Viongozi wa Tanzania kuanzia Baba wa Taifa, Mzee Mwinyi, Rais mstaafu Awamu ya Pili,na hivi sasa Rais mstaafu Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa wote hawa kwa namna moja au nyingine wamekuwa wanashughulikia usuluhishi kule Rwanda, Burundi, Sudan na Comoro.
Kumbe Taifa letu tunao wazee wenye uwezo wa kuendesha mazungumzo ya usuluhishi. Ni muda mwafaka sasa Serikali ya Jamhuri na ile ya SMZ waoneshe jitihada za makusudi kabisa kumaliza hii hali ya wasiwasi kile Visiwani.
Viongozi wastaafu hawa kutoka Bara na Visiwani, pamoja na wazee mashuhuri kama akina Maalim Seif, akina Duni, akina Amani Karume watumie karama zao za kuzaliwa kukabiliana na hali hii na kumaliza kabisa tofauti zilizopo kuhusu kuaminiana.
Kama Afrika ya Kusini, Askofu Desmond Tutu aliweza kuleta maridhiano kati ya makaburu na wananchi weusi walikaa mezani wakazungumza, hatimaye suluhu ilipatikana, tena kwa njia ya amani. Kwa nini kule kusini Wazungu na weusi wamepatana? Kule kulikuwa na ubaguzi kwa karne nzima lakini ugumu wa mioyo ya makaburu ulivunjwa. Matokeo ya maridhiano yale ulimwengu uliwazawadia Askofu Desmond Tutu na De Klerk medali ya “Amani iitwayo Nobel Peace Medal”. Kwa vipi Tanzania hilo lisiwezekane? Tukaze moyo wa kujikana matakwa yetu na tuelekeze utaifa wetu.
Ombi langu mimi sasa ni hili. Huu ni wakati mwafaka kule Visiwani Waarabu na weusi wapatane. Hakuna mgeni kule. Wote ni Wazanzibari. Nimeonesha kitakwimu za sensa za mwaka 2012. Iundwe tume ya wazee mashuhuri watakaotafuta njia za kudumu kwa maridhiano huko Visiwani. Mzee Rashid Salim, Brigadia Jenerali Haji Faki na wazee wengine kadhaa kule Visiwani wanaweza kutoa mchango mzuri sana katika usuluhishi wa hali nzima ya kutokuaminiana.
Maneno ya Mzee Rashid SalimuRashid niliyonakili humu yanafanana na maneno ya Baba wa Taifa aliyoyatoa pale Kilimanjaro Hotel Machi 13, 1995 mbele ya waandishi wa habari. Mwalimu alipata kusema “Ile dhambi ya ubaguzi haifi. Inaendelea ukisha kuitenda, inaendelea; ni kama ukila nyama ya mtu, utaendelea kula” (Nyufa Uk 10).
Dhambi ile ya kumuua Karume inaendelea kutafuna Serikali zote za SMZ. Hakuna anayenufaika na hali ya mvutano kati ya CCM na CUF kule Visiwani. Juhudu za makusudi zifanyike kuwaunganisha Wazanzibari wote. Itikadi za vyama vyao zisiwe kikwazo cha suluhisho la kudumu la kujenga moyo wa kuaminiana miongoni mwa Wazanzibari wote.
Aliyodokeza Mzee Rashid Salim yafanyiwe kazi kuondoa vinyongo miongoni mwa Wazanzibari. Mbona Afrika ya Kusini waliamua kusameheana na matokeo yake kiongozi wa ANC, Mzee Mandela, alifungulia minyonyoro ya gereza kule Cape Town na akaja kuwa Rais wa Afrika Kusini? Makaburu, pamoja na ugumu wa mioyo yao juu ya mtu mweusi, sasa tumeona kinyongo kimekwisha, kisasi kimekwisha na wote sasa wanaishi kama wazawa wananchi wa Afrika Kusini. Tunahitaji kusameheana na kusahau yote yaliyopita.
Tuanze na wazo lile la Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar. Kinachohitajika sasa hapa ni moyo wa maridhiano. Kule Afrika Kusini, Askofu Desmond Tutu aliita ‘The spirit of reconciliation’. Kwa moyo namna ile makosa ya mauaji yote yaliyotendwa na makaburu kwa watu weusi kama mauaji ya Sharpeville, vifungo vya wanasiasa akina Mandela, mauaji ya Soweto yalisamehewa na kufutika.
Hali kadhalika, ulipuaji mabomu uliofanywa na ANC kwa Wazungu yalitamkwa na kusameheka. Hiyo ndiyo maana ya ‘reconciliation’. Hayo yakifanyika Zanzibar kutakuwa hakuna Uarabu, hakuna Hizbu wala utu weusi (gozi) wala uafro. Hapo kutazaliwa Uzanzibari kwa hao wote waliozaliwa kati ya Aprili 26, 1964 mpaka leo hii.
Ni Wazanzibari pyua kabisa. Wazanzibari wote wakidhamiria kwa moyo mmoja matokeo yake amani itapatikana na Zanzibar tunayoijua sasa. Itakuwa mpya kabisa. Wazanzibari wote watakuwa wamoja. Vile vikao vya vijiweni pale Michenzani, Darajani, Mao Tse Tung, Saateni marufuku na kwingineko vitakoma na kutoweka kabisa.
Hebu tuendeleze demokrasia katika nchi yetu ya Tanzania. Ni demokrasia asilia isiyo na kivuli cha nchi za Magharibi. Kila taifa lina aina ya demokrasia yake. Yetu ni ya Kitanzania kama ilivyotokea ile demokrasia ya Afrika Kusini – kaburu na mtu mweusi ni kitu kimoja. Ni sawasawa tu.
Kwa hilo nathubutu kusema na kuomba Mwenyezi Mungu aibariki Tanzania, adumishe uhuru na umoja. Tusikumbushane yaliyopita na tuape kuwa yeyote atakayegeuka na kutazama nyuma na alaaniwe ageuke jiwe. Hakuna lisilowezekana hapa duniani. Zanzibar mpya na ya leo inawezekana. Tuwe na moyo kabla ya kutafuta silaha za masambaratiko.
Nihitimishe kwa ule mwito alioutoa Baba wa Taifa tarehe 2 Novemba, 1978 pale Diamond Jubilee kwa Taifa tulipovamiwa na Idi Amin, namnukuu “….Tunayo kazi moja Watanzania sasa. Ni kumpiga; uwezo wa kumpiga tunao, sababu za kumpiga tunazo, na nia ya kumpiga tunayo… Tutampiga”.
Mimi niombe maneno hayo hayo viongozi wetu wa CCM na CUF kule Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wayageuze kidogo tu na kusema. Wazanzibari wanayo kazi moja tu kuridhiana. Kama nia ya maridhiano wanayo, sababu za maridhiano wanazo, basi sasa wawe na uwezo yaani dhamira ya dhati kwa maridhiano. Hapo, wallah wabillah wa taala suluhu kule Visiwani itapatikana. Amina. Mungu ibariki Zanzibar.