Mwaka 2016 wakati tunakwenda kuivaa Nigeria, wachezaji wa Tanzania wanaocheza nje karibu wote waliitwa kuja kulikabili jeshi hilo linalotamba katika soka Afrika. Ila kilichotokea ilikuwa aibu. Wengine walikuwa hawajulikani, hata TFF hawawajui. Tukaanza kuulizana kama huyu kweli ni wa kwetu au la!
Hii ilikuwa ni aibu, na leo tunataka kuwakumbusha TFF umuhimu wa kukusanya data za wachezaji wa Tanzania waliopo nje. Kimoja tu. Uwezo wa vyama vya soka kuwatumia barua pepe wachezaji wa kigeni huchangiwa na ukaribu kati ya vyama hivyo na wachezaji wenyewe. TFF walipaswa kuwa na taarifa sahihi za wachezaji wetu wote wanaocheza kwenye ligi mbalimbali duniani na taarifa hizi zinapaswa kuendana na muda uliopo.
Iko haja pia ya kuhakikisha hata zile video zinazowaonyesha wakicheza, zinapatikana kwa makocha wa timu ya taifa mara kwa mara. Wakati benchi zima la ufundi la Taifa Stars linapowatazama kwa ukaribu wachezaji wanaocheza Ligi Kuu, ni vizuri wale walio nje ya nchi wakatazamwa maendeleo yao ndani ya wakati husika. TFF itoe ushirikiano mkubwa katika hili suala, inao uwezo wa kufanya hivyo. Wachezaji wetu wanaocheza nje ya nchi wana mbinu wanazozipata kutoka kwa makocha wao, zinaweza kabisa kuiongezea Taifa Stars ufundi na ari ya utafutaji ushindi.
Unamtazama Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta jinsi wanavyowakusanya mabeki wa Ivory Coast na Nigeria, unabaki kujiuliza kama tungekuwa na wengine watano wa kiwango cha kujiamini kwao, Taifa Stars ingekuwa bora kiasi gani?
Mbwana Samatta anakokota mpira kwa kasi halafu anageuka huku akitafuta upenyo wa kukung’uta shuti, anafanya mambo tunayoyaona kwenye ligi za Ulaya kila mwisho wa wiki. Thomas Ulimwengu alipitishiwa pasi ya mwisho na Said Ndemla, akapiga shuti lililompa taabu golikipa wa Nigeria. Vipi kama Said Ndemla angekuwa anacheza soka la kulipwa nje ya nchi? Shomari Kapombe alipambana na winga hatari wa Nigeria, Simon Moses. Kwanini Kapombe asiwe anakuja kuichezea Taifa Stars halafu mechi ikimalizika anapanda ndege kuelekea kwenye nchi anayochezea soka huko nje?
Wakati TFF ikiwa mbioni kuwajua Watanzania wote wanaocheza soka la kulipwa, ni wakati muafaka wa kuanza kuwauza wachezaji kama Said Ndemla.
Ukusanyaji wa taarifa za wachezaji wetu walioko nje uende sambamba na zoezi la kuwasaidia wale wenye uwezo kupata timu katika ligi za mabara mengine. Tunawakosa wachezaji wachache wenye kuweza kuituliza timu wakati inapokutana na wachezaji wakubwa wa timu za mataifa mengine ya Afrika.
TFF ambayo kwa sasa iliwakusanya watoto wa chini ya miaka 13 na kuwapeleka Afrika Kusini, ingawa hatujui yameishaje, watumie jitihada hizo hizo katika kuwafuatilia wachezaji wetu wanaotafuta maisha nje ya nchi.
TFF wasibweteke wakidhani kwamba wachezaji wenye asili ya Tanzania wataitikia mwito wa kuja kuichezea Taifa Stars kirahisi tu. Wengine wamekwenda nje kwa nguvu zao wenyewe, wamesota sana mpaka kufikia walipo.
Waheshimiwe kama watu waliotoka nje ya mipaka kwa sababu ya utafutaji wa maisha, kama wafanyavyo Watanzania wengi tu wanaoishi ughaibuni. Isiwe ni amri inayotoka kwa mkubwa kwenda kwa mdogo.
Wakati huu ndio muafaka katika kuanzisha mawasiliano ya barua pepe kati ya TFF na wachezaji wenyewe au mawakala waliowapeleka huko waliko. Wenzetu wanawafuatilia wachezaji waliotoka kwenye ligi za nyumbani mpaka wale ambao wamezaliwa nje ya Afrika lakini baba zao ni Waafrika waliokwenda ughaibuni miaka ya zamani.
Vyama vyao vya soka viko tayari kupokea taarifa za wachezaji waliozaliwa Afrika na wale waliozaliwa ughaibuni ndani ya mwaka mzima. Miezi yote kumi na mbili hutumika katika kumjua ni mchezaji gani ameumia, mchezaji gani kauzwa wapi, mchezaji gani hana nidhamu, na taarifa nyingine za aina hiyo.
TFF ipokee changamoto hii ya kuwa karibu na wachezaji wetu wote walio nje ya Tanzania. Haipendezi kumwambia mchezaji wa Tanzania arudi kuichezea timu yake ya taifa wakati ndani ya muda wote aliokuwa akihangaika kutafuta maisha huko nje hakuwahi kukumbukwa na TFF kwa namna yoyote ile.
Hivi sasa TFF inao wadhamini wakubwa, hili suala la kupata taarifa za wachezaji wetu haliwezi kuwa na gharama ambazo haliwezi kuzibeba.
Timu ya taifa inaweka kambi nje, inatumia fedha nyingi. Sidhani kama inashindwa kuanzisha mawasiliano na wachezaji wetu walio nje ya nchi. Taifa Stars ya ushindi huundwa kupitia mchango wa kila mchezaji ambaye ni Mtanzania.
Awe anachezea timu ya Ligi Kuu ya Tanzania, awe anachezea timu ya Congo au Afrika Kusini, awe anachezea timu ya daraja la pili nchini Norway au Uingereza. Siku zote mchango wao ni muhimu na unahitajika.
Mchezaji anayetafutwa na TFF ndani ya wiki moja kabla ya mechi iliyo ndani ya kalenda ya FIFA, anaweza kuidengulia TFF, lakini ikiwa yapo mawasiliano ya mara kwa mara baina yake na shirikisho letu la soka, lazima atatoa ushirikiano pindi akihitajika.
Wenzetu huhakikisha silaha zao zote za maangamizi zinakuwepo wakati timu zao za taifa zinapocheza mechi muhimu. TFF haijachelewa katika kuanzisha mawasiliano ya karibu na wachezaji ambao ni Watanzania wanaocheza nje ya nchi.
Charles Boniface Mkwasa
Aliwahi kuifundisha Stars na kwa sasa ni kocha Yanga, anakiri kuna kazi kubwa ya kupata data za wachezaji wa Tanzania waliopo nje kutokana na mambo kuendeshwa kimazoea.
“Kuna kazi kubwa, lakini tutafika, ila ilikuwa muhimu zaidi kukusanya data za Watanzania wanaocheza nje,” anasema Mkwasa.
Sven Van der Broeck
Kocha huyu wa Simba amekiri Tanzania kuna vipaji vingi na wachezaji hawa wanapaswa kutoka ili kuleta mapinduzi makubwa katika soka.
“Wachezaji wapo wenye vipaji vya kila aina, ni uthubutu tu unaotakiwa,” anasema.