Kumbukumbu zinanionesha sasa kuwa Watanzania wengi wanaamini kuwa suala la Katiba Mpya haliwezekani tena chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Ametafuta pa kutokea na kuamua kuelewana na wapinzani kupitia Kituo cha Demokrasia (TCD) na wakubwa hawa wakakubaliana yafanyike mabadiliko ya 15 ya Katiba.
Katika mabadiliko hayo waliyokubaliana ni kuwa Katiba ya sasa itabadilishwa na kuruhusu uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi, matokeo ya urais kupingwa mahakamani na mshindi kupata asilimia zaidi ya 51. Kimsingi haya waliyokubaliana ni yenye kutia moyo na nawashukuru kuwa angalau wamefikia uamuzi huu.
Sitanii, nilipata kusema na nimekuwa nikisema kuwa sioni kwa nini tusiwe na Tume Huru ya Uchaguzi ikiwa kwa hakika hatuna mpango wa kuiba kura. Kuna hoja dhaifu zinatolewa mara kadhaa kuwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa kuingiza wapinzani kwenye Tume kunaweza kuleta vurugu na mivutano isiyo ya lazima.
Napata shida na wenye mawazo haya. Kama ni mivutano ingetokea kuanzia kwenye vituo vya kupigia na kuhesabia kura. Nasema hivyo kwa maana kwamba katika vituo hivi kila mgombea ana mwakilishi kwa jina la wakala. Mawakala hawa si kazi yao kuhesabu kura, bali kuangalia kura zinahesabiwaje, basi.
Vivyo kwa Tume ya Uchaguzi, wakiwamo wapinzani si kazi ya wajumbe wa Tume kuhesabu kura, bali kujiridhisha kuwa taratibu za kisheria zimefuatwa katika kujumlisha kura na kutangaza matokeo, basi. Sasa naamini CCM ikiwa hawapendi kufunga mabao ya mkono, hili watalipokea kwa mikono miwili.
Sitanii, jingine tulikuwa tumerahisisha mno cheo cha urais hapa nchini. Kwa mfumo wa simple majority, kwamba aliyepata kura nyingi ndiye mshindi tungerejesha ukabila si muda hapa nchini. Ndiyo maana baadhi ya watu walishaanza kupiga hesabu za makabila yao ni makubwa kiasi gani.
Binafsi nakubaliana na mfumo huu wa kushinda urais kwa asilimia 50 ya kura. Angalau kwa ushindi huu rais anakuwa na mamlaka kamili. Ni vigumu kuamini kuwa wakitokea wagombea 20 wenye nguvu zinazolinganalingana nchi hii inaweza kupata rais aliyechaguliwa na wapigakura wapatao asilimia 6.
Huyu itamuwia vigumu kuongoza nchi. Aliowashinda wakifika mahala wakaunganisha nguvu hiyo asilimia 94, si ajabu wakamwondoa madarakani ndani ya wiki au ikafika mahala wao ndiyo wakawa wanaendesha nchi na kutoa amri kutokea nyumbani au makao makuu ya vyama vyao zikatekelezeka, hasa wakiiga mfumo wa UKAWA.
Mgombea binafsi ni haki ya msingi. Iweje uruhusiwe kuchagua bila kuwekewa masharti, lakini ukitaka kuchaguliwa uwekewe masharti magumu? Sambamba na hili la mgombea binafsi, naona ni vyema hata huyu rais anayeshinda matokeo yake yahojiwe mahakamani. Kuendeleza mchezo wa kutohoji matokeo ni kuchochea kasi na mchezo wa kuiba kura.
Sitanii, wakati nasisitiza hayo, nadhani ukitilia maanani kuwa muda si rafiki tena kwa maana kuwa hautoshi kuandika Katiba mpya, ni vyema tukubaliane kufanya mabadiliko ya 15 ya Katiba, lakini katika kuhakikisha kuwa mabadiliko haya yatakuwa na maana tujumuishe uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari. Vyombo vya habari ni kioo na vitamulika iwapo maafikiano yanatekelezwa vilivyo au kinyumenyume na kuwakumbusha waliokabidhiwa dhamana jukumu lao. Nasema katika mabadiliko ya 15 ya Katiba ikijumuishwa haki ya kupata habari kwa maana vyombo vya habari vikafanya kazi kwa uhuru, nchi hii itapiga hatua kwa kasi kubwa.
Sitanii, nimelisikia tangazo la Mheshimiwa Freeman Mbowe a.k.a Sauti ya Zege. Ametangaza maandamano na migomo isiyo na ukomo kwa nchi nzima. Naelewa kwa nini Mbowe ametoa tangazo hili. Anataka kushinikiza waliyokubaliana kwenye TCD yatekelezwe, lakini ametumia mgongo wa kulitaka Bunge la Katiba lisitishwe mara moja. Mbowe alikuwamo kwenye mazungumzo ya TCD na hapo ndipo ninapopata shida kuamini anawajibika kwa kiwango gani. Tangazo lililotolewa na John Cheyo lilisema walikubaliana Bunge Maalum la Katiba liendelee hadi muda alioongeza rais utakapoisha kisha yafanyike hayo waliyokubaliana.
Maishani huwa sitaki undumilakuwili. Mbowe na UKAWA kama walijua hawajakubaliana katika hilo kwenye TCD kwa nini hajakanusha aliyoyasema Cheyo? Kwa nini kama hoja yao ya msingi ilikuwa ni kusitisha Bunge Maalum la Katiba hawakuendelea kushikilia msimamo huo ndani ya TCD hadi mazungumzo yakavunjika? Leo, ndugu zangu, nasema Watanzania hatujaandaliwa kushiriki maandamano ya haki. Yakifanyika maandamano, vijana wanaoshiriki maandamano wanadhani kufanikisha maandamano ni kupora madukani, kupiga mawe vioo vya magari, kutembeza matusi na ikiwezekana kupigana na polisi.
Tumeshuhudia maandamano kadhaa nchini Marekani ambako tunasema ni baba wa demokrasia. Hata hivyo, wanapotaka kuandamana wanaomba kibali, na hata wasipoomba kibali, zikipita siku tatu, Serikali ina mamlaka ya kusambaratisha maandamano hayo na waandamanaji wanajua hivyo.
Nilipata shida kidogo, kujua kama Mbowe alikubaliana na vyama vya wafanyakazi, waajiri, watumishi wa umma na wengine kuwa uwepo mgomo usio na ukomo. Migomo hii inaweza kuwa na madhara si tu kwa Serikali, bali hata kwa wananchi kwa ujumla. Nchi yetu inatapatapa kujiondoa kwenye umaskini na hakuna nchi iliyopata kuendelea katika vurugu.
Amani tuliyonayo, tukiivuruga tutatafuta wasuluhishi wa kuja hapa nchini kuturejesha tuliko leo. Muda na mali tutakazokuwa tumeharibu havipimiki. Nasema wakati nakubaliana na hoja za wapinzani kuwa matumizi ya Bunge Maalum la Katiba huenda hayana tija, sikubaliani kabisa na dhana ya migomo na maandamano. Nawaomba Watanzania tuwe makini katika kufikia uamuzi wa kushiriki au kutoshiriki maandamano hayo. Tukienda kichwa kichwa, tutavuruga amani yetu na wakati tunakabiliana na madhara ya maandamano, Mbowe na wenzake watakuwa kwenye viyoyozi wanaendesha mazungumzo na wakiwa wameongezewa ulinzi.
Nimesikitishwa na suala la wanahabari kupigwa, nawapa pole wanahabari, ila nafikiri wakati umefika polisi wanapaswa kutambua kuwa wanahabari wapo kazini sawa na wao walivyo. Kinachopaswa kufanywa, ni kukutana haraka kadri inavyowezekana tuweke mipango mikakati ya kurekebisha penye upungufu kwani tunakoelekea 2015 hali inaweza kuwa mbaya zaidi.