanza cha siasa Zanzibar cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoongozwa na Ali Muhsin. Lengo kuu la ZNP (au Hizbu kama ilivyojulikana) lilikuwa ni kudumisha utawala wa kisultani Zanzibar.
ZNP ilijitapa kuwa chama cha raia wa sultani. Huu ulikuwa wakati wa Seyyid Khalifa bin Haroub, Sultani wa 10 wa Zanzibar, aliyetawala kwa muda mrefu zaidi kuliko wote (miaka 50 kati ya 1911-1960).
Februari 5, 1957 Waafrika na Washirazi waliunganisha nguvu. Wakaanzisha Afro-Shirazi Party (ASP). Hapo yakaanza mapambano makali ya kisiasa kati ya Waarabu na Waafrika au watu weusi. Siasa zikaendeshwa kwa misingi ya chuki, ubaguzi na utengano.
Julai 1957 ulifanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa Baraza la Kutunga Sheria Zanzibar. Wakati huo ASP ilikuwa na umri wa miezi minne tu. Kwa hiyo, ilisita kushiriki uchaguzi huo. Iliamini kuwa ZNP ingeshinda uchaguzi huo kwa kishindo.
Aliyekuwa Rais wa TANU, Mwalimu Julius Nyerere, aliwatia moyo Waafrika wa Zanzibar. Aliwaambia kwamba ambacho kingewasaidia kushinda uchaguzi ule si umri wa chama bali ni hoja zao.
ASP ikaleta hoja nzito kwamba wakati ule ulikuwa wakati wa Waafrika kurejesha heshima yao na utu wao. Siku ya uchaguzi ilipofika, ASP ikanyakua viti vitano kati ya sita vilivyogombewa.
Mwaka 1959 kikaanzishwa Chama cha Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP), kiongozi wake akiwa Mohamed Shamte. ZPPP iliungana na ZNP katika kukikandamiza chama cha Waafrika cha ASP. Vyama hivi viwili vikazoea kupora ushindi wa ASP kwa kuunganisha viti kila mara ASP iliposhinda uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria. Hii iliendeleza chuki ya Waafrika dhidi ya Waarabu.
Hali hiyo iliendelea hadi Desemba 10, 1963 Zanzibar ilipopata Uhuru kutoka kwa Mwingereza, lakini ukweli ni kwamba waliokuwa wamepata uhuru ni Waarabu. Waafrika waliendelea kutawaliwa na Waarabu mpaka walipojikomboa kwa njia ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliyotawaliwa na umwagaji damu.
Sasa tujiulize, Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na lengo lipi? Kwa kifupi, lengo la Mapinduzi ya Zanzibar lilikuwa kuleta uhuru wa walio wengi, kurejesha heshima ya Mwafrika, na kuweka nchi na ardhi ya Zanzibar chini ya Waafrika.
Aprili 26, 1964 ukazaliwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao lengo lake kuu lilikuwa kuleta umoja kati ya nchi hizi mbili. Kiuchumi, watu wa Pemba wamenufaika zaidi na Muungano huu kuliko watu wa Bara. Huu ni ukweli usiopingika.
Ukaja uchaguzi wa Rais wa Zanzibar wa mwaka 2015. Inaaminiwa kuwa ni Maalim Seif Shariff Hamad ndiye aliyeshinda uchaguzi huo. Lakini ulifutwa. Hebu tujiulize swali la msingi, kwa nini uchaguzi huo ulifutwa? Tangu mwanzo nimesisitiza kwamba tujadili kwa kina mgogoro huu wa Zanzibar.
Uchaguzi haukufutwa eti kwa sababu CUF ilishinda. Uchaguzi ulifutwa kwa sababu aliyeshinda ni Maalim Seif. Haya si mapambano ya kisiasa ni mapambano ya kihistoria.
Kwa mambo mawili, Maalim Seif ajilaumu kwa kushindwa kuchunga ulimi wake na kauli zake. Kwanza, kwa muda mrefu Maalim Seif ameendelea kudai Muungano wa mkataba. Kama tujuavyo, mkataba wowote una mwisho wake. Hii imeleta picha kwamba Maalim Seif anataka kuvunja Muungano. Na amekuwa akisema kwamba hata Muungano ukivunjika Wapemba walioko Bara hawataathirika kwa kuwa watabaki Bara kama wawekezaji. Wapemba hawakwenda Bara kama wawekezaji na wala majina yao hayapo kwenye Kituo cha Uwekezaji (TIC). Walikwenda Bara kama raia wa Muungano. Muungano ukivunjika watalazimika kuomba uraia wa Tanganyika na kuna kukubaliwa au kukataliwa. Juu ya yote, Muungano umesaidia kudumisha amani Zanzibar maana bila ya Mungano Zanzibar inaweza kuwa na machafuko yasiyokwisha kama yale ya Rwanda na Burundi. Pili, wakati wa kampeni za uchaguzi, Maalim Seif alisikika akisema kwamba kama CUF ingeshinda uchaguzi ingerejesha kwa wenyewe ardhi iliyokuwa imetaifishwa baada ya Mapinduzi. Hii ni kusema kwamba Maalim Seif anataka kuwanyang’anya Waafrika ardhi waliyogawiwa baada ya Mapinduzi ili awarejeshee Waarabu.
Ni katika mazingira hayo, Waafrika wa Zanzibar wameendelea kusisitiza kwamba hawapo tayari kusaliti Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Kwa maneno mengine ni kusema kwamba Waafrika wa Zanzibar hawapo tayari kupoteza uhuru wao, ardhi yao na nchi yao. Hawatatoa nafasi tena kwa Waarabu kuwa na sauti katika masuala ya utawala wa Zanzibar.
Simkatishi tamaa Maalim Seif, lakini nazungumzia hali halisi. Katika mazingira hayo, wale wanaombebesha Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli, lawama na mzigo wa mgogoro wa Zanzibar hawamtendei haki. Hivi wanataka afanye nini?
Wanataka ahakikishe kwamba demokrasia inafanya kazi kwa kutoa nafasi kwa Maalim Seif kutawala Zanzibar, ili Muungano uvunjike na Waafrika wa Zanzibar wanyang’anywe ardhi yao?
Tusije tukasahau, Zanzibar ni nchi na watu wa Zanzibar hawataki mtu yeyote aingilie mambo yao. Kwa hiyo, mgogoro wa Zanzibar utamalizwa na watu wenyewe wa Zanzibar kwa heri au kwa shari. Ni kwa bahati mbaya lakini hivyo ndivyo hali halisi ilivyo. Nani anabisha?