Mzimu wa tuhuma za kudai na kupokea rushwa kutoka kwa wawekezaji mbalimbali Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro umezidi kumwandama Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai ole Sabaya.

Safari hii DC huyo anatajwa kudai na kupokea rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Cuthbert Swai ambaye ni mkurugenzi wa hoteli ya kitalii, Weruweru River Lodge.

Tuhuma hizi ni mwendelezo wa tuhuma ambazo zimekuwa zikitolewa na wawekezaji wilayani Hai wakidai kupewa vitisho mbalimbali na mkuu huyo wa wilaya vinavyoendana na matukio ya kuwekwa ndani kati ya saa 24 na 48, kisha kuachiwa huru bila kufunguliwa mashitaka.

Pamoja na mkuu huyo wa wilaya kupuuza tuhuma hizo, Swai ameanika mambo kadhaa juu ya unyanyasaji ambao amekuwa akifanyiwa na mkuu huyo wa wilaya, ikiwamo kuombwa rushwa ya kati ya Sh milioni tano na milioni mbili.

Mbali na kumpa rushwa, Swai amedai kuendelea kupewa vitisho zaidi ikiwamo kupewa saa 48 kuhamisha akaunti za Weruweru River Lodge kutoka Moshi mjini kwenda Wilaya ya Hai.

Swai ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwakala wa Utalii ya Ahsante Tours, ameanika tuhuma hizi mbele ya Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo, katika mkutano wa siku moja wa wafanyabiashara na TRA uliofanyika mjini Moshi Julai 22, mwaka huu.

Amesema kwa nyakati tofauti kati ya Novemba mwaka jana na Julai mwaka huu, mkuu huyo wa wilaya ameweza kupokea Sh milioni 10 kutoka kwake, fedha ambazo amezitoa kutokana na vitisho alivyokuwa akipewa na mkuu huyo wa wilaya.

Swai amesema baada ya kuamriwa kuhamisha akaunti za hoteli yake alifanya hivyo lakini pamoja na kuhamisha akaunti hizo na kuzipeleka Wilaya ya Hai aliendelea kupata misukosuko ya kuombwa rushwa ya Sh milioni tano lakini alimpa Sh milioni mbili.

“Mheshimiwa Sabaya mwaka jana mwezi wa 11 alinipa saa 48 kuhamisha akaunti zangu za Weruweru River Lodge na kuzipeleka Hai. Nilifanya hivyo lakini mpaka sasa sijui ni kwa nini. Wakati huo huo akawa anadai Hotel Levy (ushuru wa hoteli) ambayo yeye hajui kama ukiwa unalipa VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) hutakiwi kulipa Hotel Levy, unachotakiwa ni kulipa Service Levy (Ushuru wa Huduma). Mheshimiwa hicho kitendo hakukielewa, ilituchukua sisi wiki tatu nikihudhuria kuanzia asubuhi mpaka saa nane bila kujali kuhusu wateja wangu,” amedai mfanyabiashara huyo.

Desemba 3, mwaka jana, saa kumi jioni, Sabaya anadaiwa kuvamia hoteli hiyo akiwa na walinzi wake na kuanza kuhoji ulipaji wa kodi lakini kutokana na Meneja wa hoteli hiyo, Ibrahimu Kapilima, kutokuwa mhusika wa masuala ya kodi na kushindwa kutoa majibu stahiki, aliagiza akamatwe na kuswekwa ndani.

Swai amedai kuwa alifuatilia kwa mkuu huyo wa wilaya kutaka kujua kulikoni meneja wake kuswekwa ndani. Anadai mkuu huyo wa wilaya alimtaka Swai ampe rushwa ya Sh milioni tano na baada ya msuguano wa muda aliweza kumpa Sh milioni mbili.

Tukio jingine ambalo linadaiwa kufanywa na mkuu huyo wa wilaya ni la Julai 13, mwaka huu alipovamia hotelini hapo saa kumi alfajiri akiwa na walinzi wake akishinikiza kuonana na mmoja wa wageni waliokuwa wamefikia katika hoteli hiyo.

Hata hivyo, wafanyakazi wa hoteli hiyo walimgomea huku kipande cha video kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kinachodaiwa kurekodiwa kwenye kamera za usalama (CCTV Camera) za hoteli hiyo zikimuonyesha akijibizana na mhudumu wa hoteli hiyo.

Taarifa ambazo JAMHURI limepewa zinadai kuwa baada ya jaribio lake la kuonana na mgeni huyo kukwama, Sabaya aliondoka eneo hilo na kurejea tena asubuhi yake kwa lengo hilo hilo, lakini aligonga mwamba kwa mara nyingine.

“Tumetumia gharama kubwa sana kuhakikisha mgeni huyo tunampata na kulala kwenye hoteli yetu. Ni mtu maarufu sana hapa nchini, lakini siwezi kumtaja hapa. Ni star mkubwa sana, ana wafuasi zaidi ya 30,0000 kwenye mitandao ya kijamii,” amesema Swai.

Wakati hayo yakiendelea, Sabaya ameibua sakata la tuhuma za mfanyabiashara huyo kupora eneo la wananchi wa Kijiji cha Kimashuku lenye ukubwa wa ekari 14, lakini Swai ameonyesha nyaraka kuonyesha eneo hilo analimiliki kihalali.

Miongoni mwa nyaraka hizo ni stakabadhi ya malipo ya Sh 3,212,000 kutoka Kijiji cha Kimashuku kilichopo Kata ya Machame Kusini ikiwa ni malipo ya asilimia nane kwa ajili ya ununuzi wa shamba.

Sabaya akiongozana na wananchi wachache pamoja na maofisa kutoka ofisi yake, aliutangazia umma kuwa Swai amevamia eneo hilo na kutangaza kumpoka ardhi hiyo akidai ameipora kutoka kwa wananchi.

Swai amesisitiza eneo hilo ni mali yake halali na hakuna wa kumpoka ardhi hiyo na kuwataka wanaodai amevamia ardhi yao waende mahakamani ambako ndiko haki itatendeka na si Sabaya kutumia nguvu kupora eneo lake.

“Huyo bibi anayedai ni shamba lake si kweli. Shamba lake lipo ndani ya mita 30 kutoka Mto Kikavu na hata mwaka huu amelima mahindi, kwa hiyo hao wanaosema nimevamia mashamba yao si kweli. Mimi ninamiliki kihalali shamba hilo,” amesema.

Sabaya ameshindwa kujibu tuhuma za rushwa anazotuhumiwa na Swai, akidai hawezi kujibu “upuuzi”. Pia ameshindwa kujibu tuhuma za kumsweka ndani meneja wa hoteli hiyo pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu tukio la alfajiri ya Julai 13 ‘alipovamia’ hoteli hiyo mara mbili.

Nyaraka dhidi ya Sabaya

JAMHURI limezungumza kwa kina na Swai ambaye ameonyesha ushahidi wa nyaraka kupinga madai ya Sabaya kwamba amekuwa akiendesha shughuli za ufugaji wa wanyama wakiwamo nyoka bila kuwa na vibali kutoka mamlaka husika.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI linazo, Juni 11, mwaka jana Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, S. Kundya, alitoa kibali cha miezi sita kwa Weruweru River Lodge kufanya maonyesha ya ngoma za asili za kabila la Wasukuma na maonyesho ya nyoka kwenye hoteli hiyo.

“Kwa yeyote anayehusika, Yah: kibali cha kufanya maonyesho ya ngoma za asili za Kisukuma na maonyesho ya nyoka Kampuni ya Weruweru River Lodge kuanzia 11/6/2018 hadi 31/12/2018, saa nane mchana mpaka saa tatu usiku kwa siku za maonyesho,” kinasomeka kibali hicho.

Hata hivyo, wakati kibali hicho kikibakiza mwezi mmoja kwisha muda wake, Swai amelalamika kupewa vitisho na mkuu huyo wa wilaya na kulazimishwa kuandika barua ya kukiri kufuga nyoka bila kibali, agizo ambalo alilitekeleza Novemba 5, mwaka jana.

“Naomba kuihakikishia ofisi yako kuwa nyoka hawa walikuwa si mali yangu ni mali ya Bwana Maganga kutoka Wilaya ya Nzega ambaye kwa sasa ameshawachukua nyoka wake na kuwarudisha Nzega,” inasema sehemu ya barua ya Cuthbert Swai kwenda kwa DC Sabaya.

Pia JAMHURI limeona leseni ya biashara ya nyara iliyotolewa na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), kituo cha Arusha yenye namba 07064 iliyotolewa Januari 19, mwaka huu na itamaliza muda wake Desemba 31, mwaka huu ambayo imetolewa kwa Shamba la Kikavu na kulipiwa ada ya Sh 118,000.

Kamati Ulinzi na Usalama kumhoji

Sakati hilo limeendelea kupamba moto ambapo sasa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa, Dk. Anna Mghwira, ameweka wazi kuwa watamhoji mkuu huyo wa wilaya juu ya tuhuma hizo za rushwa ambazo amedai malalamiko yamekuwa mengi.

Amesema tuhuma zilizoanikwa na mfanyabiashara huyo zilitolewa kwenye kikao rasmi, hivyo lazima wazifanyie kazi ikiwamo kumhoji Sabaya na akaenda mbali zaidi akidai upo umuhimu wa kuitisha kikao cha pamoja na wafanyabiashara kuzungumzia changamoto zinazowakabili. 

Machi mwaka huu Rais Dk. John Magufuli aliwatuma Waziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshugulikia Uwekezaji, Angela Kairuki, kwenda Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro kusaka ukweli juu ya malalamiko ya wawekezaji waliodai kuwekwa ndani kwa saa 48 na Sabaya.

Mbali na kuwekwa ndani kwa saa 48 kwa amri ya Sabaya, wawekezaji hao pia walilalamikia vitendo vya kudaiwa rushwa au kuwekwa katika mazingira ya kudaiwa rushwa na mkuu huyo wa wilaya.

Kutumwa kwa mawaziri hao na Rais Magufuli kulitokana na wawekezaji hao kumwandikia rais barua ya malalamiko dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na mkuu huyo wa wilaya.

Waziri Mpango alizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusikiliza malalamiko ya wawekezaji hao na kusema moja ya matukio ya unyanyasaji huo ni mwekezaji katika shamba la kahawa la Kibo/Kikafu, Trevor Robert, ambaye ni raia wa Zimbabwe kuwekwa ndani kwa saa 48 pamoja na kupokwa hati yake ya kusafiria.

Pia alisema Mkurugenzi wa Kampuni ya Tudeley Tanzania iliyowekeza katika mashamba hayo, Jensen Natai, pamoja na wakili wa kampuni hiyo, Edward Mrosso nao waliwekwa ndani kwa saa 48 huku mwekezaji huyo akidaiwa kukwepa kodi na kutakiwa alipe kodi ya Sh milioni 713 ndani ya siku saba.

Kwa mujibu wa Waziri Mpango, mwekezaji huyo katika malalamiko yake kwa rais alidai mbali na kupokwa hati yake ya kusafiria, pia alidaiwa kuishi nchini pamoja na kufanya kazi isivyo halali.

“Wawekezaji hawa wamemwambia Mheshimiwa Rais kuwa mbali na kuzuiwa kuendelea na uwekezaji katika shamba la Kibo/Kikafu, wamedai kuchafuliwa majina yao kwa kuitwa wezi, matapeli na kuwa wameghushi namba ya utambulisho wa mlipa kodi,” amesema waziri.

Waziri Mpango aliyaweka malalamiko ya wawekezaji hao katika makundi sita, ikiwamo kudaiwa kukwepa kodi, akaunti zao kufungwa kwa maelekezo ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwekwa ndani kwa saa 48, kudaiwa rushwa ama kuwekwa katika mazingira yanayoashiria kudaiwa rushwa.

Kutokana na madai hayo, Waziri Mpango alisema wawekezaji hao walimweleza rais katika barua yao ya malalamiko kuwa mazingira ya uwekezaji nchini ni magumu na wanashindwa kuwashawishi wawekezaji wenzao kuja nchini kuwekeza.

Hata hivyo Waziri Mpango akawaambia waandishi wa habari kuwa lipo tatizo la mawasiliano kwa idara za serikali ambalo kwa namna moja ama niyngine huchangia migogoro kama hiyo kutopatiwa ufumbuzi wa haraka.

Akatoa rai kwa idara za serikali kuanzia ngazi za halmashauri, mkoa hadi wizarani kufanya kazi kwa ukaribu sambamba na kuwapo kwa mawasiliano ya karibu katika kutatua changamoto mbalimbali zikiwamo za wawekezaji.

 Sabaya alizungumza na JAMHURI na kukana tuhuma za kuwanyanyasa wawekezaji hao huku akidai baadhi yao ni wababaishaji kutokana na kile alichodai hawakuwa na mikataba ya uwekezaji katika shamba la kahawa la Kibo/Kikafu.

“Hao wawekezaji ni wababaishaji. Hawana mkataba wowote na vyama vinavyomiliki hayo mashamba, pia hawajawahi kulipa kodi kwa hivyo vijiji na wanataka mpaka wapewe mkataba, sasa hao unawafanyaje?” amehoji.

Amesema ili uwe mwekezaji lazima ufuate taratibu za uwekezaji na kusisitiza kuwa hao waliolalamika kwa rais wameondolewa hadhi ya kuwa wawekezaji kutokana na kutofuata taratibu stahiki.

Kuhusu mwekezaji huyo kupokwa hati yake ya kusafiria, mkuu huyo wa wilaya amesema walitilia shaka maelezo yake kwamba alikuja kuwekeza kwenye kampuni iitwayo Kilimanjaro Farm ambayo kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, kampuni hiyo haipo katika Wilaya ya Hai.

Kwa upande wake Waziri Kairuki amesema lengo la serikali ni kuona uwekezaji unaendelea kufanyika katika mazingira rafiki na endelevu kwa nia ya kuwavutia wawekezaji zaidi.

Akasisitiza lengo la kufika Kilimanjaro ni kutaka kufahamu kwa undani malalamiko ya wawekezaji hao, ikiwamo madai ya kufungwa kwa akaunti za mwekezaji, Kampuni ya KUZA AFRICA, kama mchakato huo ulifuata taratibu sahihi.

Hata hivyo Kairuki alisema kuwa changamoto waliyoiona katika uwekezaji wa Shamba la Kibo/Kikafu ni hatua ya mwekezaji wa awali Kampuni ya Tudeley kuamua kuingia mkataba na Kampuni ya KUZA AFRICA bila kuvishirikisha vyama vya msingi vya ushirika vinavyomiliki mashamba hayo.

“Tupo hapa kuona kama taratibu za uwekezaji zilifuatwa, pia kupata maoni ya vyama vya ushirika vinavyoendesha mashamba haya kama wanataka kuendelea na mwekezaji wa awali ama huyo mpya,” amesema.

Waziri Kairuki amesema wameweza kupata maoni ya viongozi wa wilaya na mkoa juu ya hali ya uwekezaji katika mashamba hayo, kama wanaamini masilahi ya taifa yanalindwa pamoja na msuala ya kodi kama yanatekelezwa ipasavyo.

Kampuni ya KUZA AFRICA ambayo ni kampuni ya Ujerumani imewekeza katika kilimo cha parachichi Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya na kwa hapa mkoani Kilimanjaro, kampuni hiyo imewekeza kwenye kilimo hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amesema changamoto za uwekezaji katika shamba hilo zitapatiwa ufumbuzi baada ya mwekezaji wa awali kujitokeza na kuweka wazi mkataba wake.

“Tumefikia mwafaka mzuri na tumekubaliana yule mwekezaji wa awali aje ili atupe fursa ya kusikilizana na kutoa nafasi uwekezaji uendelee kwa manufaa ya wananchi wa Kilimanjaro na taifa kwa ujumla,” amesema.