Na Deodatus Balile,JamhuriMedia,Dubai

Wiki iliyopita nimepata fursa ya kusafiri kwenda Dubai. Nimetembelea maeneo kadhaa, ila moja ya maeneo hayo ni bandari tatu zinazoendeshwa na Kampuni ya DP World.

Kampuni hii inamilikiwa na familia ya mfalme anayetawala Dubai. Kwa Dubai, kampuni hii inaendesha bandari tatu ambazo ni Jebel Ali, Mina Rashid na Al Hamriyah. Bandari hizi ziko kati ya umbali wa kilomita nane na 46 kutoka bandari moja hadi nyingine.

Takwimu nilizozipata, bandari hizi zinasafirisha makontena milioni 22 kwa mwaka hapa Dubai. Kampuni hii inafanya kazi katika nchi zaidi ya 40 duniani na inaendesha magati 82 sehemu mbalimbali duniani kwa mwaka, ambayo hupokea na kusafirisha makontena milioni 70 yanayosafirishwa na meli 70,000 duniani kote.

Bandari ya Dar es Salaam

Sitanii, ni vigumu mtu kueleza akaeleweka anamaanisha nini. Ukifika katika Bandari ya Jebel Ali, ndipo unaona kuwa kuna binadamu wanaofikiri. Hoja si tu, makontena wanayosafirisha, bali pia mipango ya sasa na baadaye. Katika bandari hizo tatu, kuna mitambo mikubwa ya kushusha na kupakia hayo makontena milioni 22, lakini hawaridhiki.

Ndugu zetu wa hapa Dubai, kupitia DP World kwa sasa wanaendelea na mradi wanaotarajia kuukamilisha mwakani, ambao bandari itaendeshwa kwa kutumia akili tarakirishi (artificial intelligence), kwamba mteja akiwa na kontena lake, hatalazimika kusubiri ‘winch’ ipangue makontena matano kufikia kontena lake la chini.

Itakuwa zinapangwa kwenye chanja (shelves) ambayo ukibonyeza kifungo (button) na kuweka namba ya kontena husika, hata kama litakuwa katikati ya makontena 30,000 litajichomoa na kutoka nje. Hii si ya kufikirika au kusadikika, bali wameanza kujenga mitambo husika.

Sitanii, hawa DP World wapo katika nchi kadhaa za Afrika. Wapo Senegal, waliyofanya Mungu anajua. Wapo Somalia, nchi ambayo ipo vitani miaka yote tangu kifo cha Rais wao Mohamed Farrah Aidid Agosti Mosi, 1996, lakini kwa msaada wa DP World kuna habari sizizofurahisha katika masikio ya Watanzania. Kwamba kwa macho yangu nimeshuhudia kondoo, matikiti maji, vitunguu, nyanya, mchicha, viazi na kila chakula unachokiwaza kikiuzwa Dubai kutokea Somalia, ilhali sisi huu ni msamiati.

Nimeuliza inakuwaje sisi hatuwezi hili, nikapewa jibu la aina yake. “Shida si Watanzania, bali mifumo iliyowekwa na viongozi wenu. Kinachotakiwa ni kuwawezesha Watanzania. Kuwajengea maghala ya kuhifadhia bidhaa za kilimo karibu na bandari, kuwaeleza viwango na mbinu bora za kilimo. Wananchi wakifahamu mahala penye fedha, masharti watayafuata na kutengeneza fedha. Watanzania wanaweza haya,” ameniambia ofisa mmoja niliyezungumza naye katika Bandari ya Jebel Ali.

Sikukomea hapo, nimeuliza imekuwaje bandari tatu ziko pamoja zinasafirisha makontena milioni 22 kwa mwaka hapa Dubai, ilhali sisi hapo Tanzania tumezungukwa na nchi nane, lakini tunasafirisha makontena 700,000 tu kwa mwaka. Jibu nililopewa ni lile lile ujenzi wa mifumo. Tena, hawa DP World wakasema wanatafuta fursa ya kuja Tanzania kushirikiana na Tanzania, lakini miaka yote wamekwama.

Katika kukwama, wakaamua kwenda nchi jirani ya Rwanda. Wamejenga bandari kavu Rwanda. Makontena ya nchi nyingine sasa yanapitia Bandari ya Dar es Salaam yanakwenda Rwanda, nchi hizo zinachukua makontena pale. Kampuni ya vyakula ya KFC imefungua ofisi zake Rwanda. Ndugu zangu Watanzania, nimesisimuka mwili. Manyoya yamesimama. Sikuamini nilichokiona katika wasilisho.

Rwanda imewapa DP World ardhi yenye mita za mraba 20,000 kuweka bandari kavu. Hizi mita za mraba zimekuwa ufunguo wa Rwanda kuingia katika biashara ya bandari. Hivi sisi tuna kilomita ngapi za mraba katika Bahari ya Hindi, hadi leo tuzidiwe na Rwanda inayoanza kuwa nyota inayong’ara ndani na nje ya Bara la Afrika?

Kwa masikitiko, hapa nchini kwetu tumeambiwa eti Bandari mpya ya Bagomoyo ikijengwa, itaimeza Bandari ya Dar es Salaam. Wajinga ndio waliwao. Bandari zinapokuwa nyingi, ndivyo ushindani unavyoongezeka. Ndivyo mapato yanavyoongezeka. Bandari mbili hapa Dubai zinatenganishwa na kilomita nane , ila bado zinatengeneza fedha ndefu. Sisi hapo kwetu TICTS imekaa hapo miaka 22, bado tunahudumia makontena 700,000 tu kwa mwaka, wenzetu wanahudumia milioni 22. Hapana. Tutafute wenye uwezo wa kutuvusha. Bila kuuma maneno, DP World wanayo nafasi ya kuivusha Tanzania.

Sitanii, nimelazimika kumkumbuka Mwenyekiti wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema wa Afrika Kusini. Binafsi naamini wazee wetu wamepambana kupata uhuru wa nchi hii. Ila sisi hakuna tulichopambania. Naamini wakati wetu sasa umefika tupambane kupata Uhuru wa Kiuchumi. Hapo kwetu chanzo muhimu cha uchumi ni bandari.

Kwa miaka 22 tumekuwa na Kampuni ya Tanzania International Container Terminal Services (TICTS). Nasikia wiki hii mkataba wao umekwisha hapo nchini. Tuwashukuru kwa kazi waliyoifanya kwa miaka 22, ila sina uhakika kama wameifikisha nchi yetu katika malengo tarajiwa. Kwa mfano, DP World inazalisha asilimia 33 ya uchumi wa Dubai.

Moja ya eneo la makontena katika bandari zinazoendeshwa na DP World, Falme za Kiarabu (UAE).

Hii maana yake ni nini? Nchi yetu kama ikiitumia vema Bandari ya Dar es Salaam, ina uwezekano wa kuzalisha si chini ya asilimia 45 hadi 50 ya bajeti ya taifa letu. Tanzama imezungukwa na nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Zambia, Zimbabwe na Malawi, ambazo zina uwezekano mkubwa wa kutumia bandari yetu. Si hizo tu, hata sehemu ya Kenya na Msumbiji, baadhi ya mikoa yake ni rahisi kutumia bandari zetu.

Sitanii, mpendwa msomaji. Wiki hii niruhusu niishie hapa. Wiki ijayo nitaandika kwa kina wapi tumeteleza, na tunaweza kusahihisha nini. Watanzania hatukuzaliwa kula shida. Nafahamu wapo watu wachache wenye vita yao mkononi wakitaka wapewe bandari waendelee kuvuna. Mstari huu tuuvuke. Tujenge nchi. Tanzania kwanza, masilahi ya mtu mmoja mmoja baadaye.
Mungu ibariki Tanzania.