Habari yenye kichwa cha maneno, “Waziri achafua hewa mazishi ya Padri Z’bar” iliyochapishwa Februari 21, 2013, ilinikumbusha agizo la Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa (pichani chini), aliyetuasa akisema “Kama hujafanya utafiti, huna haki ya kuzungumza”.
Kwenye mazishi ya Padri Evaristus Mushi, Februari 20, 2013, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, alitoa salamu za pole kutoka serikalini akisema kifo hicho kilichotokea kwa kupigwa risasi, ni mapenzi ya Mungu.
Iliripotiwa kwamba waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar alilokuwa akilihudumia Padri Mushi, walishuhudia mmoja wa watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki, akimpiga risasi padri huyo wakati akiegesha gari lake ili aingie kanisani kuongoza ibada.
Umati wa watu waliofurika katika makaburi ya mazishi walipaza sauti wakisema kifo hicho hakikutokana na mapenzi ya Mungu, bali kimefanywa na watu wakatili.
Tuangalie sheria za nchi za kistaarabu zikiwamo nchi za Jumuiya ya Madola ambazo Tanzania ni mojawapo. Zinasema mtu atachukuliwa kisheria kuwa ana akili timamu wakati wowote unaohusika hadi itakapothibitishwa vinginevyo. Pia, zinaainisha kwamba washiriki wa mtenda jinai ni watu gani. Miongoni mwa watu hao ni anayetenda au kuacha kutenda ili kumsaidia mtenda jinai, au anayemshauri, anayesababisha au kutuma mtu atende jinai.
Waziri Emmanuel Nchimbi, aliyetembelea eneo la tukio la kuuawa kwa Padri Mushi, alisema tukio hilo ni la kigaidi. Sasa, Waziri wa Nchi huyo ana mawazo kinyume cha sheria kwamba mtenda jinai na mshiriki au washiriki wake atawachukulia kisheria kwamba hana/hawana akili timamu wakati wowote ambao unahusika hadi itakapothibitishwa kwamba ana/wana akili timamu?
Kwa mtazamo huu wa Waziri wa Nchi, ndiyo unaweza kusema kifo cha kupigwa risasi kinatokana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu aliyepiga risasi, aliyeacha kutenda ili amsaidie kupiga risasi, aliyemshauri, aliyesababisha au aliyemtuma apige risasi, wote wanapaswa kuchukuliwa kwamba, kwa kudura za Mungu, hawakuwa na akili timamu hadi umma uthibitishe kwamba walikuwa na akili timamu?
Pia, kuna hili neno, ‘freemason’ nalo limewaparamia Watanzania. Leo hii, Mtanzania akitaka kushusha hadhi ya utajiri wa mtu mwingine, anamwita mtu huyo ‘freemason’.
Je, ‘ufreemason’ ni nini? Utakuta kwamba Sheria ya Vyama ya Tanzania, Sura ya 337 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002, kifungu 2 (1) (d) kinatamka kwamba sheria hiyo haihusu wanachama wa chama cha ‘Freemasons’ kilichoundwa kulingana na kanuni chini ya lolote la mabaraza tawala yaliyosajiliwa ya wafreemasons katika Ufalme wa Muungano wa Uingereza na Irelandi ya Kaskazini. Kamusi ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), Dar es Salaam, ya English-Swahili, toleo la pili, 2000, inafafanua neno ‘Freemason’ kwamba ni mwanachama wa chama cha siri cha kusaidiana.
Tovuti ya intaneti inatangaza kwamba ‘ufreemason’ uko katika sura nyingi ulimwenguni, ukiwa na wanachama wapatao milioni sita, na ni mfumo wa kindugu ambao ulichimbuka mwishoni mwa karne ya 16 na mwanzoni mwa karne ya 17. Tovuti hiyo inahusisha mfumo huo na nchi za Scotland, Ireland na Marekani, na kwamba nchini Marekani, wanachama ni karibu milioni mbili. Je, Mtanzania anajua ‘ufreemason’ hasa ni nini? Angalau anajua masharti ya kuwa mwanachama? Hapo Magomeni Mapipa, karibu na kituo cha daladala baada ya Kituo cha Usalama, ukielekea Jangwani, nimesoma kibao kilichoandikwa, “Dr. Kibosho, 0717 934676 Akili darasani, Pesa za majini ‘Freemason’.
Hadi sasa sijaelewa matumizi ya neno hilo, ‘Freemason’. Je, ni kwamba majini ni Freemason au yeye ni Freemason? Na nimesoma katika moja ya gazeti fulani la Februari 25, 2013, kwamba ilibidi Meneja wa Taasisi ya Ufafiti wa Magonjwa ya Binadamu Nchini (NIMR), Kanda ya Ziwa, kutoa tamko la kuwatoa watu hofu kwamba taasisi hiyo haina uhusiano wowote na Freemason. Uvumi wa uhusiano huo ulisababisha wajawazito na kinamama wenye watoto wachanga kukataa kuhudhuria kliniki wakihofia usalama wa maisha yao.
Sasa, tuje kwa neno, “changamoto”. Hili linatumiwa na karibu kila Mtazania, hasa wanasiasa, kama kichaka cha kufisha makali ya mojawapo ya maneno: kikwazo, kipingamizi, kizuizi; kuchanganyikiwa; kutatanisha; kiunzi; mkwamo; utata, shaka mshangao; mtanzuko, kutokuwa na budi, kulazimika kuchagua upende usipende; kutokuwezekana, kutokueleweka; upinzani; shida, ugumu; fumbo, mtihani; tatizo gumu kutatuliwa; kizuizi; tatanishi; isiyothibitika; kukatisha tamaa; kingwangwa, n.k.
Hili neno “changamoto” ni kinyume cha ufafanuzi katika Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Dar es Salaam, toleo la pili, 2004. Kamusi hiyo inafafanua kwamba “Changamoto” ni kama ifuatavyo:” 1. Kitu, hali au jambo linalotia ari 2. Hamu ya kufanya kitu; hamasa.”
ITAENDELEA