Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Bodi Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Zuhura Muro amesema kutokana na dunia ya sasa ipo kidjitali imewezesha TTCL kupiga hatua katika kutoa huduma mbalimbali.

Amesema kwa sasa TTCL imekuja na huduma mpya ya T-CAFE ambayo itahusisha kufunga mtandao wa bure katika maeneo yenye mikusanyiko wa watu ikiwemo vyuo, vituo vya treni, viwanja vya ndege na mabasi.

Ameyasema hayo leo Julai 03, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea banda la TTCL katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

“Kwa sasa TTCL tumekuja na bidhaa mpya ya Public WIFI inayoitwa T-CAFE ambayo tunaipeleka katika vyuo, vituo vya treni, vituo vya mabasi, Viwanja vya Ndege na maeneo mbalimbali yenye mkusanyiko wa watu ambapo wakati unafurahia na WIFI ya bure unapata huduma ya chai, vitafunwa na huduma nyingine. Hii pia itasaidia kuileta jamii pamoja na kuchangamana na kuzungumza,” amesema.

Aidha amesema katika kusapoti Royal Tour tayari wameshapeleka mawasiliano yenye kasi juu ya Mlima Kilimanjaro na takwimu zinaoesha watalii zaidi ya 9000 wameshajiunga na WIFI yao.

“Kutokana na huduma hiyo tumeongeza usalama kwa wapanda mlima, ambapo wanaweza kupanda wakiamini kwamba lolote litakalotokea wanaweza wakapata mawasiliano ya haraka,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wao katika maonesho hayo amesema ushiriki unaenda sambamba na kauli mbiu inayosema ‘Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji’.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua milango mingi na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuvutia uwekezaji,TTCL tuna wajibu mkubwa sana kwa sababu katika karne hii hakuna biashara iliyosimama kama hauna maunganisho ya kidigitali,” amesema.

Ameongeza kuwa kukuza huduma za kidigitali ni maendeleo yaliyopo katika Shirika hilo kwani linaweza kuwa muhimili mkubwa katika kuhifadhi data za wafanyabiashara hata wale wa kati ambapo data zitakuwa salama.

“TTCL ni Kituo Kikuu cha Data ambacho kinaunganisha vituo yao vyote katika nchi na kwa mashirikiano mazuri ambayo wamekuwa nayo, wanahakikisha data za wateja wao zitakwenda vizuri umeme utakuwepo na wananchi wanataweza kuzipata,” alisema.

Amesema TTCL pia inatoa huduma ya call center kwa ajili ya mashirika mbalimbali na wafanyabiashara mbalimbali badala ya mashirika kuingia gharama sisi tunauwezo kwa sababu tunamajengo na Teknolojia na wataalamu wa kuendesha vituo vya kupigia simu(call center).