Na Lookman Miraji
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Innocent Bashungwa amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa wa jumuiya ya maridhiano ya Amani nchini(JMAT) kuwa mstari wa mbele kutangaza amani, upendo na umoja miongoni mwa wananchi wa Tanzania bila kujali tofauti zao za kiimani, kisiasa na kijamii.
Waziri Bashungwa ameyaeleza hayo jijini Dar es salaam alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika futari ya viongozi wa dini na wadau wa amani nchini iliyoandaliwa na Jumuiya ya maridhiano na Amani Tanzania.
“Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na JMAT katika kuhakikisha kuwa tunaendelea kuwa na jamii iliyo na amani na utulivu pasipo kujali tofauti zetu za kiimani, kiitikadi na kiutamaduni” Alisema Bashungwa.
Kadhalika nae Mufti mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir amewasihi watanzania kuendelea kuilinda amani iliyopo nchini na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani wakati ambao nchi inaendelea katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Kupitia hafla hiyo viongozi mbalimbali walitunukiwa tuzo mbalimbali za heshima shughuli iliyoongozwa na mwenyekiti wa jumuiya ya maridhiano na Amani, Sheikh Alhad Musa Salim.

