Juzi juzi hapa, wakati naangalia runinga matangazo ya BBC, kulikuwa na majadiliano makali katika Bunge la Uingereza. 

Kule kwanza kumetokea kashfa ile ya Panama. Nyaraka za Kampuni ya Mossack Fonseca zilizowataja vigogo waliokwepa kodi nchini kwao, na kupeleka fedha zao kuficha katika mabenki kule Panama.

 Katika hili, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alitajwatajwa. Huyu waziri mkuu amejinasua kwa maelezo kuwa baba yake aliwekeza huko na yeye amerithi kiasi cha pauni 300,000 hivi, na hii ilitokea kabla ya yeye kugombea uongozi katika chama chake na hatimaye kuwa waziri mkuu.

Si hivyo tu, bali alikwenda mbali zaidi hata kuanika mshahara wake wa Waziri Mkuu wa Uingereza na makato ya kodi zote. Katika kashfa hiyo, Waziri Mkuu Cameron alikiri kuwa mwanahisa katika Kampuni ya Blairmore Holdings Inc., ambayo imehifadhi fedha kwa siri katika taasisi za kifedha nchini Panama lakini alishaziuza hisa hizo.

Basi, katika Bunge lile la Uingereza, juma lililopita, Waziri Mkuu Cameron alipeleka mswaada wa wakwepa kodi na mambo ya rushwa.

Niliona wabunge wa pande zote mbili – wale wa Serikali (chama tawala cha Conservatives) na wale wa upinzani (Labour) wakimbana waziri mkuu yule awajibike kwa kashfa ile ya Panama. Mbunge mmoja mzee mzee hivi, alitoa lugha isiyokubalika mle bungeni wakati anachangia hoja ile. Hapo ndipo nilipoona demokrasia ya Uingereza ilivyo!

Spika alimwomba mheshimiwa mbunge yule afute matamshi yake mle bungeni. Yule mbunge hakuyafuta. Ndipo spika akamtoa nje ya bunge lile kwa kutamka kifungu cha kanuni za bunge kinachompa uwezo spika kumtoa nje ya bunge yeyote anayekwenda kinyume cha kanuni za bunge lao.

Mheshimiwa mbunge mzee nilimwona akisimama na kuondoka taratibu mle bungeni bila hata ya kulazimishwa na walinzi wa amani (polisi). Nikajiuliza, mbona wale wenzetu hawathubutu kumwita spika wao mbabe? Mbona hawangojei waitiwe polisi kuwaswaga, au kuwavuta na kuwatoa kwa mabavu?

Ile ni demokrasia iliyosheheni uelewa na uwajibikaji. Hapa Bongo, loo! si ajabu upinzani wote ungelipuka kwa kelele kupinga mwenzao kuondolewa na si ajabu upinzani wote ungesimama na kuondoka humo bungeni.

 Hilo linaonesha namna tunavyotafsiri uhuru wa kujieleza hapa nchini. Kanuni za Bunge wamezitunga wote humo bungeni, sasa inapofika utekelezaji kunakuwa na kigugumizi kutii mara moja vipi? Wanalalama haki za binadamu zinakiukwa. Uhuru wa kutoa maoni unaminywa. ‘Tunabanwa sana wapinzani’ ndivyo wanavyodai.

Lakini neno haki daima tunalitumia visivyo. Haki inaambatana na wajibu. Inapodaiwa haki ya mtu eti ‘hiyo ni haki yangu kikatiba’ je, wajibu wa kupata haki hiyo ni upi? Waingereza wanasema ‘rights go with fitting duties’, yaani haki zina wajibu wake. Je, sote tunalielewa hilo? Kwa nini tunakimbilia kudai haki lakini kamwe hatutaji wajibu husika kwa haki namna hizo?

Juzi juzi gazeti moja hapa nchini limenukuu matamshi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, namna hii: “Nitaendelea kutumia walinzi na gari za Serikali kwa sababu ni stahiki zangu. Situmii huduma hizi kama zawadi, hapana. Hizi ni haki zangu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar 1984 Toleo la 2010” (Gazeti la Tazama Toleo No. 7010 la tarehe 12/4/2016 Uk 2).

Hebu tuwe wakweli hapa. Haki zile alipewa kama Katibu wa CUF au kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa? Kwa mujibu wa kazi zake zile za kumsaidia Rais wa SMZ, ile ilikuwa ni stahiki yake kabisa. Je, bado hata sasa anamsaidia Rais wa SMZ katika wadhifa ule? Hapana! Hapo ni wazi kama Katiba yao huko Zanzibar bado inampa haki bila hata kuwajibika kwa lolote serikalini, basi hiyo Katiba ni mbovu, haifai!

Haiwezekani hata kidogo mtu asiyestaafu kwa heshima serikalini bado Serikali ikaendelea kumhudumia. “You must retire honorably to quality for those retirement benefits; politically or otherwise”. Huo ni utaratibu duniani kote, isipokuwa Zanzibar tu.

Mwandishi wa habari ile alitoa maelezo zaidi kuwa Maalim Seif anadai eti ‘Ni stahiki zangu kikatiba na kutamka hivi “mimi ni kiongozi tena mkubwa tu. Kwa vile yanayonistahiki kufanyiwa kisheria isionekane kuwa siitambui serikali kwa hivyo nisihudumiwe… Ni haki yangu. Isitoshe fedha hizi ni za wananchi nami nachangia kodi kama wanavyochangia wengine. Hizi fedha hazitoki mfukoni mwa viongozi wa CCM’.” 

Kwa akili za kawaida tu (mere common sense), tujiulize kwani kila mlipa kodi anastahili marupurupu namna ile? Serikali gani inatoa mastahili kama hayo kwa wananchi wake wote ilimradi wanalipa kodi? Ni madai ya mtu aliyepagawa. Fedha za kodi siyo za wanachama fulani ni fedha za taifa na zinatawaliwa na serikali inayokuwa madarakani. Kusema ‘hizi fedha hazitoki mfukoni mwa viongozi wa CCM, ni lugha ya kuudhi sana (provocative language).

Hakuna kitu kama fedha za kutoka mifukoni mwa viongozi wa chama chochote kile. Ni hekima na busara kiongozi kuongea kwa utulivu na siyo kwa jazba na ubabe. Lugha ya maudhi ni lugha ya kujihami tu siyo lugha ya maridhiano hata kidogo.

Kwa mtazamo wa ndani namna hiyo (this inward looking is self-conceited proclamation), mtu yeyote ataona Maalim anaonesha ubabe na kujiamini. Si hivyo tu lakini wanadamu na hasa wanasiasa hawaoni huo kuwa ni unafsi. Kwa kiingereza inajulikana kama ‘egoitic assertion’. Ni kujiona, ubinafsi na kutokufikiria taifa wala wengine, eti mradi mimi napata wengine shauri lao!

Ehee! hayo ni matamshi yanaonesha tabia isiyokubalika katika jamii. Mimi sipendi kuwahukumu wengine bila kujiona na upungufu wangu mwenyewe nilionao. Hivyo, hapa sithubutu kumhukumu Maalim bali ninaloonesha hapa ni ile tabia ya kujifikiria mtu siyo ya kiungwana.

Hapo juu nimetoa kichwa kijielezacho ‘Tuendeleze demokrasia’. Mimi siyo mbunifu wa hilo; hicho kilitolewa na CCM mwaka 1984 pale Dodoma. Ni kichwa cha hotuba ya Mwenyekiti wa CCM aliyotoa kwa wabunge pale Dodoma walipokaa kama Kamati ya Bunge ya chama tarehe 1 Februari, 1984.

Mwalimu alikuwa amedhamiria kuwaelimisha waheshimiwa wabunge, hali ilivyokuwa wakati ule hapa nchini. CCM wametoa kijitabu kuhusu hotuba ile na wakabuni kichwa hicho kinachosema ‘Tuendeleze demokrasia’.

Nieleze kwa ufupi yaliyojiri siku zile katika Taifa letu kwa ujumla. Mwalimu aliona hali ya watu kuogopaogopa ukweli ulivyo nchini. Watu wakiogopa kuzungumza kiwaziwazi juu ya Katiba ya nchi hii, kutoa mawazo na maoni yao waziwazi. Kulikuwa kama alivyoita Mwalimu hali ya vurumai tupu.

Mimi nina utamaduni wa kunukuu yale yaliyosemwa ili wasomaji wapate undani wa taarifa yenyewe. Mwalimu aliwaambia waheshimiwa wabunge pale Dodoma hivi; “Hali mbaya na vurugu nchini inajulikana sana. Hali hiyo imejitokeza katika sura nyingi. Labda nitaje mambo machache yaliyojitokeza katika majadiliano ya Kamati Kuu, mambo ambayo ni sehemu ya msingi wa hali mbaya ya vurugu ya siasa nchini.

Kwanza, kuna watu wanaowaambia wananchi Zanzibar kwamba mazungumzo ya marekebisho ya Katiba ni mbinu ya Bara kutaka kuimeza Zanzibar. Wananchi wengi wa Zanzibar wameanza kuamini uvumi huo. Huku Bara nako baadhi ya wananchi wameanza kuamini kwamba kwa sababu ya hofu hiyo ya kumezwa, Zanzibar inajiandaa kuvunja Muungano.

Pili, yako maoni kwamba SMZ inapinga maongozi na madaraka ya chama, yaani ‘supremacy’ ya CCM kwa mambo yanayohusu Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya SMZ.

Tatu, zimetolewa kauli hadharani na watu walio karibu na uongozi wa SMZ za kupinga Muungano na kukebehi misingi ya umoja wa Taifa letu na kukashifu siasa yetu ya Ujamaa na Kujitegemea. Lililo baya zaidi ni kwamba kauli hizo za uhaini hazikukanushwa na waliohusika hawakukewa.

Nne, mwenendo wa watu waovu umejitokeza si hapa nchini, lakini hata nchi za nje ambako wametangaza maneno ya kupinga Muungano na kashfa nyingine kiasi kwamba heshima na sifa ya Taifa letu imepakwa matope. Hata marafiki wa Tanzania wameingiwa na wasiwasi kuhusu hatima ya umoja wetu na uhai wa Taifa letu.

Tano, ni dhahiri kwamba hali ya vurugu kama hii inaweza kuhatarisha usalama wa nchi yetu na kwa kweli wakati wa kukaribia miaka 20 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilipatikana taarifa kwamba usalama wa Zanzibar ulikuwa hatarini kutokana na njama za maadui wa SMZ na Serikali ya Muungano. Ingawa njama hizo zimekwishadhibitiwa, lakini adui anaweza kuanza upya wakati hali ya vurugu ya siasa inaendelea sambamba na hali ya uchumi”. (Kijitabu “Tuendeleze demokrasia” Uk 23, kimetolewa Makao Makuu ya CCM na kimepigwa chapa Zanzibar 1984).