Mwanamuziki wa Hip-hop, Sean “Diddy” Combs kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa Serikali akisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za utapeli na utumwa wa ngono.
Kukamatwa kwake huko New York kulikuja huku kukiwa na msururu wa tuhuma za unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji wa kimwili, baadhi ya tuhuma hizo ni za tangu miaka ya 1990.
Zaidi ya watu kumi na mbili wamefungua kesi dhidi ya rapa huyo wakimtuhumu kutumia ushawishi wake katika tasnia ya burudani kwa kujishughulisha na dawa za kulevya, kuwashambulia na kuwabaka.
Orodha ya hivi punde ya mashtaka ni pamoja na madai ya unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa wanaume wawili ambao walikuwa chini ya umri wa miaka 18 wakati huo.
Wote wawili wanaeleza kuwa walikuwa na matumaini kwamba Combs angeweza kuwasaidia kukuza vipaji vyao katika tasnia ya burudani.
Rapa huyo mzaliwa wa Harlem amekanusha mashtaka yote.