Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, amezungumza mambo mazito mno mwishoni mwa wiki. Sehemu ya hotuba yake tumeishapisha neno kwa neno ndani ya gazeti hili.
Miongoni mwa maneno aliyoyazungumza kwa ujasiri ni kiwango cha weledi wa baadhi ya majaji walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete. Lissu amesema baadhi yao wana uelewa mdogo wa sheria, lugha ya Kiingereza na kwamba wapo wanaoshindwa kuandika hukumu kutokana na uduni wa weledi wao katika tasnia ya sheria.
Lissu amezungumzia uteuzi wa wakuu wa wilaya na mikoa ambao ni wabunge, na wakuu wa wilaya na mikoa ambao ni wanajeshi. Aidha, amezungumza pia kuhusu kuwapo kwa mkuu wa wilaya aliyeteuliwa juzi licha ya Mahakama Kuu kuwahi kumvua ubunge kutokana na kumtia hatiani kwa makosa ya ubaguzi.
Wakati Lissu akisoma hotuba hiyo, wabunge kadhaa wa CCM akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walionekana kukerwa na hata kumtaka mbunge huyo machachari afute baadhi ya maneno. Lissu aligoma na suala hilo sasa limepelekwa kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki na Madaraka.
Kilicho wazi ni kwamba Lissu ameibua jambo ambalo si wanasiasa wote – hasa wa CCM – ambao wangeweza kuliibua. Kuandamwa kwake wakati na baada ya kusoma hotuba yake kunaashiria unyeti wa suala hilo. Kwa upande wetu tunaona kuwa Lissu ana hoja. Ameibua jambo ambalo kwa watu weledi wanachoweza kukifanya ni kulijadili kwa lengo la kulipatia ufumbuzi.
Kama kweli kuna majaji ambao hawana uwezo, hili si jambo la kificho wala la kudhani kuwa linaweza kuhatarisha usalama wa mhimili wa Mahakama. Kilichofanywa na Lissu kinapaswa kutufumbua macho ili kuona ni kwa namna gani tunaweza kuondokana na aibu hiyo – kama kweli ipo.
Pili, suala la uteuzi wa wakuu wa wilaya na mikoa ambao ni wabunge, kwa hakika ni ukiukwaji wa sheria za nchi. Haiingii akilini kuona mbunge huyo huyo akiwa na dhima ya kuikosoa Serikali, anakuwa sehemu ya serikali. Hatuoni ni kwa namna gani mbunge ambaye ni mkuu wa wilaya au mkoa, anaweza kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba watu hawa wanateuliwa huku Tanzania ikiwa na mamilioni ya wasomi wanaoweza kushika nafasi hizo. Kama si takrima, kuna siri gani ya kumrundikia mtu mmoja vyeo vingi? Aidha, suala la kumteua mtu mbaguzi, mnyanyasaji na mleta utengano ndani ya jamii kuwa mkuu wa wilaya, kuna maana gani?
Kwa haya na mengine mengi aliyoyazungumza Lissu, tunasema Serikali na mamlaka nyingine zisizomoke kumwandama Lissu. Tunahiari kukubaliana na Serikali endapo hayo aliyoyasema yatabainika kuwa ni ya uongo; jambo ambalo tunadhani haliwezi kutokea.
Kwa mara nyingine tunampongeza Lissu kwa ujasiri wa kuweza kuzungumza mambo ambayo wanasiasa wengi ‘wanafiki’ huogopa kuyasema. Tusiwe na kasumba ya kuamini kuwa kila linalozungumzwa na wapinzani ni baya. Hili la Lissu tunaamini lina mashiko na linapaswa kufanyiwa kazi, na si kumtisha au kumkatisha tamaa.