Na Mathias Canal,JamhuriMedia,Kilimanjaro

Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Pauline Gekul amewataka wakazi wa Jimbo la Rombo mkoani Kilimanjaro na Watanzania wote nchini kushiriki kikamilifu katika michezo ili kujenga mwili na kuepukana na magonjwa yasiyo ambukiza ambayo kwa sasa ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo nchini.

Akizungumza wakati akifunga mashindano ya riadha (Rombo Marathon) yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Rombo Prof.Adolf Mkenda yaliyofanyika Desemba 23,2022 Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro yaliyokuwa na lengo la kutangaza utalii wa ndani kwa kukimbia chini ya Mlima Kilimanjaro.

Pauline amesema kuwa umefika wakati wa kila mwananchi kushiriki katika shughuli za kimichezo ili kujenga afya yake na kuisaidia serikali kupunguza gharama za matibabu kwa magonjwa yasiyo ambukizwa yanayosababishwa na kutoufanyisha mwili mazoezi.

“Ndugu zangu magonjwa ambayo hayaambukizi ,magonjwa ya presha na sukari yameongeza kasi ya kutuchukulia wapendwa wetu hapa duniani,yameongeza kasi ya kusumbua miili yetu na yameongeza kasi na kuongeza fedha za matibabu hebu tufanye mazoezi” ameongeza Pauline.

Aidha amempongeza Mkenda kwa ubunifu mkubwa wa kuanzisha mashindano yaliyokutanisha watu kutoka maeneo tofauti tofauti na kwa kuisaidia wizara ya michezo kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha shughuli za kimichezo nchini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rombo Antony Tesha amewataka wazee kwa vijana kujitokeza kwa wingi pale wanaposikia mashindano mbalimbali ya riadha na mengine ya kimichezo ambayo yatawasaidia kujenga mwili

“michezo ndio maana ni moja ya jambo ambalo lipo katika utekelezaji wa ilani ya CCM nimeona kupitia mashindano haya ya riadha mambo mengi yanaweza kufanyika ikiwemo kutangaza wilaya yetu tunamuomba Mbunge wetu Mhe.Prof Adolf Mkenda mashindano haya yawe yanafanyika kila mwaka” amesema Antony Tesha.

Aidha amempongeza Mbunge wa Rombo Mhe.Prof Adolf Mkenda kwa kuanzisha mashindano hayo kwa kuwa kupitia mashindano hayo yaliyolenga kutangaza utalii wa ndani Wilaya hiyo itakwenda kujulikana na kufunguka kwa fursa za na kibiashara kwa wakazi wa Wilaya ya Rombo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rombo na mwanzilishi wa mshindano hayo ya Rombo Marathoni amesema kuwa kutokana na mwitikio mkubwa wa washiriki wa mashindano hayo amelenga kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kila mwaka.

Ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo ya mwakani kama waandaaji wamelenga kutumia mapato ya mashindano hayo kutoa ufadhili ili kusaidia shughuli za kimaendeleo katika wilaya hiyo.

“Mwaka huu ilikuw ni ushiriki tu mwakani tunalenga kuanza kutoa ufadhili na tunakusaidia kuanza na kituo cha hosipitali ya Huruma,wanataka kuifanya hospitali ya rufaa ya ngazi ya Mkoa watu wamechangia na sisi tunataka kupitia Rombo Marathoni changie ili tuijenge iwe hospitali ya kisasa ili iweze kutoa huduma ” amesema Prof.Mkenda.

Ili kuimarisha shughuli za kimichezo wilaya ya Rombo na kujenga afya za wananchi amesema kuwa amekusudia kuanzisha pia mashindano ya baiskeli ambayo yatatangazwa na kuanza hivi karibuni.